Wakenya kutozwa kodi zaidi iwapo marekebisho ya mswada wa fedha yakiidhinishwa

simu

Chanzo cha picha, ISAAC KASAMANI

Watumiaji wa simu nchini Kenya huenda wakatozwa ada zaidi katika ununuzi wa muda wa maongezi na huduma ya mtandao.

Hii ni baada ya serikali kutangaza mpango wa kuongeza kodi ya ongezeko la thamani(VAT) kutoka 10% hadi 15%.

Nyongeza hiyo imejumuishwa katika pendekezo la rais Uhuru Kenyatta kwa bunge kufuatia tamko lake la wiki iliyopita.

Pendekezo la tozo hilo jipya la kodi likiidhinishwa na bunge litatekelezwa wakati ambapo watumiaji wa simu wanakabiliwa na gharama ya ongezeko la ada ya huduma za kutuma pesa.

Serikali iliongeza ushuru unaotozwa huduma hiyo 10% mwezi Julai ili kufadhili mpango wa bima ya matibabu kwa wote ifikapo mwaka 2022.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta

Chanzo cha picha, POOL/GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta

Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya mamlaka ya mawasiliano nchini Kenya, ushuru huo utaathiri zaidi ya watumiaji milioni 44.1 wa simu.

Serikali imekuwa ikiwahamasisha wakenya kuzingatia malipo ya kielektroniki ili kuboresha huduma na kupunguza visa vya udanganyifu.

Huduma ya kutuma na kupokea pesa kwa njia ya simu, M-Pesa ilikuwa kwa 14.2% ambayo ni sawa na bilioni 62.9 bilioni kwa mwaka wa fedha ulioishia Machi 2018.

Kodi mpya inayowalenga watumiaji wa simu za mkononi imetokana na ukosoaji mkali dhidi ya Kenya serikali kuhusu mpango wa kuongeza kwa 16% kodi ya bidhaa za mafuta.

Hoja hii ilizua malalamishi makubwa ya umma hatua ambayo ilimfanya rais Kenyatta kuingilia kati suala hilo.

App ya mitandao ya kijamii

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, App ya mitandao ya kijamii

Ni yapi yaliyomo katika mapendekezo ya rais Kenyatta kwa wabunge

Miongoni mwa aliyopendekeza rais Uhuru kando

  • Kuongeza kodi ya VAT kwa watumiajiwa simu kutoka 10% hadi 15%
  • Rais Uhuru ametangaza kupunguza kodi ya mafuta kutoka 16% hadi 8%.
  • Kupunguza gharama za mapokezi , burudani, mafunzo na mikutano, na usafiri katika nchi za nje.
  • Kuongeza fedha katika idara za utekelezaji wa sheria kuweza kukusanya mapato zaidi kupitia mahakama ya nchini.

Rais Kenyatta amesema kuwa bado kuna pengo katika bajeti ya serikali na ndio sababu amependekeza hatua hizo za kufunga mkaja au kubana matumizi katika idara zote za serikali

Mapendekezo hayo, hata hivyo yanatarajiwa kujadiliwa bungeni siku ya Alhamisi.