Jinsi familia tatu za Kenya zilivyotawala siasa za Kenya, je kutakuwa na mabadiliko?

Raila Odinga (kulia) amekuwa akikataa kumtambua Uhuru Kenyatta kama rais halali wa Kenya

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Raila Odinga (kulia) na Uhuru Kenyatta (kushoto)
    • Author, Uchambuzi na, Profesa Hezron Mogambi,
    • Nafasi, Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi

Siasa za nchi ya Kenya-kwa miaka mingi tangu Kenya kupata uhuru wake mwaka wa 1963 - zimekuwa zikizunguka sifa na taswira ya familia mbili- familia ya Kenyatta na ile ya Odinga.

Daniel arap Moi, aliyekuwa rais wa pili wa Kenya, alikuwa rais aliyekaa mamlakani kwa muda mrefu zaidi - miaka 24, na rais wa tatu, Mwai Kibaki ambaye alikuwa mamlakani kati ya 2002-2013, lakini unapofuatilia hisia na siasa za Kenya, taswira inayotawala ni kati ya familia mbili-ile ya Kenyatta na ile ya Odinga.

Ikumbukwe kwamba Mzee Jomo Kenyatta na Jaramogi Oginga Odinga walianza kutawala siasa za Kenya hata kabla ya nchi ya Kenya kupata uhuru. Wawili hawa walikuwa viongozi shupavu wa jamii zao- Kenyatta akiiongoza jamii ya Agikuyu na Odinga akiongoza jamii ya Luo.

Wanasiasa hawa wawili walifanya kazi kwa bidii bila woga kuwezesha jamii zao na kuzikinga dhidi ya unyanyasaji wa wakoloni huku wakiwa wamependwa na kutajika katika jamii zao kama viongozi shupavu na wakombazi.

Mzee Jomo Kenyatta na Jaramogi Oginga Odinga walikuwa mashuhuri nchini Kenya katika harakati na mapambano ya kupigania uhuru wa Kenya na walivutia uungwaji mkono kutoka kwa viongozi wengine mashuhuri nchini Kenya katika harakati za ukombozi.

Hata hivyo, mambo yalibadilika baada ya uhuru. Katika kitabu chake, Not yet Uhuru, Odinga anaeleza kuwa kwa Wakenya wengi, uhuru ulikuwa bado haujapatikana kwa sababu mkoloni mpya alikuwa amechukua nafasi ya mwingine.

Kilichofuatia baada ya uhuru ni kujiuzulu kwa Odinga kutoka serikali ya Kenyatta na hatua za kisiasa zilizofuata zilikuwa ni mabishano makali ya kihistoria baina ya familia hizi mbili mashuhuri nchini Kenya kwa miongo takriban mitano.

Daniel Moi alipotarajiwa kumrithi Jomo Kenyatta

Moi

Uhusiano baina ya Mzee Kenyatta na Oginga Odinga haukuwa mzuri kisiasa.

Miaka miwili kabla ya kifo cha rais wa kwanza wa Kenya, Jomo Kenyatta, mnamo Agosti 1978, na baada ya uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali wa mwaka wa 1974, kinyang'anyiro kilifikia kilele, huku washidani wakibishana na kutupiana maneno kwenye mikutano ya hadhara kuwaonya wananchi wa Kenya dhidi ya hatari za uwezekano wa Daniel arap Moi kumrithi Jomo Kenyatta.

Kikundi hiki kilitaka katiba kubadilishwa ili makamu wa rais asiwe na uwezo wa kumrithi rais iwapo rais atakufa, mabadiliko ambayo hayangemruhusu Moi kumrithi Jomo Kenyatta.

Moi alitoka kabila la Wakalenjin kutoka Baringo na kikundi kilichofahamika kama "Kiambu Mafia" kilimdharau na hakikuweza kuwaza uwezekano wa Moi kuwa rais wa Kenya.

Baada ya hapo, yeye pamoja na mtoto wake, Raila, walishutumiwa kwa makosa ya kila aina, kutupwa kuzuizini, kuzuiliwa nyumbani, na kuzuiliwa kuzungumza kwenye hadhara ama kuandaa mikutano na shutuma nyingine nyingi zikiwafuata.

Hatimaye, Jomo Kenyatta alimteua Daniel arap Moi kuwa makamu wake na kuonyesha ni nani aliyemtaka kama mrithi. Moi, aliyetoka kwenye jamii iliyoonekana ndogo- Kalenjin- wakati huo, alionekana kama chaguo zuri na kama ngazi ya kuleta jamii pamoja baina ya makundi mbali mbali.

Uhusiano baina ya faimilia ya Odinga na ile ya Kenyatta haukuweza kuwa mzuri kisiasa.

Baada ya Daniel Moi kuchukua hatamu za uongozi aliendeleza sera za Mzee Kenyatta kisiasa na kuitenga familia ya Odinga.

Raila Odinga na babake, Jaramogi, walitajwa kwenye jaribio la kuipindua serikali ya Kenya lililofanyika mwaka wa 1982 ambalo halikufaulu.

Raila alizuiliwa kwa miaka sita bila kufikishwa mahakamani lakini aliachiliwa mwaka wa 1989.

Hata hivyo, Raila alifungwa tena karibu mwaka mmoja baadaye, wakati huu, pamoja na wakereketwa wengine wa kupigania mfumo wa vyama vingine kama vile Kenneth Matiba na Charles Rubia.

Aliachiliwa mwaka wa 1991 na akatorokea Norway, akihofia maisha yake.

Mfumo wa vyama vingi

Mudavadi, Odinga na Musyoka Agosti 16, 2017

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images

Baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini Kenya, Raila Odinga alirudi Kenya na kujiunga na Forum for the Restoration of Democracy (FORD, wakati huo ikiongozwa na babake, Oginga Odinga).

Kilichofuata baadaye ni msururu wa kushirikiana kwa vyama, miungano, na kuundwa kwa vyama vipya.

Wakati mmoja, kwa mshangao mkubwa, Raila aliungana na Moi na kuunda chama kipya kilichojulikana kama New Kanu. Hali hii ilipelekea baadhi ya wandani wake, wapinzani na wafuasi sugu kumuita mtu ambaye yuko tayari "kulala na shetani" ili kufikia lengo lake la kuwa rais wa Kenya.

Alifanya kazi kama waziri wa kawi katika serikali ya mwisho ya Moi.

Kinachobainika katika historia ya siasa za Kenya, wakati wa hatamu za uongozi wa Moi, familia ya Kenyatta haikujishughulisha na siasa; badala yake ilizingatia shughuli za kuunda mtandao wa biashara.

Uhuru Kenyatta na Daniel Moi

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Marehemu Rais Moi (kulia) alimkuza Rais Uhuru Kenyatta (kushoto) kisiasa

Halafu, bila kutarajiwa, Moi alimteua Uhuru Kenyatta kama mrithi wake. Hili lilifanya wanasiasa wengi kuondoka kwenye chama tawala kwa sababu ya kuhisi kwamba Uhuru Kenyatta alikuwa na ujuzi wa kiwango cha chini katika serikali kuchukua nafasi hii.

Baadaye, Uhuru Kenyatta aliwania Urais kama mgombea kwa tiketi ya Kanu katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2002 dhidi ya Mwai Kibaki, ambaye wakati huo aliungwa mkono na Raila Odinga.

Kenyatta alishindwa vibaya na akawa kiongozi wa upinzani.

Raila Odinga (kushoto) na Rais Mstaafu Mwai Kibaki (kulia)

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Raila Odinga (kulia) na Rais Mstaafu Mwai Kibaki (kushoto)

Hata ingawa alimfanyia kampeni sana Mwai Kibaki hadi kuchaguliwa kuwa Rais, Odinga aliachwa bila wadhifa wowote jambo ambalo lilimuudhi kisiasa na kuona kama aliyechezewa shere.

Kwa sababu hii, Raila Odinga aliondoka na kuunda muungano wa Orange Democratic Movement (ODM).

Lililoshangaza lilifuata; Uhuru Kenyatta ndiye aliyekuwa anamuunga mkono Kibaki dhidi ya Odinga kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2007.

Mwai Kibaki alitawazwa mshindi kwa tofauti ya kura chache, ushindi ambao ulipingwa na chama cha ODM.

Kufuatia haya, fujo zilizuka nchini Kenya; jijini Nairobi na miji mingine na kupelekea vifo vya zaidi ya Wakenya elfu moja na wizi na uharibifu mkubwa wa mali.

Vita na hali ya wasiwasi ilimalizika kutokana na makubaliano baina ya Raila Odinga na Mwai Kibaki ambapo serikali ya muungano iliundwa mwaka wa 2008 huku Mwai Kibaki akiwa rais na Raila Odinga akiwa Waziri Mkuu.

Uhuru Kenyatta alikuwa mojawapo wa watu walioshtakiwa kwenye mahakama ya kimataifa ya ICC kwa kuchochea michafuko nchini Kenya lakini kesi yake haikuendelea kwa ukosefu wa ushahidi na mashahidi.

Kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2013, Kenyatta, ambaye sasa alikuwa kiongozi wa muungano mpya, Jubilee, alishindana na Raila kwa mara nyingine, (wakishirikiana na William Ruto ambaye walikuwa wameshtakiwa naye kwenye mahakama ya ICC) ambaye pia alikuwa ameunda muungano mkubwa, Coalition For Reform and Democracy (CORD).

Uhuru Kenyatta na William Ruto

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Bw Kenyatta na Bw William Ruto waliungana katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2013

Ulikuwa mchuano mkubwa lakini mwishowe, na hata ingawa kulikuwepo na malalamiko kutoka kwa Raila Odinga kuhusiana na uchaguzi huo, Uhuru Kenyatta alitangazwa mshindi katika uchaguzi na kuunda serikali na naibu wake akiwa William Ruto.

Mnamo Machi 9, 2018, rais Uhuru Kenyatta na mpinzani wake mkuu, Raila Odinga, katika hatua ya kushangaza, walijitokeza nje ya jumba la Harambee - makao makuu ya serikali - kutangaza hatua ya kusitisha uhasama wao wa kisiasa na kuamua kushirikiana katika kuendeleza taifa.

Baadaye, Raila, ambaye alikuwa amefanikiwa kufutiliwa mbali kwa ushindi wa rais Kenyatta mnamo Agosti 8, 2017 kwenye Mahakama ya Kilele ya Kenya, na baadaye kutoshiriki kwenye uchaguzi wa rais uliofuta mnamo October 26, 2017, alianza kuzungumzia haja ya kuwa na mabadiliko ya kikatiba.

Hivi ndivyo shughuli za upatanishi baina ya Uhuru Kenyatta na Raila Odinga zilivyoanza baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2017 ambao ulirudiwa kutokana na kufutiliwa mbali na mahakama, na ambao Raila Odinga alikataa kushiriki.

Itakumbukwa kuwa Jopo la Maridhiano nchini Kenya (BBI) liliundwa kutokana na tofauti zilizozuka baina ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga katika uchaguzi mkuu wa Kenya mwaka wa 2017 ambazo zilitishia kuleta utata nchini Kenya.

Baadaye, Rais Uhuru alipoapishwa na kuingia afisini, waliamua kuzika tofauti zao na kukutana mnamo Machi 9, 2018 na kuorodhesha ajenda tisa ambazo walisema ndizo zilizowafanya kuanza kufanya kazi pamoja kwa minajili ya kuboresha Kenya na siasa zake.

Rais Uhuru Kenyatta (mbele kushoto ) na Raila Odinga (mbele katikati) katika uzinduzi wa ripoti ya BBI - Novemba 2019

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Ripoti ya BBI ilizinduliwa kufuatia hisia tofauti

Ajenda za kuundwa kwa Jopo la Maridhiano (BBI) ni pamoja na jinsi ya kumaliza migawanyiko ya kikabila, kuwashirikisha watu wote kuhusu masuala ya utawala na siasa za Kenya, jinsi ya kushughulikia suala la kumaliza uhasama wa kisiasa unaotokea wakati wa uchaguzi mkuu, jinsi ya kuimarisha amani na usalama, kukabiliana na janga la ufisadi, jinsi ya kukabiliana na ukosefu wa maadili ya kitaifa, maswala ya majukumu na haki za raia, maswala ya kuwajibika kwa pamoja na jinsi ya kuendeleza serikali za ugatuzi.

Viongozi hawa wawili wa Kenya wenye ushawishi mkubwa zaidi nchini humo baadaye waliunda kamati ya watu kumi na nne ambao waliandaa mikutano ya umma kwenye majimbo 47 kote nchini Kenya, ili kupokea maoni kuhusu mabadiliko wayatakayo Wakenya.

Kamati hiyo ilikusanya maoni kutoka kwa wakenya wapatao elfu saba na kuandaa ripoti ambayo sasa inaendelea kujadiliwa zaidi na Wakenya ili kuiboresha.

"Wanasema ati BBI ni ya kutafutia Uhuru kazi. Mimi sitaki kazi, nimechoka. Eeeh, BBI ni ya kuhakikisha ya kwamba hakuna Mkenya atamwaga damu tena katika nchi yetu kwa sababu ya siasa. Tuko pamoja?" aliwahi kusema rais wa Kenya Uhuru Kenyatta.

Kuna tetesi kwamba mpango wa mabadiliko ya katiba kutokana na jopo la BBI ni njama ya kuendeleza uongozi wa rais Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga kwenye siasa za Kenya.

Pia, kuna wadadisi wanaodai kuwa kuna njama ya kupitia kwa mchakato huu, kumhusisha mwanawe aliyekuwa rais wa pili wa Kenya Daniel Moi, Gideon Moi, katika serikali ambayo itakuwa na nafasi zaidi kwenye serikali kuu.

Uhuru Kenyatta na Raila Odinga

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Bwana Odinga na Bwana Kenyatta walishikana mikono kama ishara ya kumaliza uhasama wa kisiasa kufuatia uchaguzi wenye utata wa mwaka 2017.

Historia hii ya siasa za Kenya inatufahamisha mambo kadhaa.

Kwanza, kuna mirathi mingi ya kiasa nchini Kenya. Pamoja na kwamba kuna ushindani mkubwa katika siasa za Kenya mara kwa mara ambao unatawaliwa na kuendeshwa na pesa nyingi, ushindani huu huzunguka familia za Kenyatta na Raila Odinga kama ilivyokuwa kwenye uchaguzi mdogo wa mwaka wa 1966.

Aidha, misingi ya jamii ama kabila inaweza kumsukuma muaniaji kwa kiasi fulani lakini si kote.

Mnamo mwaka wa 2013 kwa mfano, Raila Odinga alimshinda mmoja wa washindani wake Musalia Mudavadi katika kura kwenye maeneo ya anakotoka katika jamii ya Luhya.

Hali hii iliwezekana kwa sababau Raila Odinga alionekana kama kiongozi shupavu wa upinzani, na uhusiano wa kisiasa kati ya Mudavadi na Uhuru Kenyatta - uhusiano ambao ulikuwa wa muda mfupi- ulizua maswali kwamba alikuwa mradi wa kisaisa wa Uhuru Kenyatta.

Kwa upande wa Uhuru Kenyatta, pia aliweza kujibadilisha na kuonekana kama kiongozi wa jamii ya Agikuyu hata baada ya kushindwa vibaya kwenye uchaguzi wa mwaka 2002 pia kunaonyesha hili katika siasa za Kenya.

Aidha, kuwa na pesa na raslimali za kufanyia kampeini ni jambo muhimu. Familia za Kenyatta na Odinga ni mojawapo za familia tajiri na ukweli kwamba siasa za Kenya zinasukumwa na uwezo wa kifedha na raslimali kumesaidia familia hizi mbili kuendelea kutawala siasa.

Hii ndio sababu kuna tetesi kwamba Naibu Rais William Ruto (pia ana uwezo mkubwa wa kifedha sasa) ameanza kujitenga na rais Kenyatta na Raila Odinga kujipanga kwa siasa za mwaka wa 2022 ili anyakue Urais nchini Kenya.

Kwa zaidi ya miongo mitano ya siasa na mabadiliko yasiyotarajiwa na wakati mwingine yakitokea yasiyotarajiwa na ya kushangaza, uaminifu na usaliti, ukora, ujanja na mbwembwe za kisiasa, siasa za Kenya bado zinaonyesha kutawaliwa na msingi mmoja: ushindani baina ya familia za Kenyatta na ile ya Raila Odinga.

Je, hali hii itabadilika hivi karibuni?