Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Mwanaume mwenye silaha auawa baada ya kukaribia makazi ya Trump

Mwanaume huyo alikuwa amebeba bunduki na kopo la mafuta aliposimamishwa kabla ya kupigwa risasi na maafisa wa Secret Service na polisi

Muhtasari

Moja kwa moja

Rashid Abdallah

  1. Ghasia zazuka Mexico baada ya mlanguzi wa dawa za kulevya El Mencho kuuawa

    Wimbi la vurugu limezuka nchini Mexico baada ya mlanguzi mkubwa wa dawa za kulevya nchini humo kuuawa katika operesheni ya kumkamata iliyohusisha idara ya ujasusi ya Marekani.

    Nemesio Oseguera Cervantes, anayejulikana kama "El Mencho", alikuwa kiongozi wa genge la dawa za kulevya la Jalisco New Generation (CJNG) alifariki baada ya kujeruhiwa vibaya katika mapigano kati ya wafuasi wake na jeshi siku ya Jumapili.

    Wafuasi wanne wa CJNG waliuawa wakati wa operesheni hiyo katika mji wa Tapalpa, katika jimbo la Jalisco, na wanajeshi watatu pia walijeruhiwa, imesema wizara ya ulinzi ya Mexico.

    Kumeshuhudiwa vurugu katika majimbo kadhaa, huku CJNG ikifunga barabara kwa magari yanayoungua.

    Jumapili nzima, kulikuwa na ripoti za watu wenye silaha mitaani huko Jalisco na kwingineko.

    Gavana wa Jalisco, Pablo Lemus Navarro, alitangaza hali ya hatari katika jimbo la Guadalajara, akisimamisha usafiri wote wa umma na kufuta matukio ya halaiki na shule kufungwa.

    Watalii waliozungumza na Reuters waliuelezea mji wa mapumziko wa Puerto Vallarta, Jalisco, kama "eneo la vita."

    Vizuizi vya barabarani takriban 250 viliwekwa kote nchini wakati wa machafuko, huku 65 vikiwa Jalisco.

    Baraza la mawaziri linasema watu 25 wamekamatwa, 11 kwa madai ya kushiriki katika vitendo vya vurugu na 14 zaidi kwa madai ya uporaji.

    Maduka yaliteketezwa kwa moto na takriban matawi 20 ya benki yalishambuliwa katika vurugu hizo.

    Rais wa Mexico Claudia Sheinbaum amesema maafisa wa majimbo na shirikisho wamedhibiti vurugu hizo, akiwahimiza watu kuwa "watulivu.

    Sheinbaum aliongeza kuwa "katika sehemu nyingi za nchi, shughuli zinaendelea kama kawaida".

    Mashirika kadhaa ya ndege yamefuta safari za ndege kwenda Jalisco, ikiwa ni pamoja na Air Canada, United Airlines na American Airlines.

    Marekani imewaonya raia wake kujificha katika majimbo matano: Jalisco, Tamaulipas, maeneo ya Michoacán, Guerrero na Nuevo Leon.

    El Mencho, afisa wa zamani wa polisi mwenye umri wa miaka 59, aliendesha shirika kubwa la uhalifu linalohusika na usafirishaji wa kiasi kikubwa cha kokeini, methamphetamine na fentanyl kwenda Marekani.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani iliahidi zawadi ya dola milioni 15 (£11.1m) kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa El Mencho.

    Pia unaweza kusoma:

  2. Wanafunzi wa Iran waandamana kwa siku ya pili katika baadhi ya vyuo vikuu

    Wanafunzi wamefanya maandamano katika vyuo vikuu kadhaa vya Iran kwa siku ya pili siku ya Jumapili, kulingana na mashirika ya habari ya ndani na machapisho ya mitandao ya kijamii, huku Iran ikikabiliwa na ongezeko la uwepo wa jeshi la Marekani wakati wa mazungumzo kuhusu nyuklia.

    Machafuko mapya yanafuatia maandamano ya kupinga serikali mwezi uliopita ambapo maelfu ya watu waliuawa katika machafuko mabaya zaidi tangu Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ya 1979.

    Televisheni ya serikali ya Iran ilionyesha video za kile ilichosema ni watu "wanaojifanya wanafunzi" wakiwashambulia wanafunzi wanaounga mkono serikali huko Tehran ambao walikuwa wakishiriki katika maandamano ya kulaani ghasia za Januari.

    Maandamano pia yalifanyika katika vyuo vikuu huko Mashhad kaskazini mashariki, kulingana na video zilizochapishwa na kundi la haki za binadamu lenye makao yake Marekani la HRANA.

    Siku ya Jumamosi video inayodaiwa ya waandamanaji katika Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Sharif cha Tehran inaonesha wakimlaani Kiongozi Mkuu Ayatollah Ali Khamenei kama "kiongozi muuaji", na wakimtaka Reza Pahlavi, mwana wa Shah aliyepinduliwa Iran, awe mfalme mpya.

    Maandamano ya hivi karibuni, ambayo yalianza Desemba kuhusu ugumu wa kiuchumi, yamegeuka kuwa ya kisiasa.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Trump ashangaa kwa nini Iran 'haijasalimu amri'

    Rais wa Marekani Donald Trump anahoji kwa nini Iran bado "haijasalimu amri" licha ya ongezeko la shughuli za kijeshi la Washington huko Mashariki ya Kati, amesema mjumbe maalum wa rais wa Marekani Steve Witkoff.

    Witkoff ameiambia Fox News siku ya Jumamosi kwamba Trump ana “hamu ya kujua" msimamo wa Iran baada ya kutishia kufanya shambulio dogo la kijeshi ikiwa makubaliano hayatafikiwa kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran.

    Marekani na washirika wake wa Ulaya wanashuku Iran inaelekea kutengeneza silaha ya nyuklia, jambo ambalo inakanusha.

    Ndani ya Iran, maandamano ya kupinga serikali yalifanyika katika vyuo vikuu kadhaa mwishoni mwa juma - maandamano ya kwanza ya kiwango hicho tangu yale ya Januari, ambapo maelfu ya watu wakiuawa.

    Katika mahojiano yake na Fox News, Witkoff amesema: "Sitaki kutumia neno 'kuchanganyikiwa'... kwa sababu yeye [Trump] anaelewa ana njia mbadala nyingi, lakini ana hamu ya kujua kwa nini hawajafanya hivyo... yaani kwa nini hawajasalimu amri."

    "Kwa nini, chini ya shinikizo la aina hii, nguvu za majini tulizonazo, kwa nini hawajatwambia, 'Hatutaki silaha za nyukilia."

    "Bado ni vigumu kuwafikisha mahali hapo," mjumbe wa Trump aliongeza.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi alisema Jumapili anaamini bado kuna uwezekano kwamba mzozo huo unaweza kutatuliwa kidiplomasia.

    Katika maoni tofauti siku mbili zilizopita, Araghchi alisema Tehran ikiandaa "rasimu ya makubaliano" na itaikabidhi kwa Witkoff katika siku chache zijazo.

    Maafisa wa Marekani na Iran walijadili mpango wa nyuklia wa Iran katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja huko Geneva, Uswisi, tarehe 17 Februari. Walisema maendeleo yamepatikana.

    Oman - ambaye ndiye mpatanishi wa mazungumzo hayo - alitangaza Jumapili kwamba duru inayofuata ya mazungumzo "imepangwa kufanyika Geneva Alhamisi hii."

    Pia unaweza kusoma:

  4. Greenland yakataa meli ya matibabu ya Trump

    Waziri mkuu wa Greenland amemwomba Rais wa Marekani Donald Trump kuzungumza naye badala ya kutoa "matamshi katika mitandao ya kijamii," baada ya Trump kusema Marekani imetuma meli ya matibabu ili kutoa "huduma" kwa watu kisiwa hicho.

    Trump aliandika kwenye Truth Social kwamba anatuma meli iliyojaa vifaa vya matibabu, akidai "watu wengi" kisiwani humo ni wagonjwa na "hawatunzwi".

    Jens-Frederik Nielsen alijibu "tunakataa," na akasema Greenland hutoa huduma ya afya bila malipo kwa raia wote, tofauti na Marekani.

    Trump amekuwa akikitaka kisiwa kikubwa cha arctic kwa muda mrefu - lakini alikubali mwezi Januari kwamba hatokichukua.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Mwanaume mwenye silaha auawa baada ya kukaribia makazi ya Trump

    Mwanaume mwenye silaha ameuawa kwa kupigwa risasi baada ya kukaribia eneo la makazi ya Rais wa Marekani Donald Trump huko Mar-a-Lago, Florida, imesema Idara ya Usalama wa rais.

    Mwanaume huyo alikuwa amebeba bunduki na kopo la mafuta aliposimamishwa kabla ya kupigwa risasi na maafisa wa Secret Service na polisi, imesema Idara hiyo.

    Tukio hilo lilitokea Jumapili asubuhi, wakati rais alipokuwa Washington DC.

    Mshukiwa ametajwa kama Austin T Martin kutoka Cameron, North Carolina, kulingana na CBS.

    Familia yake huko North Carolina iliripoti kupotea kwake mapema Jumapili asubuhi, Ofisi ya Polisi ya Kaunti ya Moore imesema katika taarifa kwa BBC.

    Ofisi hiyo imesema haina historia yoyote ya uhalifu inayomhusu Martin.

    Mwanaume huyo alipigwa risasi baada ya kukataa amri, amesema mkuu wa polisi wa kaunti ya Palm Beach, Ric Bradshaw.

    "Maneno pekee tuliyomwambia yalikuwa 'acha vitu hivyo' ikimaanisha kopo na bunduki," Bradshaw aliuambia mkutano na waandishi wa habari.

    "Aliweka chini kopo la gesi, akainua bunduki yake hadi mahali pa kufyatua risasi," alisema.

    Maafisa walimpiga risasi.

    Aliongeza kuwa maafisa hao walikuwa wamevaa kamera za mwili na hakuna maafisa waliojeruhiwa.

    Usalama huko Mar-a-Lago ni mkali sana, ukiwa na uzio wa nje wa polisi wa Palm Beach na ule wa ndani unaosimamiwa na Idara ya Usalama wa rais.

    Trump amekuwa shabaha na majaribio kadhaa ya mauaji.

    Julai 2024, Trump alipigwa risasi sikioni alipokuwa amesimama mbele ya umati wa watu huko Butler, Pennsylvania.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Hujamboa na karibu

    Nakukaribisha katika taarifa zetu za moja kwa moja, leo Jumatatu tarehe 23/2/2026