Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Viongozi 6 walio madarakani na kuongoza muda mrefu zaidi duniani
Rais wa Equatorial Guinea, Teodoro Obiang Nguema kupitia chama chake cha PDGE, anarejea tena madarakani kufuatia uchaguzi mkuu wa Novemba 20, 2022, ukimpa mwanasiasa huyo nafasi ya kuendeleza miaka 43 ya utawala wake.
Wapo viongozi waliotawala miaka mingi lakini wamefariki, akiwemo Fidel Castro, aliyetawala Cuba kwa miaka 49, rais wa kwanza wa Taiwan, Chiang Kai-shek, alikuwa kiongozi wa kisiwa hicho kwa miaka 47 mpaka kifo chake mwaka 1975.
Muasisi wa Korea Kaskazini, Kim Il-sung alitawala kwa miaka 46 kabla ya kufariki akiwa madarakani mwaka 1994.
Wengine ni Enver Hoxha wa Albania aliyetawala miaka 40 mpaka anafariki mwaka 1985, Muammar Gaddafi wa Libya aliyefariki mwaka 2011, alitawlaa miaka 42, Omar Bongo Ondimba wa Gabon miaka 41 mpaka kifo chake mwaka 2009 na Robert Mugabe wa Zimbabwe ambaye alitawala kwa miaka 37 kuanzia mwaka 1980, kabla ya kuachia ngazi 2017 na baadaye kufariki dunia.
Ukiacha hao na wale viongozi wanaotawala kifalme kama utawala wa Malkia Elizabethi wa pili, hawa ndio viongozi walio hai na wako madarakani waliotawala kwa muda mrefu zaidi duniani.
6. Ali Hosseini Khamenei - Iran - 33
Ali Khamenei aliyezaliwa 19 April 1939, ni kiungozi wa juu wa pili na wa sasa wa Iran. Akiwa mamlakani tangu mwaka 1989, miaka 33 sasa.
Awali alihudumu kama rais wa tatu wa Iran kuanzia mwaka 1981-1989. Ukiacha kuwa wa tano wa muda mrefu kwa viongozi walio hai mamlakani sasa, Khamenei ndiye kiongozi wa taifa aliyetawala kwa muda mrefu katika nchi za mashariki ya kati. Huku akiwa kiongozi wa pili wa Iran kutawala muda mrefu zaidi katika muongo mmoja uliopita, nyuma ya Shah Mohammad Reza Pahlavi.Mfumo wa serikali ya Iran unakuwa na kiongozi mkuu, halaf chini yake kuna Rais, ambaye kwa sasa ni Ebrahim Raisi aliyechukua mikoba mwaka 2021 kutoka kwa Hassan Rouhani aliyetawala kwa miaka 8.
5. Yoweri Museveni- Uganda -32
Yoweri Kaguta Museveni, aliyezaliwa mwaka 1944, huko wilayani Mbarra, Uganda), amekuwa rais wa Uganda tangu mwaka 1986.
Alianza harakati za kuingia madarakani akiwa uhamishoni nchini Tanzania mwaka 1971 kwa kuanzisha kundi lake la FRONASA, kuanzisha vuguvugu la kumuondoa rais aliyekuwa madarakani waketu huo, Idd Amini.
Aliongoza mapambano ya miaka karibu 5, inaelezwa akianza na bunduki 27. Alishakuwa waziri wa Ulinzi na kiongozi mkuu katika Jeshi la Uganda.
Ni miongoni mwa marais wachache Afrika waliokaa madarakani kwa miaka zaidi ya 30. Pengine robo tatu ya wananchi wake, wamemshuhudia rais mmoja tu wa taifa hilo.
4. Hun Sen – Cambodia -33
Hun Sen aliyezaliwa mwaka 1952 ni Waziri mkuu wa sasa wa Cambodia na kiongozi aliyetawala muda mrefu zaidi taifa hilo tangu akingie madarakani mwaka 1985. Ni mmoja wa viongozi waliokaa madarakani muda mrefu zaidi, akiwa pia rais wa chama cha CPP na mbunge wa Kandal.
Mfumo wa utawala wa Cambodia unaongozwa kifalme, huku Waziri mkuu akiwa ndiye kiongozi mkuu wa masuala yote ya serikali na uendeshaji wake.
Mwaka 2014, zilipozagaa sana taarifa za afya yake kudorora, alijitokeza na kusema hana matatizo ya kiafya n ani yeye tu anayeweza kuongoza taifla hilo na kulidhibiti jeshi, bilas yeye taifa hilo lingedidimia.
2. Denis Sassou-Nguesso – Congo - 35
Sassou-Nguesso alijiunga jeshi mwaka 1960 na hapa ukawa kama mwanzo wa kuelekea kutawala nchi hiyo. Baadae mwaka 1969 akaunda chama cha Congolese Labor akiwa na Marien Ngouabi. Mwaka huo huo kukatoea mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani rais Massemaba Debat na kumuingiza Ngouabi kama rais.
Mwaka 1973, Sassou-Nguesso, alifanywa Waziri wa Ulinzi akiwa na umri mdogo wa miaka 32.
Machi 18, 1977 Ngouabi aliuawa, na jeshi likashika hatamu. Bada ya majadiliano ya ndani Sassou-Nguesso akateuliwa kuwa rais Februari 8, 1979, akatawala vipindi vitatu tofauti na kufikisha miaka 35 ya kutawala Congo.
2. Paul Biya – Cameroon - 40
Paul Biya amekuwa rais wa Cameroon tangu Novemba 6, 1982 akichukua nafasi ya Ahmadou AHIDJO aliyejiuzulu. Ndiye rais anayeshika nafasi ya pili kwa kutawala kwa muda mrefu zaidi Afrika na kongozi aliye madarakani mwenye umri mrefu zaidi duniani, ana miaka 89 sasa akihudumu madarakani kwa miaka 40.
Alinusurika kupinduliwa kijeshi mwaka 1984, huku mwaka 1992 almanusura aangushwe kwenye uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi akimpiku mpinzani wake kwa tofauti ya 4% ya kura.
Teodoro Obiang Nguema Mbasogo – Equatoria Guinea - 43
Obiang Nguema aliyechukua madaraka kutoka kwa mjomba wake mwaka 1979, ndiye kiongozi aliye hai aliyetawala miaka mingi zaidi duniani. Amekuwa akishinda uchaguzi kwa kishindo cha mpaka asilimia 90% kila uchaguzi.
Pengine asilimia 80% ya wananchi wa Equatoria Guinea wamekuwa wakimfahamu yeye tu ama wameshuhudia utawala wake tu kama rais, hawajawahi kumshuhudia raia mwingine.
Katika uchaguzi wa sasa kama ilivyotarajiwa wapinzani wawili Buenaventura Monsuy Asumu, aliyechuana nae katika chaguzi tano zilizopita na Andrés Esono Ondo, anayewania kwa mara ya kwanza, wameshindwa kumzuia mwanasiasa huyo kurejea madarakani.
Zaidi ya watu 400,000 walijiandikisha kupiga kura katika taifa hilo dogo lenye watu 1.5 million.