Zijue nchi zinazoagiza umeme kwa wingi kutoka nje na sababu za kufanya hivyo

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Rashid Abdallah
- Nafasi, BBC Swahili
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Swali ambalo wengi hujiuliza, kwa nini nchi hulazimika kuagiza umeme kutoka nchi nyingine wakati nchi zote zina vyanzo vyao vya kuzalisha umeme? Swali hili linazidi kuwa la msingi pale data zinapoonesha kuwa nchi nyingi zinazoagiza umeme kwa wingi kutoka nchi nyingine ni zile nchi tajiri.
Nchini Tanzania, mjadala umeibuka baada ya tangazo la serikali ya nchi hiyo kueleza kuwa inajiandaa kununua umeme kutoka Ethiopia kupitia Kenya kwa ajili ya eneo la Kaskazini. Wakati huo huo, taarifa rasmi za serikali zinaonyesha kuwa nchi hiyo inazalisha umeme mwingi zaidi ya unaohitajika.
Sababu iliyotolewa na serikali ya kuamua kununua umeme kutoka nje, ni kupunguza gharama ya upotevu wa umeme wakati wa kuusafirisha kutoka vyanzo vilivyo Kusini mwa Tanzania na kuupeleka katika maeneo ya Kaskazini mwa nchi hiyo. Lakini zipo sababu nyingine za nchi kununua umeme kutoka nchi nyingine:
Kwanini nchi huagiza umeme?

Chanzo cha picha, Getty Images
Nchi huagiza umeme kutoka nje kwa sababu ya unafuu wa bei. Ni kweli kwamba wakati mwingine kuagiza umeme kutoka nje kunaweza kuwa nafuu zaidi kuliko kuuzalisha ndani ya nchi, hasa ikiwa nchi inatumia gharama kubwa za kuzalisha umeme, mfano ikiwa inategemea nishati ghali ya mafuta.
Sababu nyingine ni kuwa na umeme wenye kuaminika zaidi kwa kuwa na vyanzo mbalimbali vya nishati hiyo, hilo husaidia kupunguza utegemezi wa chanzo kimoja cha nishati au teknolojia moja.
Vilevile, kusawazisha uzalishaji wa nishati inayobadilika badilika. Nchi zilizo na nishati ya upepo au jua zinaweza kuagiza umeme ili kusawazisha muda wa vyanzo hivi vinaposhindwa kuzalisha umeme vizuri, mfano wakati wa kukosekana kwa jua kali au upepo kutovuma.
Pia kwa baadhi ya nchi zinaweza kuagiza umeme kutoka maeneo yenye rasilimali nyingi za nishati mbadala, na hivyo kusaidia kuharakisha kuelekea mfumo wa nishati safi na kuachana na nishati ambayo huharibu mazingira.
Kuunganisha gridi kwenye mipaka kunaweza kuufanya mfumo wa nishati kuwa na ufanisi zaidi na kuwa wa gharama nafuu, ushirikiano huu katika uwekezaji wa miundombinu ya nishati unaweza kupunguza gharama na kujenga ushirikiano.
Nchi zinazoagiza umeme kwa wingi

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa mujibu wa Observatory of Economic Complexity (OEC), jukwaa linalotoa data juu ya biashara za kimataifa, limeyaweka mataifa matano ambayo yote ni kutoka bara la Ulaya katika tano bora ya mataifa yaliyoongoza kwa kuagiza umeme kutoka nje kwa mwaka 2023.
Ujerumani: Mwaka 2023, Ujerumani iliagiza kutoka nje asilimia 9.95 ya umeme wake, kwa gharama ya dola za kimarekani bilioni 7.52. Sehemu kubwa ya umeme wa Ujerumani hutoka Ufaransa, Austria, Uholanzi, Switzerland na Denmark.
Kulikuwa na ongezeko la uagizaji wa umeme katika mwezi Aprili, Mei, na Juni 2023, kulitokana na kuzimwa kwa vinu vitatu vya mwisho vya nyuklia nchini Ujerumani Aprili 2023, huku umeme ulioagizwa kutoka nje ukitumiwa kufidia umeme uliokuwa ukizalishwa kwa nishati ya nyuklia hapo awali.
Italy: Mwaka 2023, Italy iliagiza umeme wenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 7.21, na kuifanya kuwa muagizaji wa pili kwa ukubwa duniani. Umeme ulikuwa bidhaa ya 9 iliyoagizwa zaidi nchini Italy 2023.
Katika mwaka huo, uagizaji wa umeme wa Italy ulifikia asilimia 9.53 ya umeme wake ujumla. Umeme ulioagizwa ni kutoka Switzerland, Ufaransa, Montenegro, Slovenia na Ugiriki.
Switzerland: Ni nchi nyingine inayojulikana kwa uagizaji wake wa umeme kutoka nje. Mwaka 2023, iliagiza takribani asilimia 5.57 ya umeme wake kwa gharama ya dola za kimarekani bilioni 4.21, huku vyanzo vikuu vya umeme huo ni kutoka Ufaransa, Ujerumani, Austria, na Italy.
Huku uzalishaji wake wa umeme ukionekana kuendana kwa karibu na mahitaji ya ukuaji wa uchumi na idadi ya watu na mabadiliko ya muundo wa uchumi - uzalishaji wa ndani wa umeme wa Switzerland unatokana na nguvu ya maji (56%) na nishati ya nyuklia (33%).
Uingereza: Uingereza ni mwagizaji pia wa nishati ya umeme kutoka nje, ikiwa imeagiza asilimia 5.12 ya umeme wake kwa gharama ya dola bilioni 3.87 mwaka 2023.
Hadi 2023, gesi iliendelea kuchukua sehemu kubwa ya uzalishaji wa umeme kote Uingereza, ikiwa ni kwa asilimia 32 ikifuatiwa na upepeo 29.4 na nyuklia ambayo ni asilimia 14.2, na vyanzo vingine.
Hungary: Asilimia 4.46 ya umeme wa Hungary ulinunuliwa kutoka nje mwaka 2023, gharama ilikuwa ni dola za kimarekani bilioni 3.37.
Hungary inazalisha umeme wake kwa kutegemea nishati ya nyuklia ambayo inachukua 44.8% ya jumla, kutoka katika kiwanda chake pekee cha nyuklia cha Paks. Maeneo mengine yana ya chanzo cha umeme kwa nchi hiyo ni gesi asilia (20.5%) na jua (19.6%).
Licha ya nchi kadhaa kuagiza umeme kutoka nje katika mataifa ya Afrika, lakini sehemu kubwa ya nchi zinazoagiza umeme mwingi kutoka nchi nyingine ni kutoka Mataifa ya Ulaya.















