Makavazi ya New York Met yamerejesha jeneza la kale lililoibwa Misri

Chanzo cha picha, Reuters
Mamlaka ya Marekani imerudisha jeneza lililoibwa Misri miaka miwili baada ya kupatikana jumba moja la makumbusho ya sanaa mjini New York.
Jeneza hilo lenye miaka 2100 la muhubiri kwa jina Nedjemankh lilionyeshwa katika maonyesho ya vitu vya kale kutoka Misri.
Jeneza hilo liliuziwa makavazi hayo na mtandao mmoja wa sanaa uliodaiwa kutumia hati bandia , maafisa walisema. Jeneza hilo liliibiwa na kusafirishwa kutoka Misri 2011.
''Uchunguzi wetu umebaini kwamba jeneza hilo ni miongoni mwa mamia ya vitu vya kale vilivyoibwa na mtandao huohuo wa kimataifa'', wakili mmoja wa mji wa Manhattan Cyrus Vance alisema akinukuliwa na chombo cha habari cha Reuters, katika sherehe ya kulirejesha mjini New York, akiongezea kwamba huenda kuna vitu vingine zaidi ambavyo vilipatikana pamoja na jeneza hilo.

Chanzo cha picha, Reuters
Jeneza hilo ambalo lilitengezwa karne ya kwanza lilinunuliwa na makavazi hayo kwa kima cha $4m (£3.2m) kutoka kwa ajenti mmoja wa sanaa.
Mara ya kwanza lilipelekwa hadi Ujerumani ambapo lilihifadhiwa kabla ya kusafirishwa nchini Ufaransa.
Makavazi hayo yalipewa leseni bandia ya Misri ya mwaka 1971 miongoni mwa hati nyengine bandia kulingana na waendesha mashtaka ambao waliambia vyombo vya habari vya Marekani.
Maafisa wanasema kwamba jeneza hilo lilikuwa limezikwa katika jimbo la Minya kwa takriban miaka 2000 kabla ya kuibwa 2011.
Hili sio tu la Misri bali pia kwa turathi zetu, alisema waziri wa maswala ya kigeni nchini Misri sameh Hassan Soukry, akinukuliwa na Reuters. Jeneza hilo liwekwa katika maonyesho nchini Misri 2020.













