Rais Uhuru Kenyatta akubali kupunguza kodi ya mafuta Kenya

Chanzo cha picha, POOL/GETTY IMAGES
Rais Uhuru Kenyatta amekubali kupunguza tozo la kodi iliyopingwa na raia nchini ya 16% kwa bidhaa za mafuta nchini.
Katika hotuba kwa taifa, Rais Uhuru amependekeza kupunguza kwa nusu kodi hiyo hadi 8%
Rais Kenyatta ameeleza kwamba amesikia kilio cha Wakenya kuhusu kupanda kwa bei za bidhaa.
Awali rais Kenyatta alikataa kusaini mswada wa fedha ambao ungetoa fursa ya kusitishwa kwa tozo la kodi ya 16% kwa bidhaa za mafuta nchini.
Kumekuwa na hasira miongoni mwa raia wanaolalamika kuhusu kupanda kwa gharama ya maisha.
Miongoni mwa aliyopendekeza rais Uhuru kando na kupunguzwa kwa kodi hiyo ya mafuta kutoa 16% hadi 8% ni pamoja na kuupunguza gharama za mapokezi , burudani, mafunzo na mikutano, na usafiri katika nchi za nje.
Kadhalika amependekeza kuongezwa fedha katika idara za utekelezaji wa sheria kuweza kukusanya kipato zaidi kupitia mahakama nchini.
Ameeleza kuwa bado kuna pengo katika bajeti ya serikali na ndio sababu amependekeza hatua hizo za kufunga mkaja au kubana matumizi katika idara zote za serikali.

Mapendekezo yote yanasubiri kuidhinishwa bungeni.
Kwa mujibu wa ilani rasmi ya serikali iliyotiwa saini na spika wa bunge Justin Muturi, bunge litaandaa kikao maalum Septemba 18 kutathmini upya mswada huo na 'kwa kuzingatia pia aliyoyapinga rais Kenyatta'.
Mambo muhimu kuhusu 16% Tozo la kodi kwa bidhaa za mafuta Kenya
- Iliidhinishwa mnamo 2013.
- Bunge lilipitisha mswada wa tozo la kodi ulioidhinisha kupandishwa kwa bei za bidhaa za mafuta.
- Imenuiwa kukusanya pato la takriban $ milioni 338 kwa mwaka.
- Wizara ya fedha mnamo 2016 ilisimamisha hatua hiyo kwa miaka miwili ya ziada.
- Imelenga kutatua nakisi ya bajeti ya serikali na kupunguza deni la taifa.
- Rais Uhuru Kenyatta amekataa kusaini mapendekezo yaliowasilishwa ya marekebisho ya sheria.
Wiki iliyopita serikali iliidhinisha tozo hilo la kodi la 16% kwa bidhaa zote za mafuta , hatua iliyochangia kupanda kwa gharama za usafiri wa magari ya uchukuzi wa umma na pia bei za mafuta.

Kulishuhudiwa mgomo wa wafanyabiashara ya mafuta na hasira miongoni mwa wasafiri na umma kwa jumla.
IMF na mikopo Kenya
Kitendawili kwa serikali ya Kenya sasa ni kujua wapi itakapopata zaidi ya $ milioni 90 kuziba pengo katika nakisi ya bajeti.
Hatua iliyoidhinishwa ni sehemu ya jitihada za serikali kuimarisha uchumi wa nchi na kupunguza nakisi ya bajeti pamoja na kutafuta fursa ya kupata mikopo zaidi kimataifa.
Shirika la kimataifa la fedha IMF limeunga mkono mapendekezo ya kufunga mkaja kwa serikali ya Kenya, miaka miwili ya nyuma katika jitihada za kuziba pengo hilo la bajeti.
Mnamo Februari shirika la kimataifa la kuorodhesha uwezo wa mataifa kukopa, Moody, lilishukisha uwezo wa Kenya kukopa kutoka B2 hadi B1 kutokana na kuongezeka kwa deni la taifa ambalo kwa sasa linakadiriwa kuwa limefika 58% ya pato jumla la nchi.
Iwapo Kenya itazidi kushukishwa uwezo wake wa kukopesha, hilo linaweza kuchangia kwa nchi hiyo kuishia kuchukua mikopo kwa viwango vikubwa vya riba.
Moody pia tayari limeitahadharisha Kenya kuhusu athari ya kulimbikiza madeni yake .

Chanzo cha picha, AFP
Kibarua cha bunge kutoa mwelekeo?
Mchambuzi wa masuala ya kiuchumi Kenya, Paul Wafula anasema kinachotazamiwa ni rais kulitaka bunge sasa litoe njia nyingine ambazo zitaweza kuleta kipato kwa uchumi wa nchi .
Wafula anaeleza kwamba bunge lina nafasi ya kupinga mapendekezo ya rais kwa kupitisha mswada utakaopinga mapendekezo hayo.
Hatahivyo anatathmini kwamba ni vigumu sana kuzuia mapendekezo ya rais kutokana na changamato ya kupata uwingi bungeni wa kupitisha mswada huo mpya.
Kitakacho salia ni bunge kulazimika kupokea na kuyashughulikia mapendekezo ya rais na liamue ni njia gani litaweza kuleta uwiano kati ya mapendekezo ya serikali ya Uhuru Kenyatta na matakwa ya raia.

'Hakuna uwezekano wa sheria kuondolewa, kwasababu ni lazima bunge lipitishe bajeti inayojisismamia mapato yake na lazima yaweze kulingana na matumizi yake' anaeleza Mwanauchumi Paul Wafula.
Na faida inayotarajiwa kutokana na ushuru unaotozwa sasa kwa mafuta, ina uzito na inatazamiwa kuleta tofuati kubwa, anasema.














