Halima Mdee: Hatuondoki Chadema, tunakata rufaa

chadema

Wabunge 19 wa viti maalum waliovuliwa uanachama wa chama cha upinzani Chadema, wamesema wataendelea kuwa 'wanachama wa hiari' wa chama hicho huku wakipanga kukata rufaa juu ya adhabu walopewa.

Viongozi hao 19 hii leo wakiongozwa na Bi Halima Mdee wamesema kuwa baada ya kuvuliwa uanachama na Kamati Kuu, sasa wataenda ngazi ya juu kimaamuzi, Halmashauri Kuu, ili kukata rufaa.

Hata hivyo, Bi Mdee aligoma kujibu maswali ya waandishi juu ya hoja mbili za msingi wa sakata la kufukuzwa kwao akisema ndio hoja pia za rufaa yao.

Hoja hizo ni nani aliyepeleka majina yao Tume ya Uchaguzi ya Tanzania (NEC) na nani aliyewapa idhini ya kula kiapo cha ubunge.

esther

Chadema ilipata mbunge mmoja wa jimbo katika uchaguli uliopita, hata hivyo ilikidhi vigezo vya kuteua wabunge 19 wa viti maalum.

Hata hivyo chama hicho kinapinga matokeo ya uchaguzi.

Kwa mujibu wa uongozi wa Chadema, Katibu Mkuu wa chama John Mnyika hakuwasilisha majina ya wateule wa viti maalum NEC, na hawakutoa idhini ya kada yoyote kuapa Bungeni.

Maelezo ya video, Mgogoro Chadema: Halima Mdee asema hajanunuliwa

"Siwezi kujibu hapa juu ya hoja hizo mbili kuhusu mchakato wa kupatikana kwetu. Hoja hizo ndiyo msingi wa rufaa yetu, hivyo siwezi kujadili kesi yetu na vyombo vya habari kabla hatujaipeeka katika mamlaka husika, Baraza Kuu..." Mdee pia amehoji juu ya kuzuiliwa wabunge wa viti maalumu:

"... kuanzia 2010 hakuna uchaguzi tulioukubali, sababu chaguzi zote kulikuwa na udanganyifu, 2010, 2015 kote kulikuwa na udanganyifu lakini wabunge lakini wabunge walienda...kwanini 2020 wasiende?

Tunavyozungumza madiwani (wa Chadema) wanaapa, mbunge aliyechaguliwa ameapa.

m

Mimi naamini suala si kwenda au kutokwenda, wala usishangae iwe kesho au keshokutwa iwe sisi ama wengine wataenda kwa kuwa si jambo jipya."

Kwa mujibu wa Bi Mdee, hawakutokea katika kikao kilichochukua uamuzi dhidi yao kwa kuwa walihofia usalama wao pamoja na kujiepusha na maamuzi ya jazba.

"Kulikuwa na uhamasishaji wa hali ya juu mitandaoni uliofanywa na baadhi ya viongozi wa juu wakitaka wanachama wajitokeze ili kutushughulikia... Pili, pande zote mbili kulikuwa na hasira, tuliamini maamuzi yangefikiwa kwa jazba...tuliomba kuahirishwa kwa kikao cha Kamati Kuu kwa wiki moja lakini tukakataliwa. Hivyo, tuliona nio busara zaidi kutokuhudhuria," ameeleza Mdee.

Spika awakingia kifua

n

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amewaapisha wabunge wateule Bw. Humphrey Polepole na Bi. Riziki Said Lulida kuwa wabunge kamili , na kutoa onyo kwa wale wanaodharau na kukebehi shughuli za Bunge.

Bw. Humphrey polepole alikuwa Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza baada ya kuwaapisha wabunge wateule, Spika Ndugai amekemea vikali watu wanaodharau shughuli zinazofanywa na Bunge la Tanzania

"Wako rafiki zetu ambao hivi karibuni wamejipambanua kwa kukejeli shughuli za bunge, niwatahadharishe na kuwakumbusha labda wamesahau kuwa ni jambo lisilokubalika kwa mtu yoyote, kudharau shughuli za bunge, kudhalilisha bunge, kudhalilisha uongozi wa bunge na hata kudhalilisha wabunge waliokwisha kuapishwa.

Amesema maboresho ya kanuni inayosimamia kiapo yanamuwezesha mbunge mpya kutekeleza kazi za kibunge na kuwajibika kwa wananchi mara tu baada ya kuchaguliwa kwake au kuteuliwa kwake.

Kwa utaratibu wa zamani, Ndugai amesema ilibidi wateuliwa hao wakae bila kufanya kazi za kibunge, hadi Februari 2 mwaka 2021, lakini kwa mabadiliko haya yaliyofanyika kwenye bunge lililopita yanawawezesha sasa baada ya kula kiapo kuanza kufanya kazi moja kwa moja kama ilivyo kwa wabunge wengine wote walioapishwa tangu kuanza kwa bunge la 12.

''Shughuli za bunge huwa hazisimami ndio maana wabunge huchaguliwa kwa miaka mitano. Hakuna muda ambao mbunge yuko likizo au bunge kuwa likizo, hakuna''. Alisema Spika Ndugai.

Je, Chadema ilifikia vipi uamuzi wa kuwafukuza?

mbowe

Baada ya uchaguzi wa Oktoba 2020 kuisha, vyama vikuu vya upinzani nchini Tanzania vimejikuta katika njia panda ya kisiasa, si upande wa Tanzania Bara pekee, hadi Zanzibar.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kulikuwa na kitendawili cha ikiwa wapeleke majina ya Wabunge wa viti maalum ama la.

Kitendawili hiki kilikuwa na jawabu tofauti kutoka kwa wafuasi wa chama hicho na wachambuzi wa siasa.

Mambo yaligeuka baada ya kundi la Wabunge 19 wanawake kutoka Chadema kufanya uamuzi wenye utata wa kwenda Bungeni na kuapishwa na Spika Job Ndugai, kuwa wabunge wa Bunge la 12.

Siutofahamu sasa imekuwa kati ya uongozi wa juu wa chama hicho wakiungwa mkono na sehemu kubwa ya wafuasi wa chama dhidi ya wabunge 19. Bado mambo yako moto.

Mbowe alisema kamati kuu iliyoketi, imeona na imeridhishwa na ukweli kwamba kuna ukiukaji mkubwa wa katiba ya nchi , sheria za nchi na kanuni zinazosimamia masuala ya uchaguzi zilizokiukwa katika mchakato mzima wa uchaguzi huo hususani katika jambo zima linalohusu viti maalum.

''Tumejiridhisha katika uvunjaji huu wa katiba, sheria na kanuni kama kamati kuu ya chama cha upinzani Chadema, lazima tulifahamishe taifa baada ya kujiridhisha sisi wenyewe baada ya vikao vya ndani va chama kuhusu mapungufu kadhaa yaliyofanyika katika mchakato huu.''

Mbowe ameainisha Mapungufu ya kisheria aliyosema yako dhahiri katika mchakato wa uteuzi wa wabunge wa viti maalumu

Ibara ya 78 (3) inasema majina ya watu waliopendekezwa na tume ya uchaguzi yatatangazwa kama matokeo ya uchaguzi, baada ya tume ya uchaguzi kuridhika kwamba masharti na sheria vimezingatiwa.

Ibara ya 67 (1b) imeweka masharti na sifa ya mtu kuteuliwa kuwa mbunge kuwa lazima awe amependekezwa na chama cha siasa.

Mbowe amesema kuwa huwezi kupendekezwa na chochote kingine kwa mujibu wa sheria za nchi , isipokuwa na chama cha siasa.

Hivyo Mbowe amesema kuwa chama chao hakijateua wabunge, na kuwa hawajui mchakato huo ulivyokwenda.

''Tunaona watu wetu wanaapishwa, hatuwajui, fomu zinazopaswa kujazwa na kuletwa kwenye chama, ili katibu mkuu wa chama chetu aweze kuziidhinisha, hatujawahi kuzijaza, fomu ziko ofisini, tunaona wabunge wetu wanaapishwa''.

Mbowe alitangaza kuwafuta uanachama wabunge hao wateule na kuwavua nyadhifa zao zote ndani ya chama.

Kwa upande wa viongozi ndani ya kundi hilo la watu 19 ''Kamati imeona hawana sifa hata moja kuendelea kushika nafasi yoyote ya uongozi wa chama hiki kwa mazingira haya, kwa hiyo tumewavua mamlaka yote katika chama''. alisema Mbowe

Je, ni akina nani waliofukuzwa?

halima

Chanzo cha picha, Getty Images

  • Halima Mdee
  • Esther Matiko
  • Grace Tendega
  • Cecilia Pareso
  • Ester Bulaya
  • Agnes Lambart
  • Nusrat Hanje
  • Jesca Kishoa
  • Hawa Mwaifunga
  • Tunza Malapo
  • Asia Mohammed
  • Felister Njau
  • Naghenjwa Kaboyoka
  • Sophia Mwakagenda
  • Kunti Majala
  • Stella Flao
  • Anatropia Theonest
  • Salome Makamba
  • Conchesta Rwamlaza