'Korea Kaskazini ilinipeleka nje ya nchi kufanya kazi kwa siri, mshahara wangu ulitumika kuendesha serikali'

Chanzo cha picha, Getty Images
Jin-su anadai kuwa ametumia mamia ya vitambulisho ghushi kwa miaka kadhaa kuomba kazi za Teknolojia ya Mawasiliano katika kampuni za mataifa ya Magharibi. Hii ilikuwa ni sehemu ya mpango wa siri wa kutafutia fedha Korea Kaskazini.
''Nilihangaika kufanya kazi tofauti Marekani na Ulaya, kupata dola 5,000 za Kimarekani kwa mwezi,'' aliambia BBC katika mahojiano nadra. Baadhi ya wafanyakazi wenzake, aliongeza, walipata hela nyingi zaidi.
Kabla ya kuasi, Jin-su - ambaye jina lake limebadilishwa ili kulinda utambulisho wake - alikuwa mmoja wa maelfu ya watu wanaoaminika kutumwa nje ya nchi kwenda China, Urusi, nchi za Afrika na kwingineko kushiriki katika operesheni ya siri iliyoongozwa na Korea Kaskazini.
Wanasayansi wa kompyuta wa Korea Kaskazini wanafuatiliwa kwa karibu, na baadhi yao wamezungumza na vyombo vya habari, lakini Jin-su alitoa maelezo ya kina kwa BBC, na kuangazia maisha ya kila siku ya wale wanaofanya kazi kwa ulaghai na jinsi wanavyofanya kazi hizo. Maelezo yake ya kibinafsi yanathibitisha kwa kiasi kikubwa makadirio ya ripoti za Umoja wa Mataifa na usalama wa mtandao.
Asnaema asilimia 85 ya mapato yake yalikwenda kwa serikali. Korea Kaskazini iliyo na uhaba wa pesa imekuwa chini ya vikwazo vya kimataifa kwa miaka kadhaa.
"Tunajua tunachokifanya ni kama wizi, lakini hatunabudi," Jin-su alisema. "Ukilinganisha na hali ilivyo ni bora zaidi kufanya hivyo kuliko tulipokuwa Korea Kaskazini."
Kulingana na ripoti ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa iliyochapishwa Machi 2024, wafanyakazi wa sekta ya Teknolojia ya Mawasiliano wanaofanya kazi kisiri huzalisha kati ya $250 milioni na $600 milioni kila mwaka kwa Korea Kaskazini. Mfumo huu uliongezeka wakati wa janga, wakati mfumo wa kufanya kazi ukiwa mbali ulipofanywa kuwa jambo la kawaida, na imeendelea kukua tangu wakati huo, mamlaka na wanharakati wakutetea haki mtandaoni wanaonya.
Baadhi ya wafanyikazi wanatafuta fedha za kutuma kwa serikali, lakini wakati mwingine, wameiba data au kuwadukua waajiri wao na kudai fidia.
Mwaka jana, mahakama ya Marekani iliwafungulia mashtaka raia 14 wa Korea Kaskazini ambao walidaiwa kujipatia dola milioni 88 wakifanya kazi kwa siri na kuyaibia makampuni ya Marekani kwa muda wa miaka sita.
Raia wengine wanne wa Korea Kaskazini ambao walidaiwa kutumia utambulisho ghushi kupata kazi za mbali za Teknolojia ya Mawasiliano katika kampuni ya sarafu ya mtandaoni nchini Marekani walishtakiwa mwezi uliopita.
Kupata kazi
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Jin-su alifanya kazi kwa miaka kadhaa kama mtaalamu wa Teknolojia ya Mawasiliano kwa serikali ya China kabla ya kuasi. Aliambia BBC kwamba yeye na wenzake walifanya kazi katika timu za watu kumi.
Ufikiaji wa mtandao nchini Korea Kaskazini umedhibitiwa, lakini wanasayansi hawa wa kompyuta wanaweza kufanya kazi kwa urahisi zaidi nje ya nchi. Ni lazima wafiche utaifa wao sio tu kwa sababu wanaweza kulipwa zaidi kwa kujifanya raia wa mataifa ya magharibi, lakini pia kwa sababu ya vikwazo vikali vya kimataifa vinavyokaibili Korea Kaskazini, hasa katika kukabiliana na silaha zake za nyuklia na programu za makombora ya balistiki.
Mfumo huu ni tofauti na shughuli za udukuzi za Korea Kaskazini, ambazo pia huchangisha fedha za kuendesha serikali.
Mapema mwaka huu, Kundi la Lazarus, kundi maarufu la udukuzi linaloaminika kufanya kazi Korea Kaskazini, japo hawaijawahi kukiri hilo, lilidaiwa kuiba dola bilioni 1.5 za Kimareka kutoka kwa kampuni ya Bybit inayoendesha biashara ya sarafu ya mtandaoni.

Jin-su alitumia muda wake mwingi kutafuta utambulisho ghushi ambao angeweza kutumia kuomba kazi. Mwanzoni alijifanya kuwa Mchina na kuwasiliana na raia wa Hungary, Uturuki, na nchi nyingine kuwaomba atumie utambulisho wao kwa makubaliano ya kuwalipa asilimia fulani ya mapato yake, aliambia BBC.
"Ukiweka 'sura ya Asia' kwenye wasifu huo, hutawahi kupata kazi."
Baadaye akatumia vitambulisho alivyopata kuwasiliana na watu wa Ulaya Magharibi ili kupata utambulisho wao, ambao aliutumia kuomba kazi Marekani na Ulaya. Jin-su mara nyingi alifanikiwa kuwalenga raia wa Uingereza.
"Baada ya mazungumzo mafupi, Waingereza walinipa utambulisho wao kwa urahisi sana," alisema.
Wataalamu wa teknolojia wanaozungumza Kiingereza kizuri wakati mwingine hushughulikia mchakato wa kutuma maombi. Lakini kazi zinazotangazwa kwenye tovuti za kujitegemea hazihitaji mahojiano ya ana kwa ana, na mwingiliano wa kila siku mara nyingi hufanyika kwenye majukwaa kama vile Slack, na hivyo kurahisisha njama yakutumia utambulisha wa mtu mwingine.
Jin-su aliambia BBC kwamba alilenga soko la Marekani, "kwa sababu mishahara ni ya juu katika makampuni ya Marekani." Alidai kuwa wafanyikazi wengi wa Teknolojia ya Mawasiliano walipata kazi ambazo mara nyingi kampuni ziliajiri Wakorea Kaskazini kadhaa bila kujua. "Hii hutokea sana," alisema.
Inaonekana kwamba wafanyakazi wa IT hupokea mapato yao kupitia mitandao ya wawezeshaji walioko mataifa ya Magharibi na China. Wiki iliyopita, mwanamke wa Marekani alihukumiwa kifungo cha zaidi ya miaka minane jela kwa kuwasaidia wafanyakazi wa Teknolojia ya Mawasiliano wa Korea Kaskazini kupata kazi na kuwatumia pesa.
BBC haikuweza kuthibitisha maelezo yaliyotolewa Jin-su, lakini kwa hisani ya PSCORE, shirika linalotetea haki za binadamu nchini Korea Kaskazini, tuliweza kusoma ushuhuda wa mwanasayansi mwingine wa kompyuta aliyeasi na kuthibitisha madai ya Jin-su.
BBC pia ilizungumza na mkaidi mwingine, Hyun-Seung Lee, ambaye alikutana na Wakorea Kaskazini wanaofanya kazi katika sekta ya Teknolojia ya Mawasiliano walipokuwa wakisafiri nchini China kama mfanyabiashara wa serikali. Alithibitisha kwamba walipo katika hali sawa.
Tatizo linalokuwa
BBC ilizungumza na mameneja kadhaa wa kuajiri katika sekta ya usalama wa mtandao na maendeleo ya programu ambao wanasema wamewatambua watu kadhaa wanaoshukiwa kuwa ni wanasayansi wa kompyuta wa Korea Kaskazini wakati wa mchakato wao wa kuajiri.
Rob Henley, mwanzilishi mwenza wa Ally Security nchini Marekani, hivi majuzi alikuwa akiajiri watu katika nyadhifa za mbali katika kampuni yake na anakadiria kuwa aliwahoji hadi wataalamu 30 wa wa KoreTeknolojia ya Mawasiliano wa Kaskazini wakati wa mchakato huo. "Mwanzoni, ilikuwa kama mchezo, kama kujaribu kukisia nani alikuwa halisi na nani alikuwa bandia, lakini mchakato huo ukawa wa kuchosha," alisema.
Hatimaye, aliamua kuwauliza wagombea wakati wa mawasiliano ya njia ya video wamuonyeshe kuwa ilikuwa mchana mahali walipokuwa.
"Tuliajiri Wamarekani pekee kwenye nafasi. Lakini sikuwahi kuona ikiwa mchana."
Mwezi Machi, Dawid Moczadło, mwanzilishi mwenza wa Vidoc Security Lab yenye makao yake Poland, alishiriki video ya mahojiano ya kazi ya mbali aliyofanya ambapo mgombeaji alionekana kutumia programu ya kijasusi bandia kuficha uso wake. Baada ya kushauriana na wataalamu, alisema anaamini mgombea huyo anaweza kuwa mtaalamu wa kompyuta kutoka Korea Kaskazini.
Tuliwasiliana na ubalozi wa Korea Kaskazini mjini London ili kuripoti madai hayo katika makala haya. Hawakujibu.














