WHO yataka uchunguzi dhidi ya wafanyakazi wake kuhusu madai ya ngono ufanyike

Chanzo cha picha, Thomson Reuters Foundation
Shirika la afya duniani WHO limetaka uchunguzi ufanyika kuhusu shutuma kuwa wafanyakazi wa afya waliokuwa wakisaidia mapambano dhidi ya mlipuko wa Ebola nchini DRC waliwadhalilisha kingono na kuwanyanyasa wanawake.
WHO na wafanyakazi wa mashirika mengine ya misaada walishutumiwa na wanawake 50 katika uchunguzi wa pamoja wa mashirika mawili ya habari.
Wanawake walipewa vinywaji, ''walivamiwa'' kwenye hospitali, wakishurutishwa kufanya ngono, na wanawake wawili wakapata ujauzito.
Shutuma hizo zimeelekezwa katika matukio ya mwaka 2018 na mwezi Machi mwaka huu.
Shirika la habari linalotangaza masuala ya haki za binadamu na shirika la the Thomson Reuters yamefanya uchunguzi wa karibu mwaka mzima.
WHO imesema kuwa shutuma hizo zitafanyiwa uchunguzi wa kina.
''Yeyote atakayebainika kuhusika atawajibishwa ikiwemo kuchukuliwa hatua mara moja ya kufukuzwa, ilisema taarifa hiyo.
Zaidi ya watu 2,000 walipoteza maisha kutokana na mlipuko wa Ebola nchini DRC.
WHO, ambayo inaongoza jitihada kimataifa kupambana na kuenea kwa mlipuko huo, lilitangaza mwezi Juni mwaka huu kuwa ugonjwa huo umekwisha nchini humo.
UN na mashirika ya misaada hapo awali yaliahidi kutovumilia kabisa unyanyasaji wa kijinsia kufuatia madai kama hayo dhidi ya wafanyikazi wao katika nchi nyingine.
Msemaji wa Ofisi ya Mambo ya nje, wa Jumuiya ya Madola na Maendeleo amesema itachunguza matokeo ya WHO kwa karibu, akiongeza: "Unyanyasaji wa kijinsia na unyanyasaji ni chukizo kabisa. Mara kwa mara tunatathmini washirika wetu wote kuona wanafuata kanuni za kiusalama.
Je! Ni nani anayehusika zaidi na uchunguzi?
Madai mengi ya unyanyasaji wa kijinsia na unyanyasaji yalikuwa dhidi ya wanaume, wakiwemo madaktari, wanaodaiwa kuwa wa WHO.
Takribani wanawake 30 walitoa madai dhidi yao, vyombo vya habari viliripoti.
Idadi kubwa zaidi ya madai - iliyotolewa na wanawake wanane - ilikuwa dhidi ya wanaume wanaosemekana wanaotoka wizara ya afya ya DR Congo
Mashirika mengine mawili ya UN, na mashirika manne ya misaada ya kimataifa, pia yametajwa kwenye ripoti.

Chanzo cha picha, Thomson Reuters Foundation
Baadhi ya watuhumiwa walitoka Ubelgiji, Burkina Faso, Canada, Ufaransa, Guinea-Conakry na Ivory Coast.
Wanaume wengi walikataa kuvaa kondomu, na takribani wanawake wawili walisema walipata ujauzito kutokana na dhuluma hiyo, vyombo vya habari viliripoti.
Wanawake walisema nini zaidi?
Mfanya usafi mwenye umri wa miaka 25 alinukuliwa akisema kwamba alialikwa nyumbani kwa daktari wa WHO kuzungumzia kupandishwa cheo.
"Alifunga mlango na kuniambia:''. Tunahitaji kufanya ngono sasa hivi' "mwanamke huyo alisema.
"Alianza kunivua nguo. Nilirudi nyuma lakini alijilazimisha dhidi yangu na kuendelea kunivua nguo. Nilianza kulia na kumwambia aache ... Hakuacha. Kwa hivyo nikafungua mlango na kukimbia nje. "

Chanzo cha picha, EPA
Katika kisa kingine, aliyenusurika na Ebola mwenye umri wa miaka 32 aliyaambia mashirika ya habari kwamba alialikwa hotelini kwa ushauri.
Katika chumba alipewa kinywaji laini. Alisema aliamka saa kadhaa baadaye, akiwa utupu na peke yake katika chumba cha hoteli, na anaamini alibakwa.
Kwanini wanawake wananyanyaswa kingono?
Wanawake wengi walisema walilazimishwa kufanya mapenzi ili kupewa kazi, na mmoja akielezea kama "pasipoti ya ajira" na mwingine akasema "wanakuajiri kwa mboni za macho".
Wanawake walisema walifikiliwa nje ya maduka makubwa katika mashariki mwa jiji la Beni, vituo vya kuajiri kazi, na hospitali ambapo orodha za watahiniwa waliofaulu zilichapishwa.
Vyombo vya habari pia vilimnukuu mwanamke mmoja akisema kwamba "tabia ya wanaume kudai ngono imekuwa ya kawaida sana na ndiyo njia pekee ya kupata kazi".

Hatari kubwa ya kupoteza heshima
Uchambuzi wa Imogen Foulkes, BBC News, Geneva
WHO imetumia mwaka huu kupambana na janga la Covid-19, katikati ya uhasama wa wazi kutoka kwa Marekani, ambayo imetangaza itaacha kujihusisha na WHO kutokana na madai kwamba shirika hilo liko karibu sana na China.
Sasa zimekuja shutuma nzito.
Uwezekano wa kuharibu heshima yake unaoweza kujitokeza ni mkubwa na WHO imejibu haraka, ikiahidi uchunguzi wa haraka.
Ni zaidi ya miaka miwili tangu mashirika ya misaada ya kibinadamu kukabiliana na shutuma za unyanyasaji wa kijinsia zinazohusisha wafanyikazi wa Oxfam nchini Haiti zilipoenea hivi karibuni na kujumuisha mashirika kadhaa.
Wote, pamoja na WHO, waliahidi kutovumilia unyanyasaji huo, mafunzo mazito zaidi kwa wafanyikazi na mifumo sahihi ya waathiriwa kuripoti.
Kwa kuzingatia madai hayo kutoka DR Congo, haionekani kuwa mafunzo ya wafanyakazi au mfumo wa utoaji wa taarifa ulifanya kazi.
Hadi sasa kukosolewa kwa WHO kumetokana sana na Marekani, na shirika limefarijika na msaada wa kisaikolojia kwa waathirika na wa fedha, kutoka nchi nyingine nyingi.













