Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed aanza ziara ya kihistoria Eritrea

Chanzo cha picha, AFP/GETTY
Waziri mkuu mpya wa Ethiopia Abiy Ahmed, ameanza ziara ya kihistoria huko Eritrea siku chache baada ya nchi hizo mbili kutangaza kusitisha uhasma baina hayo.
Ethiopia na Eritrea zimewahi kupigana katika siku za nyuma kutokana na mzozo wa mpakani na tangu hapo wamekuwa na uhasama wa zaidi ya miaka 20.
Hivyo waziri mkuu Abiy Ahmed atakuwa wa kwanza kutembelea Eritrea katika kipindi hicho cha miongo miwili.
Mapema mwezi huu Ethiopia ilipokea ujumbe kutoka Eritrean ulioashiria heri njema baina yao.
Kiongozi wa Eritrea Isayas Afewerki alikuwa wa kwanza kuchukua hatua ya mawasiliano na utawala wa Addis Ababa baada ya kusifia hatua za mageuzi ya kisiasa yanayofanywa na waziri mkuu Abiy Ahmed.
Eritrea ilijinyakulia uhuru wake hapo 1993 lakini haikupita zaidi ya miaka mitano, mzozo baina yao ukazuka kuhusu kipande cha ardhi kame iliyompakani mwa mataifa hayo na kusababisha uhasama huo wa miongo kadhaa.
Uchunguzi wa umoja wa mataifa ulibaini kuwa kipande cha ardhi kilichokuwa kinazozaniwa ni cha Eritrea, uamuzi ambao Ethiopia haujaukubali kikamimilifu.
Ni kwa nini ziara hii ni ya kihistoria?
Eritrea na Ethiopia walipigana vita kuanzia Mei mwaka 1998 hadi Juni 2000. Licha ya nchi hizo kutumia mamilioni ya dola kwenye vita hivyo na watu wengi kuuawa ni manufaa kidogo sana yaliyopatikana.
Kulingana na uamuzi uliotolewa na tume ya kimataifa huko Hague, Eritrea ilikiuka sheria za kimataifa kwa kuivamia Ethiopia.
Wakati wa kumalizika kwa vita Ethiopia tayari ilikuwa imekalia arrdhi yote iliyokuwa ikizozaniwa na kuingia ndani ya ardhi ya Eritrea.
Baada ya kumalizika kwa vita, tume ya mpaka ya Eritrea na Ethiopia iliyobuniwa na Umoja wa Mataifa, iliamua kuwa eneo la Badme ambalo ndilo lilikuwa linazozaniwa lilikuwa la Eritrea.
Hadi sasa Ethiopia bado inadhibiti eneo hio lili karibu na Badme na hata mji wa Badme
Tarehe 5 Juni mwaka huu muungano wa vyama unaotawala nchini Ethiopia unaoongozwa Abiy Ahmed, ulikubali kutekeleza kikamilifu makubaliano ya amani waliyoyasaini na Eritrea mwaka 2000.












