Israel na Hezbollah: Dhoruba inayoliweka eneo la Mashariki ya kati hatarini

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Tunaanza na tahariri kutoka gazeti la Uingereza, The Guardian, "Israel na Hezbollah: Dhoruba inayoliweka eneo la Mashariki ya katika hatarini."
Gazeti hilo linasema Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Anthony Blinken, alizungumzia juu ya mvutano unaongezeka kati ya Israel na Hezbollah, alipozungumza huko Washington siku ya Jumanne, akisema, "sidhani kama pande zote mbili, zinataka kuona vita au migogoro ukipanuka.”
Gazeti hilo linasema, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Yisrael Katz alisema wiki hii, uamuzi kuhusu vita na Hezbollah utatolewa hivi karibuni, na majenerali wa jeshi wamesema mipango yao ya kuishambulia Lebanon imetiwa saini.
Hezbollah ilitoa picha za ndege zisizo na rubani zikionesha maeneo ya Israel ikiwa ni pamoja na miundombinu muhimu huko Haifa, na kiongozi wake, Hassan Nasrallah, alionya juu ya vita vikali.
Gazeti hilo linasema miezi minane iliyopita imeonyesha kuwa pade hizo mbili zimeshambuliana kwa tahadhari, licha ya kutoleana kauli za vitishio, lakini uwezekano wa kutokea vita kamili umeongezeka.
Gazeti hilo linaeleza, wakazi wengi wa kaskazini mwa Israel walipata hofu kutokana na uvamizi wa Hamas wa tarehe 7 Oktoba, na Hezbollah imeonyesha kuwa ina uwezo wa kuitishia Israel.
Gazeti hilo linasema, maelfu ya watu tayari wamekimbia makazi yao huko Lebanon na Israel. Makumi ya watu wameuawa, pamoja na mamia ya wapiganaji wa Hezbollah na wanajeshi wa Israel.
Gazeti linasema Israel imeshindwa kufikia malengo yaliyotangazwa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu huko Gaza, ambayo ni kuiondoa Hamas na kuwarudisha mateka, katika kipindi cha miezi minane - zaidi ya Wapalestina 37,000 wameuawa.
Gazeti hilo linasema kila upande una sababu ya kuepuka vita, kwani Hezbollah imeimarika, lakini Iran haitaki kupoteza nguvu yake dhidi ya mashambulizi kwenye vituo vyake vya nyuklia.
Gazeti hilo linasema Lebanon tayari inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi, na haitaki kuongeza mgogoro.
Ikiwa vita kamili vitazuka, vitakuwa tishio kwa Israel kwa njia ambayo uvamizi wa Gaza haukuleta tishio kama hilo, na Marekani imeonya kuwa ulinzi wa Israel wa makombora kaskazini unaweza kuelemewa.
Gazeti hilo linahitimisha kwa kusema, Netanyahu hausikilizi utawala wa Biden, na amevuka mstari wa Biden, na hali ya sasa ni mbaya, na suluhisho lipo katika diplomasia, sio vita.
Serikali ya Netanyahu inaporomoka na inakaribia mwisho wake

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Gazeti la Israel, The Jerusalem Post kuna makala ya Amotz Ask yenye kichwa "Serikali ya Netanyahu inaanguka na inakaribia mwisho wake."
Mwandishi analinganisha na kile kinachotokea Israel na maandamano ya kupinga Vita vya Vietnam mwaka 1969, wakati Marekani iliposhuhudia maandamano makubwa dhidi ya Vita vya Vietnam.
Mwandishi anasema, maandamano yanatikisa Jerusalem na Tel Aviv. Maandamano yanayomkabili Netanyahu ni mwanzo wa uasi uliosubiriwa kwa muda mrefu, na yanachochewa na imani kwamba vita hivi vinahusishwa na taasisi yake ya kifisadi.
Mwandishi anasema, Vita vya Vietnam vilizusha maandamano Marekani kwa sababu nyingi, lakini sababu kuu ilikuwa ni mfumo mbovu wa kuandikisha watu jeshini ambao uliwapendelea baadhi ya watu na kuwapeleka vitani wengine.
Anasema mfumo wa kujiandikisha kwenda vitani wa Netanyahu ni mbaya zaidi, na ndivyo wapinzani wa Chama cha Likud wanavyoelewa kuwa, kile ambacho kiongozi huyo hatakata tamaa nacho, ndicho kitakacho mwangusha.”
Mwandishi anasema wapinzani wa Likud na waandamanaji mitaani wanasema, Israel inahitaji mwanzo mpya.
Siku Ifuatayo: Kwa Gaza au kwa serikali ya Netanyahu?

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Tunageukia gazeti la Al-Quds Al-Arabi, tahariri yake ya "Siku Ifuatayo: Kwa Gaza au kwa serikali ya Netanyahu?"
Gazeti hilo linasema Daniel Hagari, msemaji wa jeshi la Israel, alitoa taarifa muhimu Jumatano iliyopita, alisema mazungumzo ya wanasiasa wa Israel, wakiongozwa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, kuhusu uwezekano wa kuitokomeza kabisa harakati ya Hamas ni “uwongo kwa umma na udanganyifu."
Gazeti hilo linasema kisingizio cha kuiondoa Hamas kinatumika kuhalalisha kuendelea vita dhidi ya Gaza, na kukwepa azimio la hivi karibuni la Baraza la Usalama la usitishaji vita.
Katika muktadha wa kumpa Netanyahu fursa, kama baadhi ya wachambuzi wa Israel wanavyosema, kuchelewesha kuondoka serikalni.
Gazeti hilo linasema Netanyahu anatumia vita dhidi ya Gaza kama sababu ya kuzuia Mahakama ya Juu ya Israel kusitisha maamuzi ya serikali, na kukwepa kufunguliwa mashitaka.
Sehemu ya pili ya mkakati huu imejikita katika kuongeza idadi ya watiifu wake, kutoka vyama vya kidini vya misimamo mikali ya Kizayuni.
Gazeti hilo linaamini Netanyahu alilifanya tatizo ni ucheleweshaji wa Washington katika kuipa Israel silaha ili kuiondoa Hamas, na wala si kukataa kwake kutii azimio la Baraza la Usalama la kusitisha vita.
Gazeti hilo linamalizia kwa kusema, “ni vigumu, kutabiri yajayo, lakini ndoto za Netanyahu za kuiondoa Hamas zinaweza kugeuka, ili tushuhudie kesho ya Netanyahu na serikali yake.”
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla












