Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Watoto wa marais waliopitia masaibu baada ya wazazi wao kutoka Ikulu
- Author, Mariam Mjahid
- Nafasi, BBC Swahili
- Muda wa kusoma: Dakika 8
Dalitso Lungu, mwana wa rais wa zamani Edgar Lungu ameamriwa na mahakama ya Zambia arejeshe magari 79 na vipande 23 vya ardhi pamoja na majengo, ikiwemo kituo cha biashara, kituo cha mafuta, "ghorofa za kifahari na makazi ya hadhi ya juu" katika mji mkuu, Lusaka. Kisa?, ameshindwa kueleza alikotoa utajiri huo. Haya yanajiri baada ya babake mzazi aliyekuwa rais wa nchi hiyo kustaafu na kisha kufariki dunia mwaka jana.
Kuzaliwa katika familia ya kiongozi mkuu serikalini sio kuzaliwa tu; La hasha! Ni kuzaliwa ndani ya hadithi ambayo tayari imeandikwa kwa macho ya umma.
Mtoto anakuwa nembo, ishara, na wakati mwingine shabaha. Wakati baba au mama yuko madarakani, mlango wa dunia hufunguka kwa urahisi. Lakini mlango huo huo unaweza kujifunga kwa kishindo.
Kwa baadhi yao, dhoruba haishii kwenye kuondoka madarakani. Wazazi wao wanapoondoka kwa kun'golewa, kushindwa uchaguzi, au kifo, ndiyo safasi ya misukosuko ya maisha yao huanza.
Wanapojifurukuta kuanza upya, huandamwa na kesi za ufisadi au hata wengine kuozea jela.
Historia ya kisiasa ya dunia imejaa mifano ya familia zilizotoka kileleni hadi ukingoni.
Makala haya yanaorodhesha watoto wa marais walioshindwa kuikimbia historia na jina la familia limewasakama kila mahali wanakokwenda ni huyu ni ''mtoto wa fulani''.
Dalitso Lungu- Mtoto wa rais wa zamani wa Zambia
Wa hivi karibuni ni mtoto wa kiume wa aliyekuwa rais wa zamani wa Zambia ambaye anaandamwa na kesi chungu nzima.
Alichokivuna wakati babake alipokuwa madarakani kinamsakama kooni baada ya kushindwa kuelezea alifanya biashara gani halali hadi kupata mali zenye thamani ya zaidi ya dola milioni 1.3 za Marekani (£923,000).
Mawakili wa kijana huyo mwenye umri wa miaka 39 wamedai kuwa watakata rufaa dhidi ya uamuzi wa Kitengo cha Uhalifu wa Kiuchumi na Kifedha katika Mahakama Kuu.
Na upande wa mahakama kuu umeeleza hukumu hiyo imetokana na kugundua kuwa licha mtoto huyo wa aliyekuwa rais kufanya kazi katika kampuni ya vinjwaji na kuhamia katika Mamlaka ya ushuru Zambia ujumla wa mshahara amepokea hauwezi kumtajirisha kiasi hicho.
Edgar Lungu, aliyeiongoza Zambia kwa miaka sita kuanzia mwaka 2015, alifariki dunia nchini Afrika Kusini mwezi Juni mwaka jana, lakini bado hajazikwa kutokana na mvutano wa kisheria unaoendelea kati ya familia yake na serikali ya sasa.
Saif al-Islam Gaddafi (Libya)
Baada ya kuanguka kwa utawala wa Muammar Gaddafi mwaka 2011, mtoto wake wa kiume Saif al- Islam Gaddafi alichagua ukimya, lakini jamii bado haikumshahau.
Saif al-Islam aliyesomea nchini Uingereza alihudumu kama mwanadiplomasia, lakini sifa yake iliharibiwa wakati wa maasi ya 2011, alipoapa kwamba Libya itageuka "mito ya damu" ikiwa maandamano dhidi ya utawala wa baba yake yataendelea.
Baada ya kuporomoka kwa serikali, alikamatwa na wanamgambo wakati alipokuwa akijaribu kutoroka nchini, kulingana na ripoti.
Alizuiliwa kwa miaka sita huko Zintan, na mwaka 2015 na hatimaye hukumiwa kifo mahakama ya Tripoli - uamuzi ambao baadaye ulibatilishwa chini ya msamaha.
Maisha ya Saif yaligeuka uwanja wa mapambano.
Mnamo mwaka wa 2015, mahakama ya Libya ilitoa hukumu kifo dhidi ya Saif al-Islam kwa tuhumu za uhalifu wa kivita wakati wa mapinduzi ya 2011.
Pia alishtakiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Jinai ICC, kwa tuhuma za uhalifu dhidi ya ubinadamu. Juhudi za mawakili wake kufuta kesi hiyo hazikufua dafu na hivyo kuacha mashtaka hayo bila kutatuliwa kwa miaka mingi.
Vita hivi vya kisheria vilimweka Seif al-Islam katika uangalizi wa kimataifa, licha ya kuishi maisha ya kutoonekana ndani ya Libya.
Saif ameng'angana kurejea mamlakani na kuhuisha utawala wa babake walakin amefariki dunia Februari 04 2026 katika hali tatanishi na kuondoa moja ya alama za mwisho za enzi ya utawala wa Gaddafi.
José Filomeno dos Santos, mtoto wa aliyekuwa rais wa Angola
Mnamo Agosti 14, 2020, mwana wa rais wa zamani wa Angola alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kwa kosa la udanganyifu, baada ya dola milioni 500 za Marekani (£378m) kuhamishwa kutoka Benki Kuu ya Angola kwenda kwenye akaunti nchini Uingereza.
José Filomeno dos Santos na watu wengine watatu walihukumiwa, akiwemo gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Angola.
Uhamisho huo wa fedha ulikubaliwa mwaka 2017, katika wiki za mwisho kabla ya baba yake kujiuzulu urais baada ya kuongoza kwa miaka 38.
Hii ndiyo hukumu kubwa ya kwanza ya ufisadi nchini Angola tangu mabadiliko ya uongozi yalipotokea.
José Filomeno dos Santos, anayejulikana pia kama Zenu, alikaa jela kwa miezi saba kwa tuhuma za ufisadi kabla ya kuachiliwa huru Machi.
Alikuwa mwanachama wa kwanza wa familia ya rais wa zamani kufunguliwa mashtaka kama sehemu ya kampeni ya kupinga ufisadi iliyoongozwa na Rais Lourenço.
José Eduardo dos Santos alikuwa rais kuanzia mwaka 1979 hadi alipojiuzulu mwaka 2017. Nafasi yake ilichukuliwa na João Lourenço, aliyekuwa waziri wake wa ulinzi na ambaye alikuwa amemteua mwenyewe kuwa mrithi wake.
Armando Ndambi Guebuza - Mwana wa aliyekuwa rais Msumbiji
Mnamo mwaka wa 2022,07 Disemba, Mahakama nchini Msumbiji ili mhukumu kifungo cha miaka kadhaa jela mwana wa rais wa zamani, wakuu wawili wa zamani wa idara ya ujasusi, pamoja na watu wengine 8 kwa kuhusika kwao katika kashfa ya ufisadi ambapo serikali ilijaribu kuficha madeni makubwa, hatua iliyosababisha msukosuko mkubwa wa kifedha nchini humo.
Armando Ndambi Guebuza, mwana wa rais wa zamani Armando Guebuza, alihukumiwa kifungo cha miaka 12 jela. Wengine waliotiwa hatiani walipewa adhabu ya kifungo cha kati ya miaka 10 na 12.
"Armando Ndambi Guebuza hakuonyesha majuto yoyote kwa kutenda kosa hilo, na bado anasisitiza kwamba amelengwa kwa sababu za kisiasa," alisema Jaji Efigenio Baptista wa Mahakama ya Jiji la Maputo.
Katika mwenendo wa kesi hiyo, Jaji Baptista alieleza kuwa Ndambi Guebuza alichukua hatua hizo kwa makusudi "ili kumshawishi baba yake" na kuishinikiza serikali kuidhinisha ununuzi wa vyombo vya majini.
Kwa mujibu wa mahakama, alipokea rushwa ya dola milioni 33 za Marekani ili kukidhi "tamaa yake ya maisha ya kifahari." Jaji aliorodhesha baadhi ya mali alizopata kwa fedha hizo, zikiwemo magari ya kifahari na jumba lenye thamani ya randi milioni 10 (sawa na dola 590,000) nchini Afrika Kusini.
Mbali na kifungo cha jela, mtoto wa Guebuza pia aliamriwa kulipa faini ya metikali 162,000 (takribani dola 2,500).
Haya yalijiri, baada ya Armando Guebuza, ambaye aliwahi kuwa Rais wa Msumbiji kutoka 2005 hadi 2015, kustaafu kutoka kwa urais wa chama tawala cha Frelimo mnamo Machi 2015.
Duduzile Zuma-Sambudla (Afrika Kusini)
Duduzile Zuma-Sambudla, mwanasiasa na binti wa rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma, anakabiliwa na mashtaka ya kuchochea vurugu za umma na ugaidi.
Mashtaka hayo yanatokana na machafuko makubwa yaliyotokea Julai 2021 nchini Afrika Kusini, hasa katika majimbo ya KwaZulu-Natal na Gauteng. Machafuko hayo yalizuka kufuatia kufungwa kwa baba yake jela kwa kosa la kuidharau mahakama.
Waendesha mashtaka wanadai kuwa machapisho yake kwenye mitandao ya kijamii wakati wa vurugu hizo yalichangia kuchochea ghasia. Machafuko hayo yalisababisha vifo vya mamia ya watu na uporaji mkubwa wa mali katika maeneo mbalimbali.
Kesi yake bado haijaanza kusikilizwa kikamilifu mahakamani, na Duduzile anakanusha mashtaka yote, akisisitiza kuwa hana hatia.
Isabel dos Santos - Angola
Isabel dos Santos, binti wa rais wa zamani wa Angola José Eduardo dos Santos, aliwahi kutajwa kama mwanamke tajiri zaidi barani Afrika.
Hata hivyo, utajiri wake ulianza kuchunguzwa kwa kina baada ya baba yake kuondoka madarakani mwaka 2017.
Mnamo Januari 2020, mamlaka za Angola zilimshtaki kwa tuhuma za ubadhirifu, utakatishaji wa fedha, matumizi mabaya ya madaraka na udanganyifu, zinazohusiana na kipindi chake alipokuwa mwenyekiti wa kampuni ya mafuta ya taifa, Sonangol.
Waendesha mashtaka wanadai kuwa yeye na washirika wake walijipatia zaidi ya dola bilioni moja za Marekani kutoka fedha za umma.
Mashtaka hayo yalifuatia uchunguzi uliojulikana kama Luanda Leaks, uliofanywa na Muungano wa Kimataifa wa Waandishi wa Habari za Uchunguzi (ICIJ), uliotegemea zaidi ya nyaraka 715,000. Nyaraka hizo zilieleza jinsi alivyodaiwa kupata hisa katika sekta mbalimbali za Angola kupitia amri za urais na mikataba iliyoungwa mkono na serikali.
Mahakama nchini Angola na Ureno zimeamuru mali zake zizuiwe kutumika.
Aidha, shirika la kimataifa la polisi (Interpol) lilitoa notisi nyekundu kwa ombi la Angola ili kusaidia kumtafuta na kumkamata kwa madhumuni ya kisheria.
Hata hivyo, Isabel dos Santos amekanusha tuhuma zote, akizitaja kuwa ni njama za kisiasa zinazolenga kumwandama.
Wakati historia inapogeuka
Mwanafalsafa Aung San Suu Kyi alisema ''Si mamlaka yanayoharibu, bali ni hofu. Hofu ya kupoteza mamlaka huwaharibu wale wanaoyashikilia."
Kwa muktadha huu, viongozi wengi barani Afrika hujipata wakikwamilia madarakani na wengine kuanza kuwaleta karibu wanao ili kuwarithisha mamlaka.
Kwa bahati, mbaya mambo yakienda fyongo hasa kama wametawala kwa udikteta wanapoachia ngazi, vizazi vyao hujipata matatani na inakuwa rahisi jina lao walilokuwa wakitamba nalo kuingia doa au kusahaulika baada ya miongo kadhaa.
Wachanganuzi wa siasa za kimataifa wameeleza kuwa ''mamlaka si ya kudumu, urithi unaweza kuwa baraka au laana.''
Na kupitia hadithi za watoto wa marais wanaopambana kujinasua kutoka kwa kivuli cha dola, ni dhahiri kwamba mamlaka hupita lakini majina hubaki.