Jinsi akili mnemba inavyoweza kutatua tatizo la ugumba wa wanaume

Asilimia saba ya idadi jumla ya wanaume duniani wameathiriwa na ugumba. Lakini sasa akili mnemba inaweza kuwa na uwezo wa kutatua tatizo hili.

Dkt. Steven Wasileko anasema timu yake imetengeneza programu ya ambayo inaweza kutathmini idadi ya mbegu za kiume. Programu hiyo imetengenezwa kutokana na sampuli zilizochukuliwa kutoka kwa wanaume walio tasa.

Dkt. Steven ni mhandisi wa biolojia katika Chuo Kikuu cha Teknolojia, Sydney nchini Australia na mwanzilishi wa kampuni ya matibabu iitwayo NewGenics Biosciences.

Programu ambayo wametengeneza inaitwa 'Sperm Search.' Imeundwa kusaidia wanaume ambao hawana mbegu za kiume wakati wanapokojoa.

Matibabu ya sasa kwa wanaume wenye ugumba, sehemu ndogo ya tezi dume inatolewa kwenye upasuaji na kupelekwa maabara ambako majaribio yanafanywa kutafuta mbegu zenye afya kwa kutumia darubini na ikifanikiwa mbegu hizo hutibiwa. Na kisha zinaweza kutumika kwa uzazi.

"Mchakato huo unachukua saa sita hadi saba," anasema Dk Steven.

“Mtaalamu wa kiinitete anapotazama kupitia darubini, anachokiona ni mkusanyiko wa seli. Inawezekana kabisa - sehemu nzima ina mbegu kumi za kiume tu na mamilioni ya seli nyingine. Hii ni kama kutafuta sindano kwenye nyasi.”

“Kinyume chake, programu hii inaweza kupata mbegu zenye afya kwa sekunde,” anasema Dk Steven.

Timu ya Dkt. Steven inadai kwamba programu yao ni ya haraka mara elfu kuliko mtaalamu mwenye ujuzi.

“Ikumbukwe kuwa mfumo huu si mbadala wa wataalamu bali umeundwa ili kuwasaidia. Kasi hii ni muhimu sana kwa sababu wakati ni muhimu,” anasema mtaalamu wa dawa za uzazi katika Chuo Kikuu cha Dundee, Sarah Martins.

Kulingana na ripoti, idadi ya mbegu za kiume imepungua kwa nusu katika miongo minne iliyopita, na kufanya utasa wa kiume kuwa shida kubwa.

Sababu ya tatizo hili ni pamoja na uchafuzi wa mazingira na uvutaji sigara, chakula, ukosefu wa mazoezi na msongo wa mawazo.

Wataalamu Wengine

Dkt. Meorg Gallagher pia anajaribu kutafuta suluhisho la utasa wa kiume.

Yeye ni profesa msaidizi katika Chuo Kikuu cha Birmingham, katika kitengo cha madawa ya binadamu na anatumia mbinu mpya kufuatilia mkia wa manii na utendakazi kwa kutumia programu ya kupiga picha.

"Kufuatilia mkia wa manii kunatoa taarifa kuhusu afya ya manii kwa sababu mabadiliko madogo hutuambia ni kiasi gani manii inakaribia kufa au ikiwa inaitikia kichocheo cha nje," anaeleza.

Kampuni ya Belfast Examin pia inatumia mbinu ya kutambua uharibifu wa DNA kwenye manii. Profesa Sheena Lewis na timu yake wamekuwa wakifanya kazi kwa miaka 20.

Profesa mstaafu katika Chuo Kikuu cha Queen, ambaye pia ni mtendaji mkuu wa Examiner, anasema akili bandia inavutia sana, lakini fani ya dawa inasonga kwa kasi ndogo.

“Utafutaji wa manii, kwa mfano, kwa sasa uko katika hatua ya nadharia, baada ya kupimwa hapo awali kwa wagonjwa saba pekee. Haitoshi,” anasema Profesa Lewis.

“Inaweza kuchukua miaka miwili hadi mitano kuthibitisha mbinu hizi. Itachukua muda mrefu. Pili, ni kwa ajili ya idadi ndogo ya wanaume. Chochote utakachofanya kitakuwa kizuri lakini si kwa kila mtu.”

Dkt. Steven huko Sydney anasema ugunduzi wake ndio bora kwa sasa.

“Ikiwa tunaweza kuwasaidia wataalamu wa kiinitete kufanya kazi vizuri zaidi, kwa usahihi zaidi, watapata manii ambayo hawakuweza kupata hapo awali. Mwanamme ataweza kupata nafasi ya kuwa baba wa watoto wake,” anasema Dkt. Steven.

Timu yake sasa inapeleka programu yao katika majaribio ya kliniki.