Halima Aden: Mwanamitindo wa Marekani awacha kazi yake kutokana na sababu za kidini

Halima Aden

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Halima Aden akiwa katika maonesho ya fesheni ya Milan
Muda wa kusoma: Dakika 2

Mwanamitindo wa Marekani Halima Aden anasema anaacha kazi ya kuwa mwanamitindo kwasababu inaenda kinyume na maadili ya dini yake.

Mwanamitindo huyo, 23, amewahi kuangaziwa katika majarida ya urembo ya kimataifa kama British Vogue, Vogue Arabia and Allure.

Akiandika kwenye mtandao wake wa Instagram, alisema virusi vya janga la corona vimempa fursa ya kufikiria tena kuhusu maadili yake kama mwanamke wa Kiislamu.

"Kuwa 'Muislamu' ni safari ndefu yenye panda shuka zake," alisema.

Akizungumzia kukubali kazi za uanamtindo ambayo ilienda kinyume na maadili ya dini yake, alisema: "Naweza tu kujilaumu kwa kujifikiria zaidi kuliko kile hasa kilichokuwa hatarini."

Aliongeza kuwa tatizo lilianza kwa kuwa na "ukosefu wa wanawake wa Kiislamu wanamitindo" ndani ya tasnia hiyo ambao wanaweza kuelewa umuhimu wa kuvaa hijab.

Halima Aden aliungwa mkono katika mtandao wa kijamii kutoka kwa kina dada wanamitindo Bella na Digi na pia kutoka kwa Rihanna.

Halima alizaliwa katika kambi ya wakambizi nchini Kenya na wazazi Wasomali kabla ya kuhamia Marekani akiwa na umri wa miaka 6.

Alitambuliwa na shirika la mitindo la kimataifa la IMG Models akiwa na umri wa miaka 18 baada ya kushiriki shindano la urembo Marekani la kumtafuta Miss Minnesota ambako alifika nusu fainali.

Alikuwa mwanamke wa kwanza mweusi kuvaa hijab katika shindano la urembo na ndani ya kipindi kifupi akawa maarufu kwa mavazi yake ya kipekee katika vipindi maarufu vya fasheni duniani vya kila wiki.

Ameendelea hadi kuwa nyota katika kampeni za maonesho ya urembo kwa kampuni ya Fenty ya Rihanna, na Yeezy ya Kanye.

Katika simulizi yake Instagram, alimsifu Rihanna kwa kumruhusu kuvaa hijab wakati akiwa kazini.

Anasema mara nyingi alihatarisha dini yake kama sehemu ya kazi yake - ikiwemo kukosa kusali kwa muda stahiki kulingana na dini ya Kiislamu au kukubali kufanya maonesho ya urembo bila kuvaa hijabu na hata kutumia kitu kingine kufunika kichwa chake.

Aliongeza kuwa alianza "kulia" akiwa kwenye chumba chake cha baada ya kumaliza kufanya video ya kampeni ya kutozungumza kuhusu kile unachohisi ni sawa.

"Ukweli ni kwamba sikuwa sawa kabisa," ameandika kwenye mtandao wa Instagram.

"Huyu sio mimi kabisa," aliongeza.

Halima Aden

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Halima, akishiriki maonesho ya uanamitindo ya Tommy Hilfiger, mjini New York

Februari mwaka huu, aliiambaia BBC kuwa: "Maadili sio kwa utamaduni mmoja, sio kwa kundi moja la wanawake. Badala yake ni utamaduni ambao umekuwepo tangu jadi.

"Umekuwepo tangu mwanzo. Na utakuwepo kwa miaka 100 ijayo. Ni chaguo, chaguo lingine la kuamua kama unataka kuwa miongoni mwao."