Jinsi wanajeshi wa Marekani walivyomkamata Saddam Hussein

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Saddam Hussein aliendelea kukimbia kwa muda wa miezi nane baada ya uvamizi ulioongozwa na Marekani nchini Iraq mwaka 2003 wa kumuondoa madarakani.
Hatimaye alikamatwa karibu na jiji la Tikrit Disemba 13. Vikosi vya Marekani viliomba msaada kwa raia wa Iraq, Dkt. Muafaq al-Rubaie kumtafuta.
Baada ya miezi kadhaa ya kumtafuta, Saddam Hussein alipatikana katika chumba cha chini ya ardhi katika nyumba ya shambani karibu na mji wa Tikrit.

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
"Mabibi na mabwana, tumempata," alitangaza msimamizi wa mamlaka ya mpito nchini Iraq baada ya uvamizi wa Marekani, Paul Bremer, katika mkutano na waandishi wa habari. Kila mtu aliyekuwepo alilipuka kwa furaha.
"Saddam Hussein alikamatwa Disemba 13, 2003 saa 2:30 usiku kwa saa za Iraq- kutoka katika chumba cha chini ya ardhi huko Adwar, kilomita 15 kusini mwa Tikrit. Nataka kusema kitu kwa watu wa Iraq. Leo ni siku ya kukumbukwa. Mamilioni yenu mmeonewa kwa miongo kadhaa na mtu huyu katili.”
Dkt. Mu'afaq al-Ruba'i ni nani?

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Katika miaka ya 1970, Saddam Hussein alipoingia katika siasa nchini Iraq - Dkt. Al-Rubai alikuwa gerezani. Saddam Hussein alikua rais wa Iraq kuanzia 1979, na Dkt. Rubai aliondoka Iraq mwaka huo.
Baada ya miaka 25 alirudi nyumbani - aliteuliwa katika utawala wa mpito uliowekwa na Marekani. Siku ambayo Saddam alikamatwa - Dkt. Rubai alikuwa katika mkutano. Akiwa hapo mtu wake wa karibu alikuja na kumwambia habari hiyo.
Akikumbuka wakati huo Dkt. Al-Rubai anasema, “niliingiwa na furaha. Sikuweza kujizuia, sikuweza kuifanya habari hiyo kuwa siri. Uso wangu ulisema kile kilichotokea, na wale waliokuwa kwenye mkutano pia walielewa mara moja."
"Mkutano ulivunjika ghafla, watu wakaanza kupiga kelele kwa furaha. Tulivuta pumzi ya matumaini."
"Baada ya Saddam Hussein kupinduliwa Aprili 9, 2003 na kukamatwa - watu wa Iraq hawakuamini kwamba utawala wa Saddam umeanguka."
Kupatikana kwa Saddam Hussein

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mwandishi wa BBC alielezea mahali hapo na kusema, "kwa kutazama harakaharaka ni vigumu kusema kilicho hapa. Kuna nyumba ndogo na vitu mbalimbali vimetawanyika karibu yake."
"Katika nyumba hii kuna shimo - lililofunikwa na uchafu. Ndani yake kuna mlango uliojificha, umefichwa kwa njia ambayo hauonekani kwa nje. "
''Baada ya miaka mingi ya kutawala mamilioni ya Wairaki kwa mkono wa chuma na miezi nane ya kukimbia majeshi yaliyompindua - hapa ndipo Saddam Hussein anapatikana. Mtu aliyekuwa akiishi katika Ikulu ya rais - amejificha kwenye shimo chini ya ardhi.''
Picha ya kwanza iliyotolewa baada ya kukamatwa inamuonyesha Saddam akiwa amechanganyikiwa, akiwa amelegea, akiwa na nywele ndefu na ndevu zimefunika uso wake.
Kijana wa Kiiraki anayeitwa Bashir aliwahi kufanya kazi na BBC - alishtushwa na picha hizo za kwanza.
"Nilishtuka. Picha yake kwenye TV ilionekana kama mtu wa pangoni. Nilimwona mtu ambaye alitawala Iraq kwa mkono wa chuma kama mfungwa. Lilikuwa jambo la kushangaza."

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Muafaq al-Rubai aliombwa na vikosi vya Marekani siku hiyo hiyo kuambatana na wanasiasa wengine kadhaa waandamizi wa Iraq kumtembelea Saddam Hussein, na kumtambua rasmi.
"Tulichukuliwa kwa helikopta hadi uwanja wa ndege wa Baghdad. Lengo kuu lilikuwa ni kuthibitisha kuwa mtu aliyekuwa na ndevu ndefu ni Sadam Hussein. Jenerali Sanchez aliyekuwa kamanda wa Marekani nchini Iraq. Aliniuliza kama nilitaka kwenda kumwona."
"Aliniuliza kama nataka kumuona kutoka upande wa pili wa dirisha la kioo, au kuzungumza naye kwenye simu, au kumuona moja kwa moja mbele yake."
"Nilisema - hapana, nataka kukutana naye uso kwa uso. Nataka kuzungumza naye na kumuuliza maswali. Sijawahi kumsahau tangu 1979.'' - anasema Muafaq Al Rubai.
Mazungumzo yake na Saddam Hussein

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
"Nilimwona akiwa amekaa katika ukingo wa kitanda ameinamisha kichwa. Amevaa nguo nyeupe na sweta. Nywele zake zimechafuka. Tulipewa viti vinne. Tulijitambulisha. Baada ya hapo nilimuuliza maswali mengi."
"Kwanza kabisa, niliuliza, kwa nini ulimuua Imam Sadr? Kwa nini uliishambulia Iran? Kwa nini uliikalia Kuwait? Kwa nini uliwapa sumu Wakurdi? Kusini mwa Iraq, mamilioni ya Washia waliuawa na kuna makaburi ya halaiki, kwa nini? Kwa nini maelfu ya watu waliuawa? Nilimtupia maswali mengi."
"Saddam Hussain alikuwa akidharau maswali yangu, wakati mwingine aliyapuuza kabisa, au alihalalisha matendo yake na akajibu kwa maneno yale yale aliyokuwa akisema alipokuwa madarakani."
Dkt. Al-Rubai alikuwa kwenye seli na Saddam kwa takriban saa moja. Alikuwa wa kwanza kuingia chumbani na wa mwisho kutoka.
"Sikutaka kuondoka bila kuuliza maswali yote niliyokuwa nayo. Pia nilifikiria ikiwa tutamuua mtu huyu. Ndipo ninaweza kutoka na kuwaambia watu habari njema kwamba Saddam hayuko hai tena.''

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
"Lakini baadaye, akili zangu zilirudi. Niliamini, hii ndiyo tofauti kati yangu na Saddam. Nataka ahukumiwe mbele ya watu - kesi ambayo itafungua ukurasa mpya katika historia ya Iraq."
"Kwa hiyo nilipotoka kwenye chumba hicho cha gereza, nilipumua. Nikamwambia - Saddam Hussein, laana ya Mungu iwe juu yako. Alianza kuzungumza kwa lugha chafu ya chinichini, akichanganya maneno yote machafu na kutukana."
Oktoba 2005, kesi ya Saddam Hussein ilianza huko Baghdad. Alihukumiwa kifo na kunyongwa tarehe 30 Disemba 2006.
Muaffaq al-Rubai alikuwa mshauri wa usalama wa taifa wa Iraq wakati huo. Alikuwa mmoja wa wale waliokuwepo wakati wa kunyongwa kwa Saddam.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Dinah Gahamanyi












