Fahamu utawala wa wake za marais Marekani

Mke wa rais wa kwanza kabisa nchini Marekani Martha Washington hakuwa na mtangulizi wake na alitegemea zaidi mfumo wa Ulaya aliposhika nafasi hiyo.

Mtunzaji wa makumbusho Gwendolyn DuBois Shaw alizungumza na BBC kuhusu utamaduni wa wake za marais tangu mwanzo na jinsi ulivyobadilika.

"Kwasababu hakukuwa na utamaduni wa ufalme Marekani, majukumu ya awali ya wake wa rais yaliegemea sana utawala wa ukoloni wa Uingereza".

Martha alipokuwa hadharani, watu walimuita Lady Washington kwasababu hiyo ndio lugha waliokuwa wamerithi kumuita mwanamke wa hadhi yake. Jina la 'Mama wa Taifa' lilianza mwisho wa karne ya 19."

katika utawala wake, Bi. Martha alionekana kutoa taswira ya kuwa yeye ndio mama wa taifa na alihitaji kuheshimiwa, jambo ambalo watu walifurahia kutekeleza.

Mrithi wake Abigail Adams, mke wa rais John Adams, ambaye werevu na dhamira yake ilijitokeza kipindi chake, yeye alijihusisha zaidi na siasa, akipigania haki za wanawake, elimu na kuondolewa kwa utumwa. "Alipendelea kuitwa mke wa rais lakini watu hawakupenda hivyo, walichukulia hitaji hilo kama majivuno au kimbelembele," amesema DuBois Shaw.

Bi. Adams, kama wake wengine wa marais, alionekana kuishi kwa niaba ya mume wake. "Kitu kizuri ni kwamba wanawake hawa walikuwa na akili kweli, walivutiwa sana na siasa na wenye ndoto lakini tatizo la jinsia lilikuwa kikwazo cha wao kuingia madarakani hadi karne ya 20," amesema DuBois Shaw.

Wake wengi wa marais walitegemea nguvu ya mume 'rais'

"Mary Lincoln alikuwa na hamu kweli ya kuingia kwenye siasa… alitaka hasa kuwa mke wa rais kwasababu binafsi hangeweza kuwa rais," anasema DuBois Shaw.

"Alipoingia Ikulu akaanza kutajwa kwa sifa mbaya. Watu walimzungumzia kama mwenye majivuno na fidhuli, lugha ambayo hii leo inafahamika sana na wanawake maarufu katika siasa na wafanyabiashara. Hakukubalika kama mtu mwenye weledi wa kisiasa kwasababu ya jinsia yake."

Wakiwa hawana njia nyingine, idadi kubwa ya wake wa marais walitegemea nguvu kidogo waliokuwa nayo kwasababu ni mke wa rais.

Naye, Dolley Madison, alikuwa mwanamke mwenye majukumu ya heshima kwa Thomas Jefferson kabla ya kuendelea na majukumu hayo James Madison alipokuwa rais, na alifahamika kwa ujuzi wake wa kidiplomasia katika kuwapatanisha waliokuwa mahasimu na mikakati mizuri ya kujenga urafiki na wanasiasa wakiume na wake zao.

"Mengi ya hayo sasa hivi ni historia lakini idadi kubwa ya wake wa marais walifikia malengo yao kwa njia hizo karne ya 19 na mapema karne ya 20 walipokuwa hawana njia yoyote ya kutimiza ndoto zao," amesema mtunzaji wa eneo la maonesho.

Karne ya 20

Kuanzia karne ya 20, majukumu ya mke wa rais yakaanza kungaziwa sana na umma. Kwasababu bado majukumu yake hayajafafanuliwa wazi, kumekuwa na gumzo katika vyombo vya habari na maoni ya watu kutofautiana juu ya kile hasa mama wa taifa anastahili kufanya na kuchochea zaidi mijadala ya nafasi ya mwanamke katika jamii.

Eleanor Roosevelt bila shaka alikuwa mmoja wa mama wa taifa mwenye ushawishi. Kwasababu Rais Franklin D Roosevelt alikuwa na ugonjwa wa polio, Eleanor alijipata mara nyingi akijitokeza hadharani kwasababu ya shughuli moja hadi nyingine.

Wakati mdororo wa kiuchumi ulipofika kilele chake, alisafiri sana kufikia miradi iliyokuwa imetengwa na serikali kukabiliana na hali hiyo na wakati wa vita vikuu vya pili vya dunia alisafiri kote duniani akitembelea wanajeshi wa nchini hiyo waliokuwa wamepelekwa maeneo mbalimbali.

Hata hivyo, ingawa alikuwa na ushawishi kwa umma kulikuwa na wengi waliomkosoa wakidai anataka kuwa maarufu mno.

DuBois Shaw aliona bango la kampeni ya chama cha Democratic lililoandikwa "Hatumpendi Eleanor" wakati anafanya utafiti wake katika makumbusho. "Wazo la kwamba alivuka mpaka lilitumiwa na chama chake mwenyewe," anasema.

Aidha, mke mwingine wa rais ni Betty Ford. "Watu walimpenda kwasababu aliwakilisha wazungu wa tabaka la kati ambao wengi wao walikuwa ni wake wa majumbani kulikochochewa zaidi na vyombo vya habari na msukumo wa utamaduni ambao ulitaka kubadilisha mambo."

Hata hivyo licha ya jinsi alivyokuwa, hakuogopa kupinga kile kilichoonekana kama kawaida, na kusisitiza kuwa watoto wa Wamarekani weusi waruhusiwe Ikulu katika hafla fulani wakati wa sikukuu ya Pasaka licha ya kwamba walikuwa hawaruhusiwi.

Betty alikuwa anapenda siasa, alitetea haki sawa na hakujali kuzungumzia masuala ambayo yalichukuliwa kuwa mwiko. Kuzungumzia wazi saratani ya matiti, kulihamasisha mamilioni ya wanawake kupimwa ugonjwa wa saratani na kunusuru maisha ya wengi.

Baada ya kuondoka Ikulu ya Marekani, alikuwa muwazi juu ya utegemezi wake wa dawa za kulevya na pombe baada ya kupata tatizo la navu na hiyo ndio iliyokuwa chanzo cha kuanzishwa kwa kituo cha urekebishaji tabia cha Betty Ford.

"Tunazungumzia uraibu na kupona kwa maana tofauti kabisa hii leo kwasababu alikuwa mstari wa mbele akizungumzia changamoto alizokumbana nazo maishani", anasema DuBois Shaw.

Hata hivyo anaona kuwa Bi. Ford alikuwa na ushawishi mkubwa duniani kwa jinsi alivyobalidisha maisha ya wengi.

Akiwa kwa kiasi fulani amemuiga Eleanor Roosevelt, Hillary Rodham Clinton alijipata akikosolewa na kiwango chake cha ushawishi na maono yake ya kisiasa.

Mrithi wake, Laura Bush alitambulika kama mkutubi wa shule na kuangazia zaidi miradi ya mtoto kujua kusoma na kuandika, alikubalika zaidi na wenye msimamo mkali.

Kwa Clinton, wakosoaji wake wanamchukulia kama mwenye kiburi lakini wanaompenda wanamchukulia kama mwanamke mwenye kujiamini.

Mwaka 2006 alizongwa na changamoto za Ikulu, akiwa ameandamwa na vita vya kungangania kuingia Ikulu miaka michache ijayo na ndio tu alikuwa amechaguliwa tena kuwa Seneta wa mji wa New York, kama mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo.

Licha ya kwamba pia naye ni mwanasheria kama Clinton, Michelle Obama hakuwa na nia kabisa ya kujiunga na siasa hatua iliyomfanya kuwa mama wa taifa maarufu sana.

Wakiwa na uelewa zaidi wa utamaduni na historia ya umuhimu wa kuwa rais na mke wa rais wote wakiwa weusi, Bwana Obama aliwahi kusifia mchoro wa mke wake kwa kunasa uwezo, uzuri, werevu na ucheshi wa mke wake ambaye pia amekuwa maarufu katika jumba la makumbusho.

Utawala wa Michelle Obama kama mke wa rais nao ulikuwa tofauti kabisa na Melania Trump ambaye atakumbukwa kwa mapambo yake mabaya ya mti wa Krismasi na upambaji wa bustani ya maua ya waridi kulikozua mijadala mikala kwenye mitandao ya kijamii.