Afisa wa kike aliyevamiwa na kupoteza uwezo wake wa kuona milele

Khatira during an interview with the BBC
Maelezo ya picha, Khatira alishambuliwa baada ya kumaliza zamu yake kazini ya afisa polisi, mjini Ghazni

Kama afisa wa kike nchini Afghanistan, Khatira alijua kwamba anakabiliwa na hatari.

Lakini kile alichopitia kwasababu ya kulinda nchi yake kilikuwa kikubwa mno - na kilitokea ghafla.

Alikuwa tu amemaliza zamu yake kazini na sasa anarejea nyumbani katikati ya mji huko Ghazni, wakati wanaume wawili waliokuwa kwenye pikipiki na mmoja anayetembea kwa miguu walipomvamia.

"Aliyekuwa anatembea kwa miguu alisema kwa sauti ya juu, 'Mpige risasi!'" Khatira ameiambia BBC. "Siwajui. Walinivamia nikiwa tu karibu na nyumba yangu."

Afisa aliangushwa chini na akaanguka kifudifudi. Alijipata akiwa hospitali na majeraha ya uso.

"Nilihisi maumivu na sikuweza kuona. Daktari alisema macho yangu yamepata majeraha na hivyo basi sikuweza kuyafungua" anasema.

Aliagizwa kurejea kwa uchunguzi zaidi baada ya mwezi mmoja.

Alipofanya hivyo aligundua kwamba hatakuwa na uwezo wakuona milele.

'Propaganda za vita'

Female officers in Afghanistan

Chanzo cha picha, Afghan Ministry of Interior

Uhalifu huo ulitekelezwa miezi minne iliyopita lakini sasa hivi ndio suala hilo limapata angalizo kutoka kwa serikali.

Waziri wa mambo ya ndani wa Afghan, Masoud Andarabi, alikutana na Khatira Oktoba 6 na kumuahidi nyumba na usaidizi wa matibabu.

Pia alishtumu kundi la Taliban kwa kutekeleza uhalifu, amezungumza kwenye mtandao wa Twitter: "Kundi la Taliban haliwezi kuvunja taifa hili kwa nguvu."

Kundi la Taliban limekanusha kuhusika na shambulio hilo.

Lakini katika nchi ambayo inakabiliana na utamaduni na usasa, mgogoro wake ni zaidi ya siasa, amesema Meena Baktash, mhariri wa idhaa ya BBC Afghan.

"Serikali ya Afghan imeshtumu kundi la Taliban huku Taliban wakinanusha madai hayo. Na wakati huohuo, hakuna anayejali kuhusu waliojeruhiwa, umaskini, na kurudi nyuma sana kimaendeleo kwa jamii ya Afghan, utamaduni na haki za wanawake," amesema.

Bi. Baktash anasema simulizi kama za Khatira "zinatumiwa katika propaganda za vita" kati ya serikali na kundi la Taliban.

Simulizi ya Khatira haikugonga vichwa vya habari wakati inatokea - lakini ilikuwa ni baada ya kuhojiwa na BBC na kuomba Waziri wa mambo ya ndani kuzungumzia suala hilo.

"Kila siku, makumi ya wasichana ni waathirika wa unyanyasaji. Pua zao zinakatwa, masikio yao yanakatwa, wanapigwa na kuteswa," Mhariri wa BBC Afghan amesema.

"Kuna simulizi nyingi za vijana zinazoonesha alama za vipande vya sigara kwenye miguu na mikono yao, lakini hawakugonga vichwa vya habari."

Eneo hatari kwa wanawake

Female officers in Afghanistan

Shirika la Oxfam limesema Afghanistan ni moja ya eneo hatari zaidi kwa wanawake.

Maafisa wa kike wa polisi wanatengwa na kuuawa kwasababu tu ya kufanya kazi zao, shirika hilo limesema.

Mashambulizi yanayolenga maafisa wanawake yamekuwa yakiongezeka hivi karibuni katika mikoa ya Ghazni, Kunduz na Kabul.

Lakini mhariri wa shirika la BBC Afghan anasema uhalifu huo unapewa angalizo kidogo labda pengine tukio liishie kuangaziwa na chombo cha habari.

"Serikali imelaumu kundi la Taliban, lakini wakati huohuo, haijatambua kwamba inaonesha kushindwa kulinda waathirika," amesema Bi. Baktash.

Baba yake Khatira tangu wakati huo amekamatwa na kushtakiwa kuagiza kutekelezwa kwa uhalifu. Binti huyo anasema walikuwa wamekosana kwasababu hakutaka afanyekazi.

Bwana Andarabi alimshtumu baba huyo kwa kuwa mwanachama wa Taliban lakini polisi imesema Ghazni ni raia tu wa kawaida.

Baada ya kuwa hospitali ya Kabul, Khaitira alirejea Ghazni.

Khatira during an interview with the BBC

Licha ya vionda vyake, Khatira anasema anataka kuendelea na kazi yake. Lakini mamlaka inasita.

"Waliniambia, Wewe umepoteza uwezo wako wa kuona, huwezi kufanya kazi. Unastahili kustaafu.' Nikakataa."

Amedhamiria kurejea kufanyakazi yake ya afisa wa polisi ikiwa atapata matibabu na kupona.

"Azma yangu kubwa ni kurejea kwa kazi yangu," Khatira anasema. "kujithibitisha, kufanikiwa jambo langu na kuhudumia nchi yangu."