Patrice Lumumba: Mahakama ya Ubelgiji yasema jino la shujaa huyo wa DRC linapaswa kurudishwa

Chanzo cha picha, AFP
Mahakama mjini Ubelgiji imeamuru kwamba jino lililochukuliwa kutoka kwa maiti ya shujaa wa Uhuru wa taifa la DRC wakati huo ikiitwa Congo Patrice Lumumba linapaswa kurejeshwa kwa familia yao, vyombo vya habari nchini Ubelgiji vimeripoti.
Lumumba aliyekuwa waziri mkuu wa Congo baada ya kujipatia Uhuru kutoka kwa Ubelgiji 1960, aliuawa 1961 baada ya kutekwa na wapiganaji waliotaka kujitenga.
Serikali ya Ubelgiji ilihusika katika kifo chake na mwaka 2002 iliomba msamaha rasmi.
Vitengo vya ujasusi vya Uingereza na Marekani pia vinadaiwa kuhusika.
Jino la Lumumbua linadaiwa kuchukuliwa na afisa wa polisi wa Ubelgiji aliyekuwa anasaidia kuuzika mwili wake , chombo cha habari cha AFP kimeripoti.
Baadaye jino hilo lilichukuliwa na mamlaka ya Ubelgiji , AFP kinaongezea.
Mahakama hiyo ya Ubelgiji ilisema kwamba jino hilo sasa linafaa kupewa mwana wa kike wa Lumumba Juliana Lumumba , ambaye aliandika barua kwa mfalme huyo wa Ubelgiji akiomba lirudishwe, mtandao wa Brussels Times uliripoti.
Kulingana na mtandao huo uamuzi huo wa mahakama siku ya Alhamisi unafuatia uamuzi mwengine wa ofisi ya kiongozoi wa mashtaka wa kijimbo kwamba mabaki ya Lumumba yanaweza kurudishwa kwa familia yake.
Je familia ya Lumumba inasemaje?
Hatua ya Ubelgiji kurudisha jino la Patrice Lumumba kwa familia yake kumepokelewa vyema na familia hiyo.
Mpwa wake Jean Lumumba anasema kwamba familia yake haikumzika kwasababu mwili wake ulitiwa ndani ya tindi kali uangamie.
Lumumba ni shujaa ambaye hakuzikwa , hatua ya mahakama ya Ubelgiji ni njema kujua ukweli, alisema bwana Jean Jacques .
Alisema kwamba wanaume wawili Joseph Okito na Maurice Mpolo ambao waliuawa pamoja na Lumumba pia ni mashujaa wa Congo na kwamba ukweli kuhusu mauaji yake unafaa kufichuliwa.
Mwaka 2000, Gerard Soete, kamishna wa polisi wa zamani nchini Congo akiwa na miaka 80 wakati huo aliambia AFP kwamba alimkatakata Lumumba na wenzake na kuweka miili yao ndani lakini akachukua jino lake.
Bwana Soete alifariki miaka michache baadaye baada ya kutoa ushahidi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Matukio baada ya DR Congo kujipatia Uhuru
- 1960 mwezi Juni: Congo ilijipatia uhuru wake huku Patrice Lumumba akiwa waziri mkuu na Joseph Kasavubu akiwa rais wa kwanza wa taifa hilo.
- 1960 Mwezi Julai: Mwanajeshi muasi Moise Tshombe atangaza eneo la Katanga kuwa huru huku Ubelgiji ikituma jeshi lake kusaidia kuweka amani , lakini wanajeshi hao wanatakiwa kutoingilia masuala ya ndani ya taifa hilo.
- 1960 Septemba: Rais Kasavubu amfuta kazi bwana Lumumba.
- 1961 Februari: Patrice Lumumba auawa na watu wanaoaminika kuungwa mkono na Marekani na Ubelgiji.
- 1961 Agosti: - Vikosi vya Umoja wa Mataifa vyaanza kuwapokonya silaha wanajeshi wa Katanga.
- 1963- Moise Tshombe akubali kumaliza kujitenga kwa Katanga












