Mbio za Urais Iran: Wagombea wenye misimamo mikali watawala

ij

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, (Kutoka juu kushoto) Saeed Jalili, Mohammad Baqer Qalibaf, Masoud Pezeshkian, Mostafa Pourmohammadi, Amirhossein Qazizadeh Hashemi, na Alireza Zakani
    • Author, Kasra Naji
    • Nafasi, BBC

Baraza la Walinzi la Iran limeidhinisha wagombea sita kugombea katika uchaguzi wa rais wa mwezi huu.

Takribani wote ni watu wenye misimamo mikali ya Kiislamu na wako karibu na fikra za Kiongozi Mkuu Ayatollah Ali Khamenei.

Baraza hilo la kikatiba lilikagua watu 80 waliojiandikisha kusimama kama wagombea tarehe 28 Juni kulingana na sifa zao za kidini na kimapinduzi.

Inaonekana baraza hilo limewaidhinisha wagombea wenye misimamo mikali kushikilia kiti cha urais kufuatia kifo cha Rais Ebrahim Raisi katika ajali ya helikopta mwezi uliopita.

Wenye Misimamo Mikali

L

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Saeed Jalili alikuwa mpatanishi mkuu wa nyuklia wa Iran akiwakilisha ofisi ya kiongozi mkuu

Mgombea mmoja wa mstari wa mbele ni Saeed Jalili, katibu wa zamani wa Baraza Kuu la Usalama la Kitaifa na mpatanishi wa mazungumzo ya nyuklia ambaye anafikiriwa kuwa kipenzi cha Ayatollah Khamenei.

Katika wakati wake kama mkuu wa timu ya Iran ya mazungumzo ya nyuklia, Jalili mara kwa mara alikwamisha mazungumzo na mataifa matano yenye nguvu duniani huku Iran ikiendeleza mpango wake wa nyuklia.

Anaonekana na wengi kama mtu wa itikadi kali ya kiislamu na asiye na uzoefu wa uongozi.

Spika wa sasa wa Bunge, Mohammad Baqer Qalibaf, ni mgombea mwingine mwenye nafasi nzuri ya kushinda.

Yeye ni mtu wa ndani wa serikali na jenerali wa zamani wa Walinzi wa Mapinduzi ambaye pia amewahi kuwa mkuu wa polisi wa nchi hiyo na meya wa Tehran.

ED

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Mohamad Baqer Qalibaf aligombea kiti cha urais bila mafanikio mwaka 2005, 2013 na 2017.

Mmoja kati ya hao wawili anaweza kuamua kuondoka kwenye kinyang'anyiro hicho dakika ya mwisho ili asizigawanye kura.

Wagombea wengine watatu - Meya wa Tehran Alireza Zakani, Makamu wa Rais Amirhossein Qazizadeh Hashemi na Mostafa Pourmohammadi - pia ni watu wa misimamo mikali.

Pourmohammadi ni waziri wa zamani wa sheria na Waziri wa mambo ya ndani, pamoja na Ebrahim Raisi, walikuwa wanachama wa kile kilichoitwa "Kamati ya Kifo," iliyoidhinisha kunyongwa maelfu ya wafungwa wa kisiasa mwishoni mwa miaka ya 1980.

Msimamo wa Wastani

Asiyekuwa na misimamo mikali ni Massoud Pezeshkian, mbunge wa Tabriz. Mtu wa msimamo wa wastani, ana nafasi ndogo sana ya kushinda ikiwa kutakuwa na ushiriki mdogo wa wapiga kura.

Pezeshkian anatokea jamii ya Azeri, na inaaminika ana uungwaji mkono kutoka watu wa kaskazini-mashariki mwa Iran, ambapo idadi kubwa ya watu ni Waazeri wanaozungumza Kituruki.

Kumuwacha katika kinyang’anyiro hicho kunaweza kuwa ni ujanja wa kusukuma idadi kubwa ya watu wajitokeza kupiga kura - kwani vinginevyo idadi inaweza kuwa ya chini sana.

Majina yalioondolewa

K

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Aliyekuwa rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad hajaruhusiwa kugombea

Majina mawili makubwa ambayo yamenyimwa nafasi ya kugombea ni rais wa zamani mwenye misimamo mikali, Mahmoud Ahmadinejad na Ali Larijani, spika mara tatu wa bunge, akiwa na historia ya kuwa mtu wa dini na mwenye misimamo mikali.

Kukataliwa kwao kunaonyesha jinsi wapiga kura walivyo na chaguo finyu kuchagua miongoni mwa watu wachache wenye misimamo mikali ambao kiongozi mkuu anahisi anaweza kufanya kazi nao.

Kwa wagombea wa aina hiyo, hakuna uwezekano kwamba uchaguzi huo utaleta msisimko mkubwa miongoni mwa Wairani.

Wataona huu ni uchaguzi mwingine ambapo kiongozi mkuu ameunda wagombea ili kuleta matokeo anayoyataka - ya rais mwingine mwenye msimamo mkali.

Imetafsiriwa na Rashid Abdalla