Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wafahamu viongozi wa Afrika waliovunja rekodi za kuhudumu madarakani kwa muda mrefu zaidi
Huu ni ukweli unaozingatiwa mara nyingi zaidi barani Afrika.
Katika baadhi ya nchi za Afrika, mtu anaweza kuzaliwa, kukua, kutoka shule ya msingi hadi chuo kikuu, kufanya kazi kwa miaka 15 hadi 20 katika utumishi wa umma, na kumjua rais mmoja tu wa Jamhuri.
Hakika, baadhi ya wakuu wa nchi za Afrika wamekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 40. Aina hii ya uongozi haujaonekana mahali pengine.
Hii hapa orodha ya viongozi wa Afrika ambao wamevunja rekodi za kuhudumu kwa muda mrefu madarakani.
1- Teodoro Obiang Nguema Basogo, umri wa miaka 83, Guinea ya Ikweta
Kwa upande wa umri, yeye si mkuu wa nchi mwenye umri mkubwa zaidi barani Afrika. Lakini linapokuja suala la maisha marefu madarakani, bila shaka anavunja rekodi zote.
Teodoro Obiang Nguema Basogo, 83, ametawala Guinea ya Ikweta tangu 1979 na ametawala kwa miaka 46.
Katika taifa hili la Afrika ya Kati, Teodoro Obiang Nguema Basogo ana mamlaka yasio na upinzani.
Katika miaka ya hivi majuzi, alimteua mwanawe, Teodorin Nguema Obiang, kuwa makamu wa rais.
Anasalia katika nafasi hii licha ya shutuma na kutiwa hatiani nchini Ufaransa kwa ufujaji wa mali. Teodorin anaonekana kama anayependa zaidi kumrithi baba yake.
2- Paul Biya, miaka 92, Cameroon
Akiwa na umri wa miaka 92, Paul Biya ndiye mkuu wa nchi mwenye umri mkubwa zaidi barani Afrika. Ameketi katika kiti chake cha urais, ambacho ameshikilia tangu 1982, jumla ya miaka 43 kama rais.
Rais huyo mkongwe zaidi barani Afrika hatetereka licha ya mizozo mingi ya kisiasa na kiusalama ambayo imekuwa ikikumba utawala wake.
Mara kadhaa, mamlaka yake ilitikiswa na mpinzani wake wa zamani John Fru Ndi, (aliyefariki mwaka 2023) wa Social Democratic Front, Boko Haram na hasa uasi wa Anglophone unaodai kuundwa kwa taifa huru, lakini Biya bado anashikilia.
Huku uchaguzi ujao wa rais nchini Cameroon ukipangwa kufanyika Oktoba, Paul Biya ametangaza bado kugombea tena. Kambi yake ya kisiasa inatarajia atachaguliwa tena.
3- Denis Sassou Nguesso, umri wa miaka 82, Congo
Amekuwa madarakani kwa miaka 41 nchini Congo Brazzaville, ambayo imegawanywa katika sehemu mbili. Denis Sassou Nguesso alitawala Congo kwa miaka 13 kati ya 1979 na 1992, na tena kutoka 1997 hadi leo.
Utawala wake ulikatizwa kwa miaka mitano mwaka 1992 wakati wa uchaguzi wa rais ambapo alishika nafasi ya tatu kwa 16.9% ya kura nyuma ya wagombea wawili wakuu, Pascal Lissouba, rais mtarajiwa, na Bernard Kolélas, mpinzani wake katika duru ya pili.
Mwaka 1997, Denis Sassou Nguesso alirejea madarakani baada ya kumpindua Pascal Lissouba wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Ametawala Congo bila kuingiliwa tangu wakati huo, akikandamiza upinzani wote muhimu wa kisiasa.
4- Yoweri Museveni, umri wa miaka 81 - Uganda
Nchini Uganda, Yoweri Museveni amekuwa 'shujaa' wa mchezo wa kisiasa tangu 1986.
Kwa jumla, amekuwa Rais wa Jamhuri kwa miaka 39.
Museveni, mgombea anayetarajiwa kuchaguliwa tena katika uchaguzi ujao wa urais wa Uganda, ameondoa kikwazo cha kikatiba kilichoweka mipaka ya umri unaoruhusu kuhudumu katika wadhifa wa Rais wa Jamhuri hadi miaka 75.
Mnamo 2021, mwimbaji mchanga maarufu, Bobi Wine, alitikisa sana serikali yake, lakini bila kufanikiwa kuiangusha.
5. Isaiah Afewerki, umri wa miaka 79, Eritrea
Ikifafanuliwa kama "Korea Kaskazini ya Afrika" na Vanessa Tsehaye, mwanaharakati wa haki za binadamu wa Uswidi mwenye asili ya Eritrea, Eritrea imetawaliwa kwa mkono wa chuma na Isaias Afewerki tangu uhuru wake mwaka 1993.
Afewerki, ambaye aliongoza vita vya uhuru wa Eritrea kutoka kwa nchi jirani ya Ethiopia, alianzisha mfumo wa chama kimoja bila uchaguzi baada ya kuingia madarakani.
Kisha, kuanzia miaka ya 2000, baada ya vita vya pili dhidi ya Ethiopia (1998-2000), alianzisha utawala wa kiimla.
6- Paul Kagame, miaka 68 Rwanda
Kimya kimya, amekuwa madarakani nchini Rwanda kwa miaka 31, ikiwa ni pamoja na miaka 25 kama Rais wa Jamhuri.
Paul Kagame, 68, aliingia madarakani kama kamanda wa Rwandan Patriotic Front (RPF), vuguvugu la waasi linalopigana na utawala wa Wahutu.
Kagame alichukuliwa kuwa kiongozi mkuu wa nchi, akihudumu kama makamu wa rais na waziri wa ulinzi chini ya Rais Pasteur Bizimungu.
Ilikuwa mwaka wa 2000 ambapo alikuwa rais wa nne wa Rwanda.
Ingawa wengi wanathamini rekodi yake ya kiuchumi, wengine wanakosoa ukosefu wake wa uwazi wa kidemokrasia na uongozi wake .
7- Ismail Omar Guelleh, umri wa miaka 77 , Djibouti
Hatusikii mengi kumhusu, lakini Ismail Omar Guelleh, mwenye umri wa miaka 77, Rais wa Jamhuri ya Djibouti, amehudumu kwa muda ambao haupaswi kupuuzwa.
Baada ya kuingia madarakani mwezi Mei 8, 1999, kufuatia kuondolewa uongozini kwa Hassan Gouled Aptidon, amekuwa madarakani kwa miaka 26 mwaka huu.
Mnamo Aprili 9, 2021, Ismaïl Omar Guelleh alichaguliwa tena kuwa mkuu wa nchi katika duru ya kwanza kwa 98.58% ya kura.
Katika Pembe ya Afrika, Ismail Omar Guelleh anaonekana yuko kwenye nafasi nzuri ya kusalia madarakani.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla