DeepSeek: Programu ya China ya akili mnemba (AI) inayozungumzwa duniani

Muda wa kusoma: Dakika 5

Programu ya akili mnemba iliyotengenezwa nchini China inayoitwa DeepSeek, imepakuliwa na watumiaji wengi kwenye Apple Store.

Programu hiyo ilitolewa tarehe 20 Januari 2025, na kuwavutia wataalamu wa AI, kabla ya kuingia kwenye macho ya sekta nzima ya teknolojia na duniani kwa ujumla.

Rais wa Marekani Donald Trump amesema ni "wito wa uamsho" kwa makampuni ya Marekani ambayo lazima "yashindane ili kushinda."

Kinachoifanya DeepSeek kuwa ya kipekee ni madai ya kampuni hiyo kuwa imeundwa kwa gharama ndogo, kwa sababu inatumia chipu chache za uwezo mkubwa, ikilinganishwa na programu kubwa ya AI ya OpenAI.

Madai hayo yamesababisha kampuni kubwa ya kutengeneza chipu ya Nvidia kupoteza karibu dola za Kimarekani bilioni 600 (£482bn) ya thamani yake katika soko siku ya Jumatatu - hasara kubwa zaidi kwa siku moja katika historia ya Marekani.

DeepSeek pia inazua maswali juu ya juhudi za Washington za kudhibiti ushawishi wa Beijing katika teknolojia - moja ya vidhibiti hivyo ni kupiga marufuku usafirishaji wa chipu zenye uwezo mkubwa kwenda China.

Rais Xi Jinping ametangaza kuwa teknolojia ya AI ni kipaumbele kikubwa kwa sasa. DeepSeek ni muhimu kwani China ni gwiji katika utengenezaji wa nguo na samani na sasa inashindana katika teknolojia ya chipu, magari ya umeme na AI.

Pia unaweza kusoma

DeepSeek ni nini?

Kwa lugha nyepesi DeepSeek ni programu ya (chatbot) inayoendeshwa na akili mnemba (AI), kama vile ChatGPT.

Hii ni programu ya bure inayopatikana kwenye Apple. DeepSeek inasema imeundwa "kujibu maswali yako na kuboresha maisha yako."

Ni AI inayotumia muundo (modeli) unaoitwa R1 – ambao una vipengele bilioni 670, na kuifanya kuwa modeli kubwa zaidi ya lugha miongoni mwa programu za AI, kulingana na Anil Ananthaswamy, mwandishi wa kitabu cha Why Machines Learn: The Elegant Math Behind Modern AI.

Inaripotiwa kuwa na nguvu kama modeli ya OpenAI iitwayo O1 - ambayo inaendesha ChatGPT - katika hisabati, usimbaji na kujenga hoja.

Kama miundo mingine mingi ya AI za China - DeepSeek imeundwa kukwepa maswali nyeti ya kisiasa.

BBC ilipouliza programu hiyo ni nini kilitokea katika uwanja wa Tiananmen Square tarehe 4 Juni 1989, DeepSeek haikutoa maelezo yoyote kuhusu mauaji hayo, mada ambayo ni mwiko nchini China.

Ilijibu: "Samahani, siwezi kujibu swali hilo. Mimi ni AI iliyoundwa kutoa majibu ya manufaa na yasiyo na madhara."

Udhibiti wa serikali ya China unaelezwa kuleta changamoto kubwa kwa maendeleo ya AI.

Inaaminika imeundwa kwa gharama nafuu - watafiti wanadai iligharimu dola milioni 6 (£4.8m). Gharama kidogo ikilinganishwa na mabilioni ya pesa yaliyotumiwa na makampuni ya AI nchini Marekani.

Waliwezaja hasa kuiunda kwa gharama kidogo, ni jambo ambalo halijuulikani. Inaelezwa mwanzilishi wa DeepSeek alitumia chipu za Nvidia aina ya A100, ili kuitengeneza. Ni chipu ambazo zimepigwa marufuku kuingizwa China tangu Septemba 2022.

Wataalamu wanaamini mkusanyiko wa chipu hizo - wanakadiria ni chipu 50,000 - ulimfanya atengeneze programu ya AI yenye nguvu, kwa kuunganisha na chipu za bei nafuu zisizo na uwezo mkubwa.

Nani mwanzilishi wa DeepSeek?

DeepSeek ilianzishwa Disemba 2023 na Liang Wenfeng, na ilitoa modeli yake ya kwanza ya AI mwaka uliofuata.

Hakuna mengi yanayojulikana kuhusu Liang, mhitimu wa Chuo Kikuu cha Zhejiang katika digrii za uhandisi wa habari za kielektroniki na sayansi ya kompyuta. Na sasa yuko katika uangalizi wa kimataifa.

Hivi karibuni alionekana kwenye mkutano ulioandaliwa na waziri mkuu wa China, Li Qiang, akionyesha uwezo wa DeepSeek katika sekta ya AI.

Bw Liang pia ana historia katika fedha. Ni mkurugenzi Mtendaji wa mfuko unaoitwa High-Flyer, ambao hutumia AI kuchanganua data za kifedha ili kufanya maamuzi ya uwekezaji katika maeneo yenye fursa. Mwaka 2019 High-Flyer ilikuwa hazina ya kwanza nchini China kukusanya zaidi ya yuan bilioni 100 (dola milioni 13).

Katika mahojiano ya nadra mwaka jana, alisema sekta ya AI ya China "haiwezi kubaki nyuma milele."

Aliendelea: "Mara nyingi, tunasema kuna pengo la mwaka mmoja au miwili kati ya China na Marekani katika AI, lakini pengo lenyewe ni kati ya uhalisia na kuiga. Ikiwa hilo halitabadilika, China siku zote itakuwa inafuata nyuma nyuma tu."

Alipoulizwa ni kwa nini DeepSeek imewashangaza watu wengi huko Silicon Valley, amesema: "Mshangao wao unatokana na kuona kampuni ya China ikijiunga nao kama mvumbuzi, sio mfuataji nyuma – jambo ambalo makampuni mengi ya China yamezoea kuwa nyuma nyuma."

Makampuni ya Marekani yataathirika?

Mafanikio ya DeepSeek yanapunguza imani juu ya bajeti kubwa na chipu za kiwango cha juu kuwa ndizo njia pekee za kuendeleza AI, na kuleta mashaka kuhusu mustakabali wa chipu zenye uwezo mkubwa.

"DeepSeek imethibitisha kuwa miundo ya kisasa ya AI inaweza kuendelezwa kwa rasilimali chache," anasema Wei Sun, mchambuzi wa AI katika Kituo cha utafiti cha Counterpoint.

"OpenAI, yenye thamani ya dola bilioni 157, inakabiliwa na changamoto ya kudumisha ukuu wake katika uvumbuzi au kuhalalisha matumizi yake makubwa bila kuleta faida kubwa."

Gharama za chini za DeepSeek ziliathiri masoko ya fedha tarehe 27 Januari, na kusababisha kampuni ya Nasdaq kushuka zaidi ya 3% katika mauzo ya njea, yanayojumuisha chipu na vituo vya data duniani kote.

Nvidia inaonekana kuathirika zaidi kwani bei yake ya hisa ilishuka kwa 17% kwa siku nzima. Ni kampuni kubwa ya kutengeneza chipu, yenye thamani kubwa zaidi duniani, lakini ilipopimwa kwa mtaji wa soko, imeanguka hadi nafasi ya tatu nyuma ya Apple na Microsoft siku ya Jumatatu.

Forbes imeripoti kuwa thamani yake ya soko imeshuka hadi dola za kimarekani trilioni 2.9 kutoka dola trilioni 3.5.

China inasemaje?

Kupanda kwa DeepSeek kumeiinua serikali ya China, ambayo imekuwa ikitaka kujenga teknolojia isiyoitegemea Magharibi.

Chama cha Kikomunisti bado hakijatoa maoni, lakini vyombo vya habari vya serikali ya China vinaeleza kuwa makampuni makubwa huko Silicon Valley na Wall Sreet "yanakosa usingizi" kuhusu DeepSeek, ambayo "imelipindua" soko la hisa la Marekani.

"Nchini China, maendeleo ya DeepSeek yanasherehekewa kama ushahidi wa kuongezeka kwa uwezo wa kiteknolojia na kujitegemea kwa nchi hiyo," anasema Marina Zhang, profesa katika Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Sydney.

"Mafanikio ya kampuni hiyo yanaonekana kama uthibitisho wa uvumbuzi wa China. Enzi mpya ya teknolojia ya nyumbani inayoendeshwa na kizazi kipya cha wajasiriamali."

Lakini pia anaonya kuwa hisia hii ya furaha inaweza kusababisha China "kutengwa katika sekta ya teknolojia."

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi