Kenya: Seremala aishtaki serikali kwa kutomlipa fedha za viti alivyomtengenezea rais mstaafu

Rais mstaafu nchini Kenya Daniel Arap Moi

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Rais mstaafu nchini Kenya Daniel Arap Moi

Seremala mmoja nchini Kenya ameishtaki serikali akidai kutaka kulipwa $2m malipo ya viti viwili vya rais alivyomtengenezea rais mstaafu Daniel Arap Moi yapata miaka 26 iliopita.

Kwa mujibu wa mtandao wa Nairobi News nchini Kenya, Solomon Njoroge Kiore amesema kuwa aliwasilisha viti hivyo kwa afisi ya maonyesho ya kilimo ya Nairobi kwa hafla ya rais ya siku tatu.

''Bwana Moi alivitumia viti hivyo kwa mwaka mmoja, kabla ya viti hivyo kurudishwa kwangu'', bwana Kiore alinukuliwa akisema.

Alikuwa hajalipwa malipo ya viti hivyo licha ya kuwasilisha ombi lake kwa idara ya ulinzi ambayo ilitoa zabuni hiyo ikishirikiana na Ikulu ya rais.

Bwana Kiore alisema viti hivyo viwili vimechukua eneo kubwa la karakana yake na biashara yake imeanguka.

Mtandao huo wa habari umeripoti kwamba mawakili wa serikali walidai mwezi Februari kwamba waliafikiana kumaliza kesi hiyo nje ya mahakama lakini hawajawasiliana tena na bwana Kiore tangu wakati huo.

Bwana Kiore amesema kuwa angependelea viti hivyo kuwekwa katika jumba jipya la makumbusho lililopo katika Ikulu ya rais.