Donald Trump: Maafisa wa Ikulu ya White House washutumiwa kujaribu kuficha mawasiliano

TRUMP

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 3

Maafisa waandamizi wa Ikulu ya White House walijaribu kuficha vielelezo vya mawasiliano ya simu baina ya rais Donald Trump na rais wa Ukraine, ameeleza mfichua siri wa sakata hilo.

Sakata hilo ambalo limekuwa kaa la moto kwa utawala wa Trump, linahusisha mawasiliano ya simu yaliyovuja juu ya raisi Trump akimtaka rais Volodymyr Zelensky kumchunguza mpinzani wake wa kisiasa, Joe Biden.

Taarifa mpya ya mtoa siri inabainisha kuwa, nakala halisi ya mazungumzo hayo ya simu haikuhifadhiwa kwenye mfumo stahiki wa kompyuta.

Badala yake nakala hiyo ilihifadhiwa kwenye mfumo tofauti wa kompyuta kwa ajili ya taaifa za siri.

Spika wa Bunge la Congress kutoka chama cha Democrats,Nancy Pelosi, ameshatangaza kuwa chama hicho kitaanzisha uchunguzi rasmi wenye lengo la kumng'oa madarakani Trump kutoka chama cha Republican.

Pelosi amemtuhumu Trump kwa kutafuta msaada kutoka nchi ya kigeni kwa minajili ya kumchafua kisiasa mpinzani wake na kutumia msaada wa kijeshi kama nyenzo ya kutaka matakwa yake yatimizwe.

Bw Biden ndiye kinara wa mbio za tiketi ya kugombea urais 2020 kwa chama cha Democrats.

Bwana Trump amekiri kuwa alimzungumzia Joe Biden na Bwana Zelensky, na kuwa alizuia msaada wa kijeshi kwa nchi hiyo wa thamani ya dola milioni 400. Lakini amekanusha kuwa alifanya hivyo kama shinikizo kwa Ukraine ili kumchunguza Biden.

Trump amedai kuwa uchunguzi dhidi yake ni "feki" na "kusaka mchawi" na ameonesha hasira zake kupitia mtandao wake pendwa wa kijamii, twitter.

Ruka X ujumbe
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: Imetoka kwingine na inaweza kuwa na matangazo

Mwisho wa X ujumbe

white space

Mazungumzo baina ya Trump na Zelensky yalikuwaje?

Kwa mujibu wa mukhtasari uliotolewa jana na Ikulu ya White House, Trump alimwambia Zelensky juu ya namna ambavyo Joe Biden akiwa makamu wa rais alishawishi Ukraine kumtimua kazi mwendesha mashtaka wake mkuu, Viktor Shokin mwaka 2016.

Ofisi ya Shokin ilifungua jalada la uchunguzi dhidi ya Burisma, kampuni ya gesi asili ambayo mwana wa Joe Biden, Hunter alikuwa ni mjumbe wa bodi yake.

Nchi kadhaa za magharibi pia zilikuwa zikishinikiza Bw Shokin atimuliwe kazi kwa madai alikuwa akivumilia vitendo vya rushwa.

"Nimesikia mlikuwa na mwendesha mashtaka ambaye alikuwa ni mzuri kweli na alifutwa kazi kwa njia ya uonevu. Watu wengi wanalizungumzia jambo hilo," Trump ananukuliwa akisem kwenye mazungumzo hayo na kuongeza: "Kitu kingine, kuna mjadala mkubwa kumhusu mtoto wa Biden, kuwa baba yake alizuia waendesha mashtaka na watu wengi wanataka kujua undani wa hilo, so chochote unachoweza kufanya na Mwanasheria Mkuu (wa Marekani) litakuwa jambo jema.

"Biden alikuwa akijitamba kuwa amezuia uchunguzi angalia utakachokifanya hapo...ni jambo baya sana kwangu."

Zelensky anaripotiwa kujibu: "Tutalishughulikia hilo na tutafanyia kazi uchunguzi wa kesi hiyo.

"Juu ya hilo, pia ningeomba kama una taarifa zozote za ziada pia tupatie, zitatusaidia sana."

Akimshukuru Trump, bw Zelensky alisema kuwa alikaa kwenye jumba lake la jijini New York, Trump Tower, mara ya mwisho alipozuru nchini humo

Zelensky amesema nini?

Ukraine's President Volodymyr Zelensky and US President Donald Trump meeting on the sidelines of the United Nations General Assembly in New York on Wednesday

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Bw Zelensky na Trump wamekutana Jumatano jijini New York Jumatano

Raisi huyo wa Ukraine amesema alidhani kuwa maelezo ya Trump pekee katika mawasiliano hayo ndiyo ambayo yangechapishwa.

"Nadhani, wakati mwengine, mawasiliano ya simu baina ya marais wa nchi huru hayatakiwi kuchapishwa," Zelensky ameviambia vyombo vya habari vya Ukraine akiwa jijini New York, kwa mijubu wa shirika la habari la kimataifa la Reuters.

Bw Zelensky ameongeza kuwa kesi ya Hunter Biden ni miongoni mwa kesi nyingi ambazo huwa anazijadili na viongozi wa kimataifa.

"Kwangu mie, hii ni moja ya kesi nyingi ambazo huwa nazifanyia mazungumzo na viongozi wa mataifa mengine, endapo wananiuliza," ameeleza raisi huyo.

"Wakati mwengine, kesi hizi huchunguzwa ama huwa hazijachunguzwa kwa muda mrefu - na sijui kwanini," ameeleza.

Mchakato wa uchunguzi