Mganga anapohitaji mganguzi: Safari ya mtaalamu wa tiba ya akili aliyetaka kujiua

.
Maelezo ya picha, Toluse anasema safari yake ilimfundisha kuthamini jamii zaidi.
    • Author, Chigozie Ohaka, Carolyne Kiambo & Makuochi Okafor
    • Nafasi, Africa health, BBC News

Mwonekano wa Bahari ya Atlantiki, unapovuka daraja la tatu la bara huko Lagos, Nigeria, kunavutia sana .

Mawimbi yanapongeza ufuo huo, yakitengeneza bwawa kubwa la utulivu la ajabu.

Lakini kwangu, hali haikuwa hivyo kila wakati; kipindi fulani, ilikuwa kama ukumbusho wa taabu na kila kitu kisichopendeza.

Kutana na Toluse Francis, mtaalamu wa afya ya akili na mshauri mwenye umri wa miaka 35, anayetokea Lagos, Nigeria.

Makala hii inaangazia safari yake akipitia tatizo la sonona.

Licha ya dhana kwamba "wataalam wa magonjwa ya akili" wana kinga dhidi ya changamoto za tatizo hili, uzoefu wa Toluse unaonyesha vinginevyo.

Mwishoni mwa mwaka 2020, katika kilele cha janga la Covid-19, Toluse alianza kugundua kuwa taratibu anapoteza shauku katika nyanja nyingi za maisha.

Aliepuka kwenda kujivinjari na wengine, akaanza kukosa usingizi, na hakuwa na hamu ya kula.

Upweke ukawa mwandani wake wa kudumu. Muda si muda, akili yake ikaghubikwa na giza, na akawaza kujitoa uhai.

Duniani, mtu hujiua kila baada ya sekunde 40, na kupita vifo vya kila mwaka vinavyohusiana na vita.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2019, Afrika inaongoza kwa kiwango cha juu zaidi cha watu kutoa uhai.

.
Maelezo ya picha, Takwimu za WHO zinaonyesha nchi za Kusini mwa Afrika zina viwango vya juu zaidi vya kujiua katika bara hilo.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Takwimu zinaonyesha kuwa barani Afrika kuna daktari mmoja wa magonjwa ya akili kwa kila wakazi 500,000, mara 100 chini ya pendekezo la WHO.

Kwa shinikizo kama hilo kwa huduma, safari ya Toluse inaangazia swali muhimu: "Daktari wa mtaalamu wa magonjwa ya akili ni nani?"

Toluse mwanzoni alipuuza dalili za kile alichokuwa anapitia mwenyewe.

Alihangaika kutafuta msaada, akisumbuliwa na mawazo yaliyomuandama, "Toluse Francis, watu wanakuja kwako ili kupata usaidizi; ungeenda kwa nani ili usaidiwe?"

Hata hivyo, mnamo Desemba 2021, alijikuta katika mfadhaiko mkali na mawazo mengi ya kujiua.

Akiwa amekata tamaa, aliandika aliochokuwa akipitia kwenye mtandao wa WhatsApp, akisema, "Nadhani ni wakati wa mimi kuokolewa."

Ilikuwa hatua muhimu wakati marafiki walipojitokeza, wakitoa usaidizi wa kila aina.

Kuelezea hisia zake ikawa changamoto kubwa. Toluse alimweleza rafiki yake siri, akikiri, "Kwa kweli sijui kinachonitokea."

Rafiki huyo alimtia moyo atafute usaidizi wa kitaalamu, jambo lililomsukuma Toluse kupiga simu hiyo muhimu kwa daktari wa magonjwa ya akili.

Ilikuwa mwanzo wa safari yake ya uponyaji.

Toluse anasisitiza kwamba hakuna mtu anayetamani kifo; simu moja tu au kuingilia kati kunaweza kutoa mtazamo mpya juu ya maisha.

Alisema uzoefu wake unaangazia vichochezi vitatu vya kawaida vya sonona na mawazo ya kujiua: kuvunjika kwa uhusiano na kusababisha kujidharau na aibu, migogoro ya kifedha inayotokana na matatizo ya kiuchumi, na mfadhaiko wa siku za nyuma ambao haukutatuliwa.

Ndani ya mzunguko wake wa kitaaluma, Toluse mara nyingi husikia msemo, " Mganga Hajigangi."

Wakati mtaalamu wa magonjwa ya akili hubeba mizigo ya kihisia ya wengine, wao pia, wanahitaji njia ya kukabiliana na matatizo wanayokumbana nayo.

Ni mchakato wa kiafya ambao, kesi ya Toluse, ilitatizwa na kutengwa, na kuzidisha sonona.

Kutafuta usaidizi kulimfanya Toluse kuwa mnyenyekevu zaidi kwa kuwa alihurumia matatizo ya wateja wake katika kueleza matatizo yao ya ndani.

Ukweli ni kwamba, hakuna matibabu ya moja kwa moja kwa mawazo ya kujiua; badala yake, wataalamu hushughulikia hali za kimsingi za afya ya akili, kama vile sonona.

Katika kisa cha Toluse, tiba ya mazungumzo pekee haikutosha; dawa ikawa sehemu muhimu ya kupona kwake.

Anasisitiza tofauti: dawa hushughulikia biolojia, wakati tiba ya mazungumzo inalenga michakato ya mawazo na mitazamo.

Ingawa dawa inaweza kusababisha uraibu na kuathiri mwili kimetaboliki, Toluse alidumisha mtazamo mzuri, kuzuia utegemezi.

.

Chanzo cha picha, Toluse Francis/Instagram

Maelezo ya picha, Toluse sasa anatumia mtandao wake wa kijamii kuwatia moyo watu wengine ambao huenda wanakabiliana na matatizo ya akili kutafuta usaidizi wa kitaalamu.

Ili kusaidia uponyaji wake, Toluse alitekeleza mabadiliko ya mtindo wa maisha.

Alizingatia lishe yake na kuhakikisha anapata usingizi wa kutosha, alizidisha mwingiliano wa kijamii, na akachukua mapumziko ya miezi minne kutoka kazini, bila kuona wateja wake.

Yeye hupinga kujitibu kupitia mtandao, kwani makala za mtandaoni zinaweza kuzidisha hali ya mtu, zikisisitiza umuhimu wa kuwasiliana na mtu mwenye huruma katika simu yako ambaye huenda haelewi kabisa lakini anaweza kukuongoza kukusaidia.

Wengine walipendekeza "pepo wabaya" wa wateja wake walikuwa wamehamishia sonona yao kwake, dhana ambayo Toluse anakanusha kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa kisayansi.

Ujumbe wake uko wazi: bila kujali imani, msaada wa kitaalamu wa matibabu ni muhimu.

Toluse alisema kunusurika kwake kunaonyesha umuhimu wa kutafuta usaidizi wa kitaalamu anapokabiliana na changamoto za afya ya akili.

Anapinga hatua ya mgonjwa kutafuta kile kinachomtatiza kiafya kupitia mtandao, kwani makala za mtandaoni zinaweza kuzidisha hali ya mtu kuwa mbaya zaidi, na kusisitiza umuhimu wa kuwasiliana na mtu mwenye huruma katika simu yako ambaye huenda haelewi kabisa lakini anaweza kukuongoza kukusaidia.

Mawazo ya kujiua mara nyingi hukufanya ujisikie kutengwa, na kukushawishi kwamba kujitoa uhai ndio suluhisho pekee.

Ushauri wa Toluse: "usizingatie mawazo hayo; yakatae na uyapuuze, na ikiwa huwezi, tafuta msaada wa kitaaluma."

Anasisitiza uwezo wetu wa kudhibiti mawazo yetu, akituhimiza kukabiliana na fikra mbaya na kukumbatia mawazo yenye kuleta tija na kuridhika na safari ya maisha ya mtu binafsi.

Kwa muhtasari, kwa mtu yeyote anayepambana na changamoto za afya ya akili, Toluse anatoa maneno ya hekima: "usipitie hili peke yako; zungumza."

Safari ya Toluse imebadilisha kabisa mtazamo wake juu ya taaluma yake.

Ingawa hawezi kuelewa kikamilifu kile ambacho wengine wanapitia, anaweza kuwahurumia kwa sababu yeye mwenyewe amepitia hayo.

Ikiwa wewe au mtu unayemjua ana matatizo ya afya ya akili au mawazo ya kutaka kujiua, tafadhali tafuta usaidizi.

Unaweza kuzungumza na mtaalamu wa afya au shirika linalotoa usaidizi.

Utafiti na uchambuzi wa data na Brian Osweta.