Tassia: Idadi ya watu waliofariki baada ya jengo kuporomoka Kenya yafikia watu 5

Watu wakishuhudia jengo lililoporomoka

Chanzo cha picha, Victor Kenani, BBC

Maelezo ya picha, Watu wakishuhudia jengo lililoporomoka

Watu watano wamethibitishwa kufariki kufikia sasa baada ya jengo la ghorofa sita kuanguka Ijumaa asubuhi katika eneo la Embakasi jijini Nairobi, Kenya huku wengine kadhaa wakihofiwa kunaswa chini ya kifusi cha jengo hilo.

Shughuli za uokoaji zinaendelea. Ripoti zinasema watu kadhaa wameokolewa na kukimbizwa hospitalini kwa ajili ya matibabu.

Watu watatu wakiwa na majeraha mabaya wametolewa kutoka kwenye kifusi na kupelekwa kwenye hospitali ya rufaa ya Kenyatta, jijini Nairobi, wakiwemo mama na mtoto.

Familia 46 walikuwa wakuwa wakiishi kwenye jengo hilo.

Maelezo ya video, Aliyeshuhudia aelezea kilichotokea?

Polisi na kikosi cha msalaba mwekundu kutoka kaunti ya Nairobi wako kwenye eneo la tukio. Wanapata wakati mgumu kudhibiti kundi kubwa la watu waliojitokeza kushuhudia mkasa huo.

Haijabainika ni kwanini jengo hilo liliporomoka na ni watu wangapi wamekwama kwenye jengo hilo.Wenyeji wanadai kuwa huenda ikawa watu wengi wamekwama kwani jengo lenyewe liliporomoka mapema asubuhi na wakati huu shule zikiwa zimefungwa.

Baadhi ya maafisa wa St Johns wakishirikiana na maafisa wa polisi pamoja na wasamaria wema kuokoa baadhi ya watu waliokuwa wamenaswa chini ya vifusi vya jengo hilo
Maelezo ya picha, Baadhi ya maafisa wa St Johns wakishirikiana na maafisa wa polisi pamoja na wasamaria wema kuokoa baadhi ya watu waliokuwa wamenaswa chini ya vifusi vya jengo hilo

Wenyeji wanailaumu Idara ya mipango ya Ujenzi nchini kwa kutohakikisha majengo yaliyojengwa ni salama kutumika.Wanadai kuwa Idara hiyo imezembea katika kukagua usalama wa majengo hasa jijini Nairobi na hivyo kuwaacha watu katika hatari.

Shughuli za kuwaokoa walionasa kwenye jumba hilo zinaendelea huku magari ya kubeba wagonjwa yakiwa yamefika kutoa msaada wa dharura.

Mkuu wa polisi Philip Ndolo amesema kuwa wanafanya kila wawezalo kuwaokoa watu waliokwama.

Watu wanahofiwa kunasa kwenye kifusi

Chanzo cha picha, Dickson Omari

Maelezo ya picha, Watu wanahofiwa kunasa kwenye kifusi

Hili si jengo la kwanza kuporomoka. Mwezi Septemba mwaka huu jengo la ghorofa moja la shule eno la Dogoretti Nairobi liliporomoka na kuwaua wanafunzi saba huku wengine 64 wakijeruhiwa. Mwaka 2015,Jengo jingine la ghorofa sita liliporomoka eneo la Huruma jijini Nairobi na kugharimu maisha ya watu.

Serikali wakati huo ilianza ukaguzi wa majengo yote haswa ya makazi jijini Nairobi.

Ripoti ya ukaguzi ilionyesha kuwa zaidi ya majengo 800 si salama na hivyo yalihitaji kubomolewa kwani hayakidhi viwango vya ubora.

Hata hivyo shughuli hiyo ilisimamishwa baadaye serikali ikidai haikuwa na fedha za kutosha kubomoa majengo hayo yote.