Virusi vya Corona: Rais na mawaziri wa Malawi kukatatwa 10% ya mishahara yao

Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Malawi na mawaziri wote nchini humo watakatwa asilimia kumi ya mishahara yao ya miezi mitatu ili kupata fedha za kukabiliana na mlipuko wa virusi vya corona.
Rais Peter Mutharika alitangaza hatua hiyo ili kukabiliana na athari za kiuchumi ambazo zimesababishwa na corona.
Malawi imeripoti kisa cha kwanza cha mgonjwa mwenye virusi vya corona siku ya Alhamisi, na lilikuwa taifa la mwisho kutangaza kuwa na maambukizi.

Chanzo cha picha, Reuters
Hatua hii imechukuliwa wakati rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta alitangaza kwamba yeye na makamu wake watapunguziwa asilimia 20% katika mshahara wao.
Alihimiza hatua hiyo ichukuliwe na viongozi wengine serikalini kukatwa 10%.
Bwana Kenyatta na wabunge wa Kenya ni miongoni mwa watu wanaolipwa fedha ningi zaidi barani Afrika.


Taifa hilo ambalo ni miongozi mwa mataifa maskini zaidi duniani limetangaza hali ya dharura nchini mwake.
Hawajafungia watu kutoka nje lakini shule zimefungwa na serikali imesisitiza watu wafanyie kazi nyumbani na kufuata muongozo uliotolewa wa kujikinga kwa kuosha mikono kila mara na kutosogeleana.
Mikusanyiko yote ya watu zaidi ya 100 imesitishwa kuanzia misiba, sherehe, ibada na mikutano ya kisiasa.
Bwana Mutharika anapata mshahara unaofikia dola 3,600 kwa mwezi lakini haijawekwa wazi ni kiasi gani cha fedha kitakatwa kutoka katika mishahara ya mawaziri wa nchi hiyo.
Vilevile rais ametaka kodi ipunguzwe katika biashara mbalimbali kama mafuta na kuongeza kipato cha wafanyakazi wa afya ambao wako katika mazingira hatari zaidi ya ugonjwa, Reuters imeripoti.

Chanzo cha picha, AFP
Tumbaku ndio zao lao kuu la biashara , na rais amesema maduka ya tumbaku yatabaki wazi ili kusaidia kupata fedha za kigeni na wakulima waweze kupata kipato chao.
Sasa wana wagonjwa wanne ambao wote wanahusishwa kuwa walisafiri kutoka Uingereza.
Bwana Mutharika, 79, aliingia madarakani mwaka 2014 na uchaguzi mwingine unatarajiwa kufanyika Julai 2.














