Kwanini baadhi ya nchi Afrika zinakabiliwa na uhaba wa umeme?

k

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Nchi kadhaa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara zinakabiliwa na tatizo la nishati kwa miezi kadhaa.
    • Author, Ladislas Didier Lando
    • Nafasi, BBC

Chad, Guinea, Niger, Mali, na nchi nyingine nyingi za Afŕika Kusini mwa Jangwa la Sahaŕa zimekuwa zikikabiliwa na uhaba wa nishati kwa miezi kadhaa.

Kulingana na ripoti ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati (IEA) iliyochapishwa Juni 2023, watu milioni 567, Afŕika Kusini mwa Jangwa la Sahaŕa hawakupata umeme mwaka 2021, ikiwa ni zaidi ya asilimia 80 ya watu wote duniani ambao hawakupata umeme.

Jumatatu, Mei 6, wananchi wa Chad watapiga kura kumchagua kiongozi wao kwa miaka 5 ijayo. Wakati kampeni zikipamba moto, nchi hiyo inakabiliwa na tatizo la nishati ya umeme ambalo halijawahi kushuhudiwa.

Pia unaweza kusoma

Hali nchini Chad

SD

Chanzo cha picha, AFP

Katika baadhi ya vitongoji vya mji mkuu wa Chad, N'djamena, wakaazi walikaa kwa zaidi ya miezi 2 bila umeme, katika mazingira ya joto kali ambapo halijoto ilikuwa karibu 45°.

Suala hilo lipo katika ajenga za kampeni. Rais wa mpito na mgombea urais, kwa mfano, aliahidi umeme wa masaa 24, siku saba kwa wiki kwa kila mtu wa Chad.

Ahadi kama hiyo ilitolewa pia na Succès Masra, Waziri Mkuu na mpinzani wake mkuu. "Nilipokuwa serikalini, niligundua asilimia 90 ya wananchi wa Chad hawajawahi kuona umeme tangu uhuru. Nikichaguliwa kuwa rais, nitakomesha miaka 60 ya giza,” alisema Rais wa chama cha Les Transformateurs.

Chad ambayo ina sera ya maji na umeme bila malipo kwa matumizi yasiyozidi kiwango cha kila mwezi cha kWh 300 kwa umeme na mita za ujazo 15 za maji, haijaeleza haswa juu ya sababu za shida ya umeme.

Lakini kulingana na Taasisi ya Thinking Africa, mzozo wa nishati nchini Chad ni matokeo ya usimamizi mbovu wa kiufundi na kibiashara, na kusababisha tatizo kubwa la umeme.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ingawa nchi hiyo ina uwezo mkubwa wa nishati kama vile jua, majani, upepo, jotoardhi na hidrokaboni, vyanzo ambavyo vinaweza kuchangia maendeleo ya sekta hiyo.

"Wagombea hutoa ahadi nyingi kuhusu upatikanaji wa umeme. Lakini watu hawaamini. Wananchi wa Chad wanashughulika kutafuta njia za kukabiliana na ukosefu wa nishati. Kwa hiyo hawachukulii ahadi za kisiasa kwa uzito,” ameripoti Maji Maji Odjitan, mwandishi wa BBC huko Ndjamena.

Wananchi wa Chad hutafuta njia mbadala kukabiliana na joto, ikiwa ni pamoja na kwenda katika bustani za Seminari ya Bakara, takribani kilomita kumi na tano kutoka katikati mwa N'djamena, kupata hewa na upepo wa mahali hapo.

Akiwa ameketi kwenye benchi kwenye kivuli cha mti, Maryse anasema "kuwa na umeme Ndjamena imekuwa kama muujiza".

"Ilinibidi ninunue sola tatu za umeme wa jua, angalau kuwa na mwanga ndani ya nyumba yangu. Lakini umeme huo hautoshi kuwasha hata feni, seuze kiyoyozi. Usiku, hutumia muda mwingi kuwapepea watoto ili walale vizuri. Hali ni ngumu sana,” anasema Manga Bosco.

Wamiliki wa jenereta, kwa upande wao, wanakabiliwa na gharama kubwa ya mafuta. Petroli iliongezeka kutoka faranga 518 hadi 730 kwa lita, ongezeko la 40%, na dizeli iliongezwa hadi faranga 828 badala ya faranga 700, ongezeko la 18%.

Katika taarifa rasmi kwa vyombo vya habari kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, imeeleza ongezeko hili la bei ya mafuta limetokana na ukweli kwamba uzalishaji katika kiwanda cha kusafisha mafuta ni mdogo.

Guinea yaigeukia Senegal

SDX

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Nchini Guinea, mlipuko katika ghala kuu la mafuta nchini humo mwezi Desemba 2023 ulisababisha mkwamo wa uzalishaji wa umeme huko Coronthie.

Nchini Guinea, mlipuko katika ghala kuu la mafuta nchini humo mwezi Desemba 2023 ulisababisha kutatizika uzalishaji wa umeme huko Coronthie.

Tangu wakati huo, nchi hiyo imepata shida ya nishati na kusababisha kukatwa kwa umeme mara kwa mara. Siku ya Alhamisi Machi 14, 2024, kukatika kwa umeme kuliliingiza jiji kuu gizani na kusababisha ghasia katika vitongoji vingi.

Zaidi ya hayo kuna upungufu wa maji unaoathiri mabwawa ya kuzalisha umeme na kujiondoa kampuni ya kuzalisha umeme ya Uturuki ya Karpowership ambayo ilitoa asilimia 10 ya mahitaji ya jumla ya umeme nchini Guinea tangu Desemba 2019.

Katika kukabiliana na maandamano ya kupinga kukatwa kwa umeme, mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Electricité de Guinée (EDG) na manaibu wake wawili waliondolewa na mkuu wa junta, Jenerali Mamadi Doumbouya.

Zaidi ya mwezi mmoja baada ya tukio hili, Guinea iliamua kurudi kwa majirani zake, ikianza na Senegal, ili kupata tena umeme kutoka Senegal.

"Tangu Aprili 25, 2024, njia ya kuhamisha umeme wa megawati 120 kutoka Senegal (SENELEC) hadi Société Électrcité de Guinée (EDG) imefunguliwa," ilitangaza Wizara ya Nishati, katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyochapishwa Jumanne hii, Aprili 30, 2024.

Wizara inasema wanaendelea na majadiliano na nchi nyingine katika kanda hiyo ili kutafuta suluhu mbadala kwa hali ya sasa ya nishati.

Hali ilivyo Niger

SDX

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Niger inakabiliwa na changamoto katika usambazaji wa umeme.

Kurejeshwa kwa laini ya umeme ya Nigeria nchini Niger, hakujabadilisha chochote. Nigeria, kupitia Bwawa la Kainji, ndiyo msambazaji mkuu wa umeme wa Niger.

Kufuatia mapinduzi ya Julai 26, 2023, Nigeria ilikata umeme kwenda Niger. Lakini hivi sasa, laini hiyo imerejeshwa.

"Laini ya Nigeria imerejeshwa lakini hali ya sasa ni mbaya zaidi kuliko ile tuliyopitia wakati laini ilipozimwa. Kwa zaidi ya miezi 3, Niger imekuwa ikikabiliwa na kukatika kwa umeme. Katika baadhi ya maeneo, umeme unapatikana kwa saa 4 hadi 5 tu kwa siku. Siku za joto kali, mahitaji ya nishati ya umeme yanaongezeka.

Mikoa yote 8 ya nchi imeathiriwa. Lakini mikoa ya Dosso, Tillabery na Niamey ndiyo iliyoathiriwa zaidi,” anaripoti Mariama Soumana, mwandishi wa BBC nchini Niger.

“Tuna matatizo makubwa sana ya upatikanaji wa umeme katika kipindi hiki cha joto kali. Ni kweli hakuna maandamano mitaani kupinga kukatika kwa umeme. Lakini watumiaji wanalalamika sana, hasa kwenye mitandao ya kijamii,” anasema Mahaman Nouri, rais wa Chama cha Kutetea Haki za Watumiaji wa Umeme, (ADDC) cha Niger.

Zaidi ya hali ya kutokuwepo kwa umeme, pia kuna ukosefu wa taarifa kuhusu kukatika huko.

“Haki ya mtumiaji kupata taarifa inakiukwa. Tunataka taarifa za wazi ili kuruhusu watumiaji kujitengenezea mipangilio yao wenyewe na kujipanga vyema. Ni lazima wawafahamishe wateja,” anasisitiza Mahaman Nouri.

Ili kupunguza tatizo la nishati, kampuni ya umeme ya Nigerien (Nigelec) hivi majuzi ilizindua mtambo wa megawati 30 (MW). Lakini mtambo unahitaji matumizi makubwa ya dizeli.

Lakini pamoja na matatizo hayo yote, Niger inapanga kusaidia nchi jirani ya Mali ambayo pia iko katika hali mbaya.

Niger kuisaidia Mali

W

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Kampuni ya Mafuta ya SONIDEP, itasambaza lita milioni 150 za dizeli.

Kampuni ya Mafuta ya Nigerien (SONIDEP) itasambaza lita milioni 150 za dizeli. Hiki ndicho tunachoweza kukumbuka katika taarifa ya rais wa Mali, Kanali Assimi GOÏTA ya Aprili 16 kufuatia ujumbe kutoka Niger ukiongozwa na Waziri wake wa Mafuta, Mahaman Moustapha Barke.

Mafuta haya yatatumika kuwezesha vituo vya umeme Mali, ili kuimarisha usambazaji wa umeme na kupunguza kwa kiasi fulani kukatika kwa umeme.

"Mali ni ndugu na nchi rafiki. Mwaka jana, kulikuwa na awamu ya kwanza iliyohusisha lita milioni 22. Tunafanya kazi pamoja kuwezesha usambazaji wa lita hizi milioni 150 za dizeli nchini Mali haraka iwezekanavyo,” alitangaza Mahaman Moustapha Barke.

Nchini Mali, kukatwa kwa umeme kunaweza kudumu hadi saa 18 kwa siku. Tatizo hilo linaelezwa, kwa upande mmoja ni uchakavu wa mitambo na kwa upande mwingine na ugumu katika kufadhili ununuzi wa mafuta ya kuendesha mitambo ya uzalishaji wa nishati ya umeme.

Hivi karibuni, Bintou Camara, Waziri wa Nishati na Maji wa Mali, alitangaza nchi hiyo itaunda ushirikiano mpya ambao utairuhusu kuwa na miundo minu iliyoboreshwa na kufadhili ununuzi wa mafuta ya kusambaza mitambo ya kuzalisha nishati ya umeme.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la kitaifa la umeme alitangaza, ili kukidhi mahitaji ya umeme kwa mwaka wa 2024, inahitaji lita milioni 500 za mafuta.

Kampuni hiyo, ambayo inateseka chini ya deni la zaidi ya bilioni 200 za FCFA (euro milioni 300), inazidi kupata ugumu wa kuhakikisha upatikanaji wa umeme katika mji mkuu na maeneo mengine nchini humo.

Ghana haina pesa za kutosha

J

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Ghana haina pesa za kutosha kununua mafuta.

Nchini Ghana, sekta zote za zinaathiriwa na kukatika kwa umeme. Kulingana na Wakala wa Kimataifa wa Nishati (IEA), 63% ya umeme wa Ghana unatokana na gesi asilia.

Lakini nchi imekuwa tegemezi zaidi kwa mafuta, kwa sasa haina uzalishaji wa kutosha wa gesi asilia ili kusambaza katika vituo vyake vya umeme na hivyo lazima iagize kutoka nje ya nchi.

Ugumu wa kufadhili ununuzi wa mafuta pamoja na matengenezo ya miundombinu duni ya umeme umeitumbukiza nchi hiyo, ambayo inalenga kufikia 10% ya uzalishaji wa umeme kutoka nishati mbadala ifikapo 2030, kwenye shida kubwa ya umeme.

"Fedha zinazohitajika kwa ajili ya ununuaji wa mafuta mara kwa mara hazijapatikana na kwa hivyo hatujaweza kuwasha jenereta ambazo zinahitaji mafuta," anaelezea Benjamin Boakye, mchambuzi katika Kituo cha Africa Center for Energy Policy.

Ghana ina uzalishaji wa umeme ambao haukidhi mahitaji yanayoongezeka kila mara. Vilevile, wizi na uuganishaji haramu husababisha hasara ambayo inaweza kufikia wastani wa 25% ya uzalishaji wa umeme.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah