Je misuguano ya kisiasa kati ya viongozi wa Afrika mashariki inaathiri vipi utendakazi wa EAC

Chanzo cha picha, IKULU TANZANIA
- Author, Ezekiel Kamwaga
- Nafasi, Mchambuzi
TANGU kufufuliwa kwake takribani miaka 23 iliyopita, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imepitia katika mitihani anuai ya kiuchumi, kiusalama na tofauti za waziwazi baina ya viongozi wa nchi wanachama wake.
Mwaka 2014, Tanzania na Rwanda nusura ziingie vitani kutokana na kupishana kwa mtazamo wa namna ya kushughulika na makundi ya waasi ya taifa hilo lililopitia katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.
Kenya na Uganda zimewahi kutunushiana misuli kutokana na suala la umiliki wa visiwa vya Migingo vilivyoko ndani ya Ziwa Victoria. Rwanda na Burundi zilikaribia kuingia vitani kati ya mwaka 2017 na 2018 kutokana na tofauti za watawala wa nchi hizo.
Mwanachama mpya wa EAC, Sudan Kusini, alikaribia kuingia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe miaka miwili iliyopita. Hata sasa, watawala wa taifa hilo bado wanatafuta namna ya kuponyesha majeraha ya vidonda vya mgogoro huo wa miaka miwili iliyopita.
Kenya na Tanzania zitabaki kuwa Kenya na Tanzania. Kwa takribani miaka 40 sasa, kumekuwa na malumbano na kurushiana maneno makali baina ya mataifa haya; ingawa yamebaki kuwa maneno tu kwa sababu hakujawahi kuwa na wakati ambao migogoro hiyo ilitishia kuziingiza katika migogoro ya kijeshi.
Hata hivyo, EAC sasa ina mgogoro mkubwa wa kiuchumi ambao unatishia uwepo wake. Hadi Julai mwaka huu, wabunge na watumishi wa Jumuiya walikuwa wakidai mishahara na marupurupu yao inayodaiwa kufika miezi minne kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari.
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kutoka Kenya, Abdulkadir Omar Aden, aliliambia gazeti la The Citizen la Tanzania wiki iliyopita kwamba; "EAC inapita katika nyakati zisizo za kawaida".
Nchi wanachama sita wa EAC; Kenya, Burundi, Sudan Kusini, Tanzania, Uganda na Rwanda wanadaiwa michango inayokaribia kiasi cha dola za Marekani milioni 50 - kila nchi ikitakiwa kuchangia kiasi cha dola milioni 8.2 katika bajeti ya mwaka huu.
Matokeo yake ni kwamba hadi leo bajeti ya EAC haijapitishwa ingawa muda wa kufanya hivyo umepita. Bajeti hupitishwa na Baraza la Mawaziri la EALA ambalo halikukutana kwa sababu ya vifo vya aliyekuwa Rais wa Burundi, Pierri Nkurunziza na aliyekuwa Waziri wa Masuala ya EAC wa Sudan Kusini, John Luk Jok.
Katikati ya mgogoro huo, Kenya na Tanzania zimeibua tena mgogoro mpya katika eneo la masuala ya anga. Kenya ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari ikitangaza nchi ambazo raia wake wanaruhusiwa kuingia Kenya baada ya kukidhi vigezo vya ugonjwa wa Korona; orodha ambayo Tanzania haikuwemo.
Kwa kujibu mapigo, Tanzania nayo ikatangaza kwamba ndege za Shirika la Ndege la Kenya (Kenya Airways) hazitaruhusiwa kutua katika viwanja vya ndege vya taifa hilo.
Suala la anga ni suala lenye maumivu kwa Tanzania kwenye mahusiano yake na Kenya. Siku ambayo EAC ilitangazwa kuvunjwa kwa mara ya kwanza mwaka 1977, Kenya ilibaki na ndege zote zilizokuwa zikimilikiwa kwa pamoja na nchi wanachama wa EAC; jambo lililoifanya Tanzania kuanza upya kutengeneza shirika lake la ndege la Air Tanzania ikiwa haina ndege ya kibiashara.
Mgogoro wa sasa baina ya majirani hawa ni mlolongo mrefu wa migogoro ya karibuni, ikiwamo ule wa mamlaka za Tanzania kuchoma moto kuku 6,400 kutoka Kenya waliokuwa waingizwe nchini pasipo kufuata taratibu za viwango za EAC.
Jambo hili liliwaudhi Wakenya wengi na lilizua mjadala mkali katika mitandao ya kijamii, huku wananchi wa nchi zote hizo wakirushiana maneno. Marais Uhuru Kenyatta na John Magufuli walizungumza kwa simu na baadaye kukutana kumaliza jambo hilo na mengine yanayotajwa kuleta mgogoro.

Chanzo cha picha, Anadolu Agency/Getty
Viongozi huamua aina ya jumuiya
Tofauti moja kubwa na ya msingi baina ya EAC na jumuiya kama ile ya Umoja wa Ulaya (EU) ambayo nayo huundwa na nchi tofauti za bara la Ulaya iko kwenye asili ya nchi wanachama.
Kabla ya kuundwa kwa EU, nchi za Ulaya zilikuwa na muda wa zaidi ya miaka 100 kujijenga kama nchi, kutengeneza taasisi za utatuzi wa migogoro yao na asasi za kiraia zenye nguvu.
Kwa hiyo, wakati wanaungana, tayari walikuwa na mifumo ya ndani na mambo ya msingi ya kukubaliana kwenye nini hasa nchi hizi zinahitaji kwenye jumuiya hiyo. Hali hiyo ni tofauti na EAC.
Wakati EAC inaundwa kwa mara ya kwanza; nchi waanzilishi zilikuwa hazina hata miaka 10 ya utaifa. Maana yake ni kwamba hazikuwa zimepitia changamoto za ndani za ujenzi wa taifa na taasisi za uchechemuzi wa mambo na utatuzi wa migogoro.
Kwa sababu hiyo, kinachofanya EAC idumu tangu ilipoanzishwa mara ya kwanza na hata ilipofufuliwa tena mara ya pili mwaka 1997 ni utashi wa viongozi waliopo madarakani wakati huo kuliko kitu kingine chochote.
Mwaka 1967, waliokuwa viongozi wa nchi za EAC; Jomo Kenyatta wa Kenya, Julius Nyerere wa Tanzania Milton Obote wa Uganda walikuwa ni viongozi walioamini katika dhana ya Umajumui wa Kiafrika -wakiwa ni viongozi wa kizazi cha kwanza cha viongozi wa bara hili baada ya Uhuru.
Wakati EAC inavunjika mwaka 1977, Uganda ilikuwa inatawaliwa na Idi Amin ambaye hakuwa na uhusiano mzuri na Nyerere lakini pia uhusiano wa Tanzania na Kenya nao haukuwa mzuri.
Wakati EAC inafufuliwa mwaka 1997, waliokuwa marais wa nchi hizo walikuwa ni Benjamin Mkapa, Yoweri Museveni na Daniel Arap Moi. Mkapa na Museveni ni wanasiasa walioamini katika Umajumui wa Afrika na hata kama Moi hakuwa katika kiwango chao cha maarifa na itikadi, alijua umuhimu wa EAC itakayotanua wigo wa biashara kwa taifa lake.
Hivi sasa EAC inaundwa na viongozi wa aina tofauti na wale wa kizazi cha kwanza baada ya ukoloni. Kama ilivyo katika siasa za kidunia, viongozi hao sasa wanaangalia zaidi mambo ya ndani kwao kuliko kwenye jumuiya.
Salva Kiir wa Sudan Kusini anapambana kuongoza taifa lake katika mgogoro wa muda mrefu na swahiba wake wa zamani, Riek Machar. Tangu aingie madarakani, Rais John Magufuli wa Tanzania ameonyesha kwamba mara zote ataweka maslahi ya taifa lake mbele ya maslahi ya jumuiya.
Baada ya kukaa madarakani kwa zaidi ya miaka 30, pengine Yoweri Museveni ameanza kuchoka ingawa kulinganisha na wenzake, pengine yeye ndiye pekee aliyebaki anayeamini katika ndoto ya Shirikisho la Afrika Mashariki.
Paul Kagame wa Rwanda ni mwanajumui lakini tatizo lake na Burundi ni kwamba nchi zao hazina uzito mkubwa kwenye jumuiya kulinganisha na Kenya, Uganda na Tanzania.
Katika miaka ya mwishoni ya hayati Pierre Nkurunziza; hasa baada ya jaribio la mapinduzi dhidi yake kufeli mwaka 2017 wakati akiwa anahudhuria kikao cha viongozi wa EAC jijini Dar es Salaam, aliamua kubaki nyumbani na hakuhudhuria vikao vya viongozi hadi anaondoka madarakani. Ni kama alikuwa ameamua kuisusa jumuiya.

Mwalo na Obufuura
Faida moja kubwa ambayo EAC inayo iko kwa wananchi wake. Kwa kawaida, wananchi wa Afrika Mashariki ni watu ambao kwa asili huwasikiliza viongozi wao na kuwatii.
Utamaduni huo umejengwa katika misingi ya makabila yanayozunguka nchi hizi. Wajaluo walio katika nchi zote za Afrika Mashariki wana mila inayoitwa Mwalo ambayo Wanyankore wa Uganda huiita Obufuura. Ni mila inayotaka watu waheshimu wakubwa zao au viongozi waliopewa mamlaka.
Pia, wananchi wenyewe wa EAC wameanza kuhusiana wenyewe kibiashara, kijamii na kitamaduni kwa muda mrefu pengine kuliko hata kuwapo kwa jumuiya yenyewe. Wananchi wa EAC wameoleana, kusomeshana, kutaniana na kushirikiana katika mambo mbalimbali pasipo kushirikisha serikali zao.
Hivyo, hata kama viongozi wataamua kwamba EAC haina nafasi tena na kuvunjwa kama ilivyokuwa mwaka 1977, wananchi wataendelea kushirikiana kwa namna ileile ambayo walikuwa wakishirikiana kwa miaka mingi; na utandawazi sasa ukirahisisha kila kitu.
Mustakabali
Mustakabali wa EAC unategemea zaidi ushirikishwaji na uimarishwaji wa raia na taasisi za kiraia katika mchakato mzima wa kufungamanisha jumuiya hiyo, hali ya usalama ya eneo hilo, hali ya ukuaji wa uchumi wa nchi wanachama na utashi wa viongozi wa nchi wanachama.
Uimarishaji wa haki za kiraia ikiwamo uhakika wa usalama katika nchi hizi za EAC, ukuaji wa demokrasia na uhuru wa kutoa maoni ni mambo ambayo yamesaidia jumuiya kama EU kuvuka vizingiti vingi na kudumu hadi leo.
Katika hali ya sasa ya EAC, kudumu kwake kunategemea zaidi kuwapo kwa viongozi wenye utashi wa kutaka idumu, wenye mtazamo mpana wa kimajumui na kidunia na wa nchi zenye usalama wa kutosha wa ndani na ukuaji wa uchumi unaoridhisha.
Bahati nzuri, viongozi karibu wote wa sasa wa EAC wanaamini katika ukuzaji wa uchumi wa nchi zao na wanajua kwamba jumuiya hii ni soko kubwa kwa ajili ya bidhaa zao lakini pia kiusalama.
Ndiyo sababu, pamoja na changamoto zote za sasa, hakuna hata kiongozi mmoja wa nchi wanachama wa EAC ambaye amezungumza hadharani kuwa anatamani kujiondoa kwenye jumuiya.












