Jinsi nchi za Magharibi zinavyoisaidia Urusi kufadhili uvamizi wake nchini Ukraine

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 6

Urusi inaendelea kupata mabilioni kutokana na mauzo ya mafuta na gesi inayouzwa nchi za Magharibi, kulingana na data iliyochambuliwa na BBC. Hivyo, Moscow inaendelea kufadhili uvamizi wake kamili wa Ukraine, ikiwa ni pamoja na kupitia mapato kutoka kwa mauzo ya nje ya hydrocarbon.

Mafuta na gesi huchangia karibu theluthi moja ya mapato ya bajeti ya Urusi na zaidi ya 60% ya mauzo yake ya nje.

Kufuatia uvamizi wa Urusi mnamo Februari 2022, washirika wa Ukraine waliweka vikwazo kwa hidrokaboni za Urusi. Marekani na Uingereza zimepiga marufuku uagizaji wa mafuta na gesi ya Urusi, wakati Umoja wa Ulaya umeweka marufuku kwa usafirishaji wa mafuta ghafi ya Urusi - lakini sio gesi.

Urusi inapata kiasi gani hasa?

Licha ya hayo, kulingana na Kituo cha Utafiti wa Nishati na Hewa Safi (CREA),kufikia Mei 29 Urusi ilikuwa imepokea zaidi ya euro bilioni 883 (dola bilioni 973) kutokana na mapato ya mauzo ya mafuta, mkiwemo euro bilioni 228 kutoka kwa nchi zilizoweka vikwazo.

Sehemu kubwa ya kiasi hiki, euro bilioni 209, ilitoka kwa nchi wanachama wa Ulaya (EU).

Mataifa ya EU yaliendelea kuagiza gesi ya bomba moja kwa moja kutoka Urusi hadi Ukraine iliposimamisha usafirishaji mnamo Januari 2025. Wakati huo huo, mafuta yasiyosafishwa ya Urusi yanaendelea kutosafirishwa kupitia mabomba hadi Hungaria na Slovakia.

Zaidi ya hayo, gesi ya Urusi inaendelea kutolewa Ulaya kupitia Uturuki - kwa viwango vinavyoongezeka kila wakati: kulingana na CREA, usambazaji wake mnamo Januari na Februari 2025 uliongezeka kwa 26.77% ikilinganishwa na kipindi kama hicho mnamo 2024.

Hungary na Slovakia pia zinaendelea kupokea gesi kupitia bomba la Urusi kupitia Uturuki.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Licha ya vikwazo vya Magharibi, mapato ya mafuta ya Urusi yalipungua kwa 5% tu mwaka 2024 ikilinganishwa na 2023, wakati kiasi cha mauzo ya nje kilipungua kwa 6%, kulingana na data ya CREA . Mwaka jana, mapato ya Urusi yaliyotokana na mauzo ya mafuta yasiyosafishwa yalikua kwa 6%, wakati mapato kutoka kwa mauzo ya gesi ya bomba yalikua kwa 9% kila mwaka.

Moscow inakadiria kuwa mauzo ya gesi inayopelekwa Ulaya yataongezeka kwa 20% mnamo 2024, wakati mauzo ya gesi asilia (LNG) yatafikia viwango vya juu vya rekodi. Hivi sasa, nusu ya mauzo ya nje ya LNG ya Urusi huenda kwa EU, CREA inabainisha.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas alisema EU haijaweka "vikwazo vikali zaidi" kwa mafuta na gesi ya Urusi kwasababu baadhi ya nchi zinahofia kuongezeka kwa mzozo na kwasababu kununua hidrokaboni za Kirusi "kulikuwa na bei nafuu kwa muda mfupi."

Uagizaji wa LNG haukujumuishwa katika duru ya 17 ya hivi karibuni ya vikwazo dhidi ya Urusi, lakini umoja huo umeidhinisha "ramani" ya kumaliza kabisa uagizaji wa gesi ya Urusi ifikapo mwisho wa 2027.

Mwanaharakati wa Global Witness Mai Rosner anaamini kwamba wanasiasa wengi wa Magharibi wanahofia kwamba kupunguza uagizaji wa mafuta kutoka Urusi kutasababisha bei ya juu ya nishati.

"Serikali nyingi hazina hamu ya kweli ya kuzuia uwezo wa Urusi wa kuzalisha na kuuza mafuta. Kuna hofu kubwa sana kwamba hii itamaanisha nini kwa masoko ya nishati duniani kote. Kuna mstari ambao, ukivuka, unaweza kusababisha masoko ya nishati kuharibiwa vibaya na kutupwa nje ya usawa," Mai Rosner aliambia BBC.

g

Chanzo cha picha, Thierry Monasse/Getty Images

Maelezo ya picha, Maandamano mbele ya makao makuu ya Lukoil nchini Ubelgiji mnamo Mei 2022

Mwanya wa Kusafisha Mafuta

Mbali na mauzo ya moja kwa moja, baadhi ya mafuta yanayosafirishwa na Urusi hufika Magharibi baada ya kutengenezwa katika nchi za tatu. Wakati mwingine mafuta ya Urusi hupunguzwa na mafuta yasiyosafishwa kutoka nchi nyingine.

CREA inasema imetambua viwanda vitatu vya kusafisha mafuta nchini Uturuki na vitatu nchini India vinavyosindika mafuta ya Urusi na kuuza mafuta yaliyopatikana kwa nchi ambazo zimeweka vikwazo. Kulingana na makadirio ya CREA, mitambo hii ilichakata mafuta ya Urusi yenye thamani ya Euro bilioni 6.1 kwa ajili ya kuuza baadae kwa nchi ambazo zimeweka vikwazo kwa hidrokaboni za Kirusi.

Wizara ya mafuta ya India imeikosoa ripoti ya CREA, na kuiita "jaribio lisilo la uaminifu la kuchafua sifa ya India".

"[Nchi hizi] zinajua kwamba nchi zilizoweka vikwazo ziko tayari kustahimili hali hii ya mambo. Hili ni pengo. Hili ni halali kabisa. Kila mtu anajua kulihusu, lakini hakuna anayefanya lolote kukabiliana nalo kwa umakini," anasema mchambuzi wa CREA Vaibhav Raghunandan.

Wanaharakati na wataalamu wanasema serikali za Magharibi zina zana zote za kuzuia mtiririko wa mapato ya mafuta na gesi kwenye hazina ya Kremlin.

Mai Rosner anasema kuwa kupiga marufuku usafirishaji wa mafuta wa Urusi kwenda Ulaya na kufunga mwanya wa kusafisha mafuta ya Urusi katika mamlaka ya Magharibi itakuwa "hatua muhimu katika kukamilisha mchakato wa mpito wa Magharibi kwa hidrokaboni za Urusi."

Kulingana na mchambuzi Vaibhav Raghunandan, EU inaweza kwa urahisi kuachana na uagizaji wa LNG ya Urusi.

"Asilimia hamsini ya mauzo ya nje ya Urusi yamafuta na gesi yanaenda kwa Umoja wa Ulaya, lakini hii ilichangia tu 5% ya jumla ya matumizi ya EU katika 2024. Kwa hivyo ikiwa EU itaamua kuachana kabisa na gesi ya Kirusi, itaiathiri Urusi zaidi kuliko watumiaji katika Umoja wa Ulaya," aliiambia BBC.

d

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Mapato ya mauzo ya nje huisaidia Urusi kupata silaha

Je, mpango wa Trump utafanikiwa?

Wataalamu waliohojiwa na BBC hawakukubaliana na wazo la Donald Trump kwamba vita vya Ukraine vitaisha ikiwa OPEC itapunguza bei ya mafuta.

Vaibhav Raghunandan anasema kuwa gharama za uzalishaji wa mafuta ghafi za Russia ni za chini kuliko zile za nchi za OPEC kama Saudi Arabia, kwa hivyo watateseka zaidi kutokana na bei ya chini ya mafuta kuliko Urusi.

"Saudi Arabia haitakubali kamwe jambo hili. Hili tayari limejaribiwa. Hii ilisababisha mzozo kati ya Saudi Arabia na Marekani," anasema.

Mai Rosner anasema kuwa kuna matatizo ya kimaadili na kiutendaji na nchi za Magharibi kununua hidrokaboni za Kirusi huku zikiunga mkono Ukraine kwa wakati mmoja.

"Sasa tuko katika hali ambayo tunamfadhili mshambuliaji katika vita ambavyo tunashutumu, na wakati huo huo tunafadhili upinzani dhidi ya vita. Utegemezi huu wa nishati ya mafuta inamaanisha kuwa kweli tuko kwenye huruma ya soko la nishati, wazalishaji wa nishati duniani na madikteta maadui," anasema.

Je, bajeti ya Urusi kwenye mafuta inategemewa kiasi gani?

Olga Shamina, mhariri wa uchumi wa BBC Russian Service:

Bajeti ya Urusi bado inategemea sana mapato ya mafuta na gesi. Mwishoni mwa mwaka jana, zilifikia rubles zaidi ya trilioni 11. Mapato yasiyo ya mafuta na gesi yalifikia zaidi ya ruble trilioni 25.

Kuanzia mwanzoni mwa 2025, bajeti ya Urusi itapata ruble trilioni 3.7 kutokana na mapato ya mafuta na gesi, na zaidi ya trilioni 8.5 kutoka kwa sekta zingine za uchumi.

Bajeti ya Urusi haiko katika hali nzuri hivi sasa, ingawa hakuna haja ya hofu. Kuanzia Mei 27, nakisi ya bajeti inazidi ruble trilioni 5-gharama ni kubwa zaidi kuliko mapato. Kwa kweli, mwanzoni mwa mwaka, mamlaka za Urusi zilikua zikitumia kikamilifu - uwezekano mkubwa, gharama hizi zinahusishwa kwa namna fulani na vita. Kulingana na data hii, tunaweza kuhitimisha kuwa hakuna mazungumzo bado ya kurekebisha uchumi wa Urusi kwa njia za amani.

Wakati huo huo, kutoka kwa mtazamo wa mapato, hatari zinaongezeka. Kwanza, bei ya mafuta inashuka. Mafuta ghafi ya Brent kwa sasa yanauzwa kwa $63.7 kwa pipa. Mafuta ya Kirusi kwa ujumla ni ya bei nafuu kuliko Brent. Na hiyo inamaanisha mapato ya mafuta pia yatapungua.

Pili, uchumi wa Urusi unakabiliwa ustawi wa 'pole pole' baada ya vita kutokana na matumizi mengi ya bajeti. Sasa, licha ya matumizi makubwa, kasi ya ukuaji wa uchumi inapungua. Na hii pia itamaanisha kupunguzwa kwa mapato ya ushuru, kwani kampuni zitapata kidogo.

Je, haya yote yanahatarisha sana bajeti? Bado, nakisi na deni la umma nchini Urusi kubaki chini. Lakini hali inabadilika; Wizara ya Fedha ya Urusi tayari imeanza kuzungumza juu ya kupunguza gharama mara kadhaa. Lakini hii inawezekana vipi wakati Urusi iko vitani haijulikani wazi.