Adhabu kali zaendelea kutolewa dhidi ya wanaomkashifu rais Tanzania

Chanzo cha picha, AFP
Raia mwingine nchini Tanzania amehukumiwa kwenda jela kwa kipindi cha miezi sita au kulipa faini ya sh.200,000 kwa kosa la kutumia lugha ya kumdhihaki rais Magufuli.
Yuston Emmanuel mwenye umri wa miaka 31 ambaye ni mkaAzi wa Ngara mkoani Kagera,Tanzania amehukumiwa kwa kosa a ambalo mwendesha mashtaka alidai kwamba alikuwa amekwenda kinyume na kifungu cha 89(1) (a) cha kanunu ya adhabu iliyorekebishwa na kuna umuhimu wa adhabu kali kutolewa ili iwe fundisho kwa wengine.
Raia huyo ni miongoni mwa watu wasiopungua kumi wa nchi hiyo, idadi ambayo inajumuisha viongozi wa upinzani na raia wa kawaida walioshitakiwa kwa kosa la kumdhihaki au kumtusi rais Magufuli tangu aingie madarakani.
Mwezi Juni mwaka 2016, Mulokozi Kyaruzi ni miongoni mwa raia wa Tanzania ambaye alishtakiwa chini ya sheria ya uhalifu wa mtandaoni baada ya kudaiwa kumtusi Rais John Pombe Magufuli .

Chanzo cha picha, Getty Images
Mbunge wa chama cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema Halima Mdee mwezi agosti 2017 alishtakiwa kwa kosa la kumtusi rais na aliachiliwa huru kwa dhamana ya shilingi milioni kumi za Tanzania .
Muhadhiri mmoja pia alishtakiwa katika mahakama moja nchini Tanzania kwa kumtusi rais wa taifa hilo chini ya sheria ya uhalifu iliowekwa mwaka uliopita.

Chanzo cha picha, CHADEMA
Kulingana na afisi mkuu wa polisi wa eneo la kusini magharibi mwa Tanzania, alidai shtaka hilo ni hatia na mtu anaweza kufungwa hadi miaka mitatu jela ama kupigwa faini ya dola 3,000 ama zote.
Mhadhiri huyo alikana mashtaka hayo.
Mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Osmund Mbilinyi, mnamo tarehe 26 Februari alihukumiwa kifungo cha miezi mitano na mahakama ya hakimu mkazi Mbeya kwa kupatikana na kosa la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli.
Hatia ya mashtaka imesema maneno waliyoyatamka yalienda kinyume na Sehemu 89(1) a ya Sheria za jinai ambayo inaharamisha kutumiwa kwa lugha ya matusi.

Chanzo cha picha, Mr.Sugu
Maneno hayo, hati za mashtaka zinasema, yangeweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Sheria hiyo ilikosolewa sana kwa kukandamiza uhuru wa kujieleza wakati ilipoanza kutekelezwa mwaka uliopta.
BBC ilifanya mahojiano na wakili Jebra Kambole ambaye alisema adhabu hizo zinatekelezwa kwa mujibu wa sheria ya makosa ya jinai kifungu cha 89 ambapo kifungo huwa ni miezi sita au faini ambayo hutolewa kwa kuangalia uwezo wa mtu mwenyewe.
"Sheria ipo lakini sheria hii ni tishio la uhuru wa mtu kujieleza na demokrasia kwa pamoja kwa sababu inawezekana kuwa tafsiri za maneno zikatofautiana na hii sheria inawagusa hata kwa mtu kwa mtu sio kwa viongozi peke yake,labda ni wakati sasa watetezi wa haki za binadamu nao waingilie kati suala hili",Jebra alieza.
Licha ya kuwa watu kadhaa wamekamatwa katika siku za nyuma kwa kuchapisha ujumbe katika mitandao ya kijamii ambayo mamlaka inadai inaingilia kisiasa.
Mamlaka inaamini kwamba inafuata sheria na kuchukua hatua za kuhakikisha kwamba hakuna ''migogoro yoyote miongoni mwa wananchi'' nchini Tanzania.












