Israel-Iran: Tunachokijua kuhusu usitishwaji mapigano uliopendekezwa na Trump

Chanzo cha picha, EPA-EFE/Shutterstock
Hatua ya "usitishaji mapigano sasa imeanza kutekelezwa. Tafadhali isikiukwe," aliandika Rais wa Marekani Donald Trump katika ujumbe uliochapishwa Jumanne kwenye jukwaa la mitandao yake ya kijamii la Truth Social.
Kulingana na ujumbe wa Rais wa Marekani, usitishwaji mapigano kati ya Iran na Israel, utaanza kutekelezwa "saa sita" baada ya tangazo lake.
"Usitishaji wa mapigano umekubaliwa kati ya Iran na Israel – baada ya saa sita kutoka sasa, baada ya Israel na Iran kukamilisha mashambulizi yao ya mwisho," Trump aliandika saa 7:30 usiku Jumanne, saa za Iran (saa za tisa unusu usiku kwa zaa za Afrika Mashariki).
Ratiba ya kusitisha mapigano
Kulingana na ratiba ya Donald Trump, usitishaji mapigano ulianza saa 12 kwa saa za Afrika Mashariki. Kulingana na rais wa Marekani, Hatimaye, ndani ya saa 24, mzozo wa siku 12 kati ya nchi hizo mbili utaisha.
Kabla ya usitishaji mapigano kati ya Israeli na Iran, uliopendekezwa na rais wa Marekani, kuanza kutumika, pande zote mbili zilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya kila mmoja. Jana usiku, vitongoji kadhaa huko Tehran na sehemu nyingine za Iran vilipigwa mabomu.
Iran pia ilirusha msururu wa makombora kwenda Israel, ambapo maafisa wa uokoaji wa Israel walisema yaliwauwa watu wasiopungua wanne.
Katika taarifa iliyotolewa na ofisi yake, Benjamin Netanyahu alisema amekubali pendekezo la kusitisha mapigano la Donald Trump na Iran. Taarifa hiyo ilisema kwamba Israel "imefikia malengo yake yote juu ya vituo vya nyuklia na makombora.
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araqchi alitangaza katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X: "Kama utawala wa Israei hautasitisha uchokozi wake haramu dhidi ya watu wa Iran ifikapo saa 10 asubuhi leo, pia hatutakuwa na budi kuendelea na majibu [mashambulizi]."
Waziri wa mambo ya nje wa Iran pia akaandika: "Mashambulizi yetu dhidi ya Israel yaliendelea hadi dakika ya mwisho."
Katika taarifa siku ya Jumanne, msemaji wa wizara ya afya ya Iran alisema watu 610 wameuawa na 4,746 wamejeruhiwa katika mashambulizi ya Israel tangu mzozo huo uanze.
Iran na Israel zajibizana
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Saa mbili baada ya Israel kusema kuwa imekubali mapatano hayo, Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilisema limegundua makombora yaliyorushwa kutoka Iran.
Waziri wa Ulinzi, Israel Katz aliishutumu Iran kwa "ukiukaji" wa masharti hayo, akiongeza kuwa aliagiza jeshi "kuendeleza na kuishambulia Tehran ili kupiga maeneo ya serikali na miundombinu ya kigaidi".
Jeshi la Iran lilikanusha kuwa lilirusha makombora baada ya usitishaji mapigano kuanza kutekelezwa.
Baadaye, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) lilisema kwamba "katika dakika za mwisho kabla ya usitishaji mapigano", lilishambulia "vituo vya kijeshi na vifaa" huko Israel.
Shirika la habari la Tasnim linaloshirikiana na IRGC liliripoti kuwa Israel ilianzisha mashambulizi ya kijeshi ya "awamu tatu" baada ya kusitishwa kwa mapigano.
Baraza Kuu la Usalama la Taifa la Iran hapo awali lilisema mashambulizi ya Israel "yatakabiliwa na jibu madhubuti, thabiti na kwa wakati muafaka na Iran".
IDF ilisema mashambulizi yaliibuka Jumatatu usiku hadi Jumanne. Wafanyakazi wa uokoaji walisema watu wanne waliuawa na 22 kujeruhiwa katika mji wa Beersheba.
Wakati huo, vyombo vya habari vya serikali ya Iran vilisema Iran ilirusha "makombora" dhidi ya Israel.
Trump amesema nini?
Katika chapisho kwenye mtandao wa kijami wa Truth Social, Trump ameihimiza Israeli - "usirushe mabomu" kwenda Iran.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Ikulu ya White House muda mfupi baadaye, Trump alisema "hana furaha" na Israel.
"Kulikuwa na roketi moja ambayo nadhani ilirushwa kutokea baharini baada ya muda uliopangwa wa kusitisha mapigano na sasa Israel inataka kufanya mashambulizi. Israel [inabidi] ijizuie," alisema.
Katika kauli ya ghadhabu alisema nchi hizo mbili hazijui wanachofanya.
Katika chapisho la baadaye, alisema: "Usitishaji wa mapigano unaendelea."
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi












