Mwandishi ashtakiwa kwa makosa ya Ugaidi nchini Rwanda

Nchini Rwanda, kesi dhidi ya mwandishi wa habari wa kujitegemea Phocus Ndayizera imeanza kusikilizwa rasmi na mahakama ya makosa ya jinai katika mji wa Nyanza kusini mwa Rwanda.
Yeye na kundi lake la watu 13 wameshitakiwa makosa manne yakiwemo ugaidi na kuunda kundi la kijeshi kwa lengo la kuipindua serikali.
Mwandishi huyo alifanyia kazi vyombo vya habari mbalimbali nchini Rwanda na mara kwa mara alikuwa akiripotia BBC Idhaa ya Kinyarwanda-Kirundi.
Wote wanakana mashtaka dhidi yao.
Mwandishi huyo wa kujitegemea na wenzake 13 waliingia mahakamani wakiwa wamefungwa pingu miguuni na mikononi, huku wakiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi.
Unaweza pia kusoma
Mwendesha mashtaka ndiye aliyechukua sehemu kubwa kufafanua mashtaka dhidi ya washtakiwa, lakini kikubwa ni kwamba wameshtakiwa makosa manne ambayo ni pamoja na kushawishi vijana kujiunga na kundi la waasi la RNC linaloongozwa na jenerali Kayumba Nyamwasa mkuu wa zamani wa majeshi ya Rwanda ambaye yuko uhamishoni nchini Afrika kusini, kosa la kutaka kuangusha utawala wa Rwanda na makosa ya ugaidi.
Ufafanuzi wa kimsingi wa mashtaka hayo
Mwendesha mashtaka amesema Phocus Ndayizera alikamtwa na maafisa wa upelelezi akiwa na vilipuzi ambavyo alitumiwa na bwana mwingine anayefahamika kwa jina la Cassien Ntamuhanga, bwana huyu sasa hivi ni msemaji wa kundi la RNC , ambaye naye alikuwa mwandishi wa habari nchini Rwanda kabla ya kutoroka gerezani.
Alishutumiwa kwa makosa kama hayo ya uhaini. Sasa anaishi uhamishoni nchini Msumbiji.
Kadhalika mwendesha mashtaka ameonesha ujumbe wa WatsApp ambao Phocus Ndayizera amekuwa akiandikiana na msemaji huyo wa RNC kuhusu mipango ya matumizi ya vilipuzi hivyo ambavyo vingelipuliwa kwa njia ya teknolojia ya simu ya mkononi yakilengwa maeneo muhimu kama ghala za mafuta ya petroli,na mitambo ya nishati na maeneo mengine.

Upande wa utetezi umesema nini?
Mwanzoni kabisa Jaji aliwauliza ikiwa wanakiri au wanakana mashtaka dhidi yao ,wote walikana mashtaka hayo.
Lakini kauli yao ni kama imemshangaza mwendesha mashtaka kwa sababu mwaka jana mchakato wa kesi hii ulipoanza Phocus Ndayizera mwenyewe alikiri mashtaka dhidi yake na kusema kwamba yuko tayari kuisaidia mahakama na kubainisha ukweli.
Hata hivyo wakati wao wa kujieleza ama kutoa hoja zao bado haujafika na kesi imeahirishwa ambapo kesi itasikilizwa ten tarehe 28 mwezi huu.













