Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Liang Wenfeng: Mjue mvumbuzi wa DeepSeek
Programu mpya ya akili mnemba (AI) iliyotengenezwa China, iitwayo DeepSeek, imezusha taharuki katika ulimwengu wa teknolojia, na kuleta changamoto kwa ChatGPT, programu ya bure inayotumiwa zaidi nchini Marekani.
Na mwanzilishi wake, bilionea Liang Wenfeng, amepata umaarufu wa mara moja nchini China. Programu hiyo ilizinduliwa wiki iliyopita. DeepSeek imeundwa kwa gharama nafuu – ikilinganishwa na AI nyingine za Marekani.
Rais Donald Trump amesema DeepSeek imeleta "wito wa uamsho" kwa kampuni za Marekani "yashindane ili yashinde."
Liang Wenfeng ni nani?
DeepSeek ilianzishwa Disemba 2023 na Liang Wenfeng. Ilitoa modeli yake ya kwanza ya lugha ya AI mwaka uliofuata. Hayajuulikani mengi kuhusu mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 40, ambaye alizaliwa kusini mwa Guangdong nchini China na kuhitimu Chuo Kikuu cha Zhejiang na shahada za uhandisi wa habari za kielektroniki na sayansi ya kompyuta.
Ni mara chache Liang, huonekana hadharani au kufanya mahojiano. Ni mwanzilishi pekee wa programu ya AI aliyechaguliwa kuhudhuria mkutano wa wajasiriamali na kiongozi wa pili mwenye nguvu China, Li Qiang.
Liang pia ana historia katika sekta ya fedha. Ni Mkurugenzi Mtendaji wa mfuko unaoitwa High-Flyer, ambao hutumia akili mnemba kuchanganua data za kifedha ili kufanya maamuzi juu ya fursa za uwekezaji.
Mwaka 2019, High-Flyer ilikuwa hazina ya kwanza nchini China kukusanya zaidi ya yuan bilioni 100 (dola za kimarekani milioni 13).
Timu yake ilitumia chipu za H800 zilizotengenezwa na mbunifu wa chipu, kampuni ya Nvidia. Mwaka 2023, alizindua DeepSeek, na akatangaza nia yake ya kuvumbua AI ya kiwango cha binadamu.
Kampuni hiyo ina wahitimu wa Shahada za Uzamivu kutoka vyuo vikuu vya China – mfano Peking, Tsinghua, na Beihang - na si wataalamu kutoka vyuo vya Marekani.
Kama ilivyo kwa TikTok, DeepSeek nayo inatoa malipo makubwa kwa wahandisi wake wa AI nchini China, pamoja na wafanyakazi walio katika ofisi zake za Hangzhou na Beijing.
Katika mahojiano na vyombo vya habari vya ndani mwaka jana, alisema timu yake kuu "haina watu waliosoma nje. Wote ni wa ndani. Tunapaswa kukuza vipaji sisi wenyewe."
Amesema sekta ya AI nchini China "haiwezi kubaki nyuma milele."
"Mara nyingi, tunasema kuna pengo la mwaka mmoja au miwili kati ya China na Marekani juu ya AI, lakini pengo halisi ni kati ya uhalisi na kuiga. Ikiwa hilo halitobadilika, China itakuwa nyuma siku zote."
Alipoulizwa ni kwa nini DeepSeek imewashangaza watu wengi huko Silicon Valley, Liang amesema: "Mshangao wao unatokana na kuona kampuni ya China ikijiunga na uvumbuzi wao kama mvumbuzi, na si mfuasi - kwani makampuni mengi ya China yamezoea kuwa wafuasi."
Ushindani wa DeepSeek
DeepSeek inatumia muundo wa R1. Programu hiyo inakadiriwa imetumiwa chipu kati ya 10,000 hadi 50,000, kulingana na MIT technology Review.
Chipu hizo ni muhimu kwa ajili ya kujenga muundo wenye nguvu wa AI, ambao unaweza kufanya kazi mbalimbali za binadamu, kama kujibu maswali hadi kutatua maswali magumu ya hesabu.
Septemba 2022, Marekani ilipiga marufuku uuzaji wa chipu zenye uwezo mkubwa kwa China. Liang alieleza kuwa hatua hiyo imeleta "changamoto kubwa," wakati wa mahojiano na vyombo vya habari vya China.
Programu kubwa za (akili mnemba) AI katika nchi za Magharibi hutumia takribani chipu zenye uwezo wa hali ya juu 16,000. Lakini DeepSeek inasema imeunda muundo wake wa AI, wa R1, kwa kutumia chipu za uwezo wa hali ya juu 2,000, na maelfu ya chipu za kiwango cha chini – na kuifanya programu yake kuwa ya gharama nafuu katika kuiunda.
Kwa mujibu wa watengenezaji wake, programu hiyo iligharimu dola za kimarekani milioni 5.6 kuiunda, ikilinganishwa na dola bilioni 5 zilizotumiwa mwaka jana na kampuni ya OpenAl kuunda programu ya akili mnemba ya ChatGPT.
Baadhi ya watu, akiwemo bilionea wa teknolojia wa Marekani Elon Musk, wametilia shaka madai ya DeekSeek, akisema kampuni hiyo haiwezi kufichua ni chipu ngapi za uwezo wa hali juu imetumia kwa sababu ya vikwazo.
Wataalamu wanasema vikwazo vya Washington vimeleta changamoto kwa sekta ya AI ya China.
"Vikwazo hivyo vimeyalazimisha makampuni za China kama DeepSeek kuwa wavumbuzi ili waweze kufanya mambo mengi na kutumia chipu kidogo," anasema Marina Zhang, profesa katika Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Sydney.
"Vikwazo hivi vinaleta changamoto, pia vimechochea ubunifu na ustahimilivu, kuendana na malengo mapana ya sera ya China ya kufikia uhuru wa kiteknolojia."
China yeye uchumi wa pili kwa ukubwa duniani imewekeza kwa kiasi kikubwa katika teknolojia - kutoka betri za magari ya umeme na paneli za jua, hadi AI.
Kuifanya China kuwa nchi yenye uwezo mkubwa wa teknolojia, ni malengo ya muda mrefu ya Rais Xi Jinping. Kwa hiyo vikwazo vya Washington ni changamoto ambayo Beijing iko tayari kupambana nayo.
Maoni mseto
Baada ya kuzinduliwa DeepSeek, imesababisha kushuka kwa thamani za hisa katika soko la teknolojia. Hisa za kampuni ya Nvidia, zilishuka kwa 17% siku ya Jumatatu. Hasara ya dola za kimarekani bilioni 600 kulingana na Bloomberg. Ni anguka kubwa zaidi katika historia ya soko la hisa la Marekani.
Marc Andreessen alichapisha kwenye X siku ya Jumapili, akisema "DeepSeek-R1 ni kama Sputnik," akimaanisha satelaiti ambayo ilikuwa chachu ya kuanzisha mbio za anga.
Yote kwa yote, programu hii pia imezusha maswali kwa watu wengi.
"Nadhani bado ukweli hatujaujua kuhusiana na kile kinachoendelea," anasema mchambuzi wa teknolojia Gene Munster, akizungumzia masuala ya gharama za kifedha ambazo DeepSeek imezieleza.
Waziri wa Sayansi wa Australia, Ed Husic alizungumzia masuala ya usalama. "Kuna maswali mengi ambayo yatahitaji kujibiwa kuhusu ubora, matakwa ya watumiaji, data na usimamizi wa faragha," aliiambia ABC. "Nitakuwa makini sana kuhusu mambo hayo. Masuala ya aina hii yanahitaji kupimwa kwa umakini."
Baadhi ya wataalamu wanaamini, kuwasili ghafla kwa DeepSeek kunaibua maswali kuhusu nguvu za Marekani katika AI na ukubwa wa uwekezaji ambao makampuni ya Marekani yanapanga.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa ana Ambia Hirsi