Kwa nini jiji la Lagos linaweza kuamua mshindi wa uchaguzi Nigeria

Chanzo cha picha, Nduka Orjinmo/BBC
Wakati Nigeria inapojiandaa kwa uchaguzi mkuu wa Februari 25, kitovu chake cha kibiashara cha Lagos kinatoa taswira ya vyama pinzani vinavyotaka kuunda mustakabali wa nchi hiyo - wale wanaoonekana kuridhika na hali ilivyo sasa na wale wanaotaka mabadiliko.
Jimbo hilo lina idadi kubwa zaidi ya wapiga kura waliojiandikisha - milioni saba - na limeibuka kama uwanja muhimu wa vita katika kinyang'anyiro ambapo kila upande unaungwa mkono na kundi la vijana, wengi wao wakijumuisha theluthi moja ya Wanigeria ambao hawana kazi au wanatekeleza majukumu hayafikia sifa zao.
"Aliwahi kubuni nafasi za kazi hapo awali na ataifanya hivyo tena," alisema Jimoh Adesina, 40, dereva wa mabasi ya umma huko Lagos ambaye anamuunga mkono Bola Tinubu wa chama tawala cha All Progressives Congress (APC).
Ingawa kuendesha basi la umma ni kazi nzuri, hungetarajia mtu aliye na shahada kutoka kwa chuo cha kiufundi afanye, lakini Bw Adesina anafurahi walau kuwa kazini tu.
Ukosefu wa ajira na uchumi ni masuala muhimu kwa wapiga kura katika uchaguzi. Licha ya kuwa nchi kubwa zaidi ya kiuchumi barani Afrika na mzalishaji wa mafuta, Wanigeria wanne kati ya 10 wanaishi chini ya dola moja kwa siku, kulingana na Benki ya Dunia.
Bw Tinubu ameegemeza kampeni yake ya urais kutokana na mihula yake miwili kama gavana wa jimbo la Lagos, na mafanikio ya chama alichosaidia kukiingiza mamlakani mwaka wa 2015.
Haya yanaonekana wazi kupitia mradi wa mabasi ya mwendo kasi vyema (BRT) aliyoanzisha ili kupunguza msongamano wa magari unaoshuhudiwa sana jijini.

Chanzo cha picha, GIFT UFUOMA/BBC
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mtu tajiri zaidi barani Afrika, Aliko Dangote, anajenga kiwanda cha kusafisha mafuta katika eneo la biashara huria ambalo sehemu yake inamilikiwa na serikali, karibu na bandari mpya iliyojengwa na Wachina sasa inafanya kazi na kuna mazungumzo ya daraja la nne kuunganisha bara la wafanyikazi na wilaya za biashara katika kisiwa hicho.
Miradi hii yote imebadilisha Lagos kutoka jiji la machafuko lililokuwepo kabla ya mwaka 1999.
Sehemu kubwa ya Lagos ya kisasa imetokana na juhudi za Bw Tinubu au imetekelezwa na wafuasi wake waliyomemrithi tangu 2007.
"Yeye ni baba yangu," alisema Bw Adesina, ambaye anasema Bw Tinubu alimlipia karo akiwa na wanafunzi wengine katika shule za umma mwaka wa 2001, na pia kumpa kazi hii ya udereva.
Yeye ni mmoja wa baadhi ya watu nchuni Nigeria ambao maisha yao yameguswa na ukarimu wa Bw Tinubu, ama kupitia rasilimali za serikali au utajiri wake binafsi.
Orodha hiyo inawajumuisha nyota wa soka, wanamuziki, wanasiasa ambao alifadhili kampeni zao na biashara alizoziokoa katika nyakati ngumu.
Ndio maana kauli mbiu yake ya uchaguzi ni Emi Lokan, ambayo inatafsiri kwa urahisi kuwa It Is My Turn, kimsingi ni mwito wa kutaka ukarimu ulipwe ili kuunga mkono azma yake ya urais.

Chanzo cha picha, NDUKA ORJINMO/BBC
Mfalme sasa anataka kuwa mfalme.
Ijapokuwa chama chake kimepoteza uungwaji mkono baada ya miaka minane madarakani, ufuasi wake mashinani unaipatia nafasi nzuri ya ushindi na Bw Tinubu anapanga kuzuru majimbo yote nchini Nigeria.
"Wale anaokutana nao maisha yao yanabadilika na wengine wananufaika kwa njia isiyo ya moja kwa moja," alisema Adekanye Adetutu, mfuasi mwenye bidii ambaye pia alilipiwa karo akiwa mwanafunzi wa shule ya upili.
Lakini wapinzani wanasema Bw Tinubu ametumia ukarimu kama huo kuimarisha mfumo wa ufadhili ili kuunda msingi wa wafuasi waaminifu, kujenga himaya ya kisiasa na kushikilia rasilimali za serikali.
"Tinubu anapaswa kuondoa mguu wake kwenye shingo zetu," alisema Daniella Brodie-Mends, mpiga kura wa mara ya kwanza mwenye umri wa miaka 25 katika uwanja wa zamani wa wakoloni huko Lagos ambapo maelfu walikusanyika kwenye mkutano wa mwisho wa Chama cha Labour, ambacho mgombea wake Peter Obi anapendwa na wapiga kura wa mijini.
Umati wa watu katika Uwanja wa Tafawa Balewa ulikuwa sawa na ule uliokusanyika kwenye lango la Lekki la kukusanya kodi wakati wa maandamano ya EndSars ya 2020, ambayo yaliendesha kampeni dhidi ya ukatili wa polisi na kisha kubadilika kuwa vuguvugu la kushinikiza utawala bora katika taifa hilo lenye watu wengi zaidi barani Afrika.
Ni wachanga, wanajiamini na wengi ni matajiri, wanatumia simu mpya za iPhone na vyatu vya Yeezy kando na kutoboa pua, kuwa na nywele za rasta maarufu dreadlocks na kuchora tattoo, ingawa msaada wake hauko kwa watu wa tabaka la kati.
Wengi hawa wamezaliwa wakati Bw Tinubu na wengine wakabiliana na serikali ya kijeshi ya Sani Abacha katika miaka ya 1990, au walikuwa bado watoto wachanga alipokuwa gavana kati ya 1999-2007.
Lakini hawana muda wa kuangazia sifa zake za kidemokrasia na kwani wanawakilisha ujasiri wa kizazi kipya cha vijana wa Nigeria ambao wanahisi kwamba wanasiasa wa zamani wanaoendesha nchi wamekuwa kizingiti kwao na wanataka wawapishe.

Chanzo cha picha, NDUKA ORJINMO/BBC
Wao sio waaminifu kwa mtu yeyote, hawataki pesa kutoka kwa serikali au kazi za wafagiaji wa barabarani, wadhibiti wa trafiki na wahudumu wa bustani ambayo inatolewa ba Bw Tinubu kwa wingi mjini Lagos.
Wao ni marafiki na wajasiriamali vijana wa teknolojia ambao biashara zao zimefaulu katika jiji hilo na wanafahamu fika fursa zilizopo jijini Lagos mazingira yakiboreshwa.
"Nilikuwa nikienda likizo barani Ulaya kila msimu wa joto kabla ya hii APC kuingia mamlakani," alisema mwanamume mmoja ambaye alifika kwenye mkutano huo akiwa na kofia nyingi za Chama cha Labour.
Licha ya uhusiano wake wa zamani na chama kikuu cha upinzani cha Peoples Democratic Party (PDP), Bw Obi anachukuliwa kuwa mtu wa nje ikilinganishwa na wanasiasa ambao wafuasi wake wanawashutumu kwa kurudisha nyuma Nigeria.
Mzee huyo mwenye umri wa miaka 61 ameahidi kukomboa uchumi wa Nigeria kutokana na utegemezi wa kuagiza bidhaa kutoka nje kwa kujenga mazingira ambayo mauzo ya nje yatachochea ukuaji, na ameegemeza kampeni yake kwenye usimamizi wa busara wa fedha za umma wakati alipohudumu kwa mihula miwili kama gavana wa jimbo la Anambra mashariki.
Ameendesha kampeni mahiri, akiwatembelea wanavijiji maskini katika maeneo ya mbali ambako ana umaarufu mkubwa, na kuingia kwake Lagos, kwa kishindo kutoka sehemu moja ya jiji hadi nyingine kulitoa taswira ya gwaride la ushindi.

Chanzo cha picha, EPA
Lakini katika hali ya kutia wasiwasi kabla ya siku chache kabla ya uchaguzi, makumi ya wafuasi wake walishambuliwa na kujeruhiwa wakiwa njiani kuelekea ukumbini.
Ni hali ambayo iliwahi kusitokeza hasa katika uchaguzi mkuu wa 2019 ambapo upigaji kura katika ngome za upinzani ulitatizwa mjini Lagos na wapiga kura wengi kuzuiwa kupiga kura.
Mashambulizi kama hayo kwa kawaida hufanywa na magenge ya majambazi yenye nguvu mjini Lagos ambao hupatikana katika viwanja vya magari na masoko.















