Mapato yatokanayo na Tanzanite yaongezeka baada ya ukuta kujengwa

Madini ya Tanzanite yanapatikana Tanzania pekee
Maelezo ya picha, Madini ya Tanzanite yanapatikana Tanzania pekee

Mapato ya serikali kutokana na madini ya Tanzanite yameongezeka mara nne zaidi katika kipindi cha miezi mitatu tangu ukuta ulipojengwa kuzunguka migodi, Waziri Mkuu wa Tanzania amewaambia wabunge.

Kassim Majaliwa amesema kati ya mwezi Januari na Machi, Serikali ilipata kiasi cha dola za Marekani zaidi ya 316,000.

Amesema kuwa hiyo ni zaidi ya mara nne ya kiasi ambacho serikali ilikuwa ikipata mwaka jana kutotokana madini

Taarifa hiyo imetolewa siku kadhaa baada ya Rais wa Tanzania, Dokta John Magufuli kuzindua ukuta wa umbali wa Km 24 kuzunguka mgodi unaozalisha Tanzanite mjini Mirerani kaskazini mwa Tanzania

Waziri Majaliwa alisema kabla ya kuwepo ujenzi wa ukuta uliofayika mwezi Novemba mwaka jana, takriban asilimia 40 ya madini ilikuwa ikiibiwa.

Ukuta ulijengwa na jeshi la taifa hilo na kugharimu dola za marekani milioni 3.5 kiasi kilichogharamiwa na serikali.

Ukuta wa kuzunguka mgodi wa Mirerani umejengwa kuzuia wezi wanaotorosha madini
Maelezo ya picha, Ukuta wa kuzunguka mgodi wa Mirerani umejengwa kuzuia wezi wanaotorosha madini

Hivi karibuni,Tanzania imeweka sheria kali kuhusu uchimbaji na usafirishaji ili kupata mapato zaidi, sera ambayo wachumi wanasema itapunguza kasi ya uwekezaji nchini.

Wakati Tanzania ikijivunia hatua hiyo kuhusu faida ya ukuta huo mpya,wachambuzi wa mambo wanasema ni mapema mno kuainisha faida zake na kuwa hatua nyingi zapaswa kuchukuliwa kuzuia wizi.