Je, Morocco inaweza kuwa suluhu ya mzozo wa nishati ya umeme barani Ulaya?
Na Jonathan Josephs, BBC News, Rabat

Chanzo cha picha, Getty Images
Morocco ina matarajio makubwa ya kusafirisha umeme unaozalishwa kwa njia ya jua na upepo kwenda Ulaya, lakini je, inapaswa kuweka kipaumbele nishati hiyo mbadala kwa soko lake la nyumbani?
"Rasilimali tulizo nazo hapa zinaweza kuwa mojawapo ya majibu makubwa kwa mahitaji ya umeme Ulaya," anasema mjasiriamali wa nishati wa Morocco Moundir Zniber.
Bw Zniber ni mtu mwenye shauku ambaye anaona fursa badala ya matatizo.
"Nadhani Morocco inawakilisha fursa nzuri zaidi ya kuliondoa bara la Ulaya kutoka kwa utegemezi ulio nao leo kwa gesi ya Urusi," anasema.
Bw Zniber ametumia miaka 15 iliyopita kuimarisha kampuni yake inayoitwa Gaia Energy, na kuwa moja ya makampuni yaliyoleta mapinduzi ya nishati mbadala katika nchi yake.
"Morocco ina moja ya rasilimali bora zaidi za jua na upepo duniani zikiunganishwa," anasema. "Hatuna mafuta, hatuna gesi asilia, lakini tuna uwezo ambao ni wa kushangaza tu."
Vita nchini Ukraine vimewachochea wanasiasa wa Ulaya kuongeza juhudi zao za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa kwa kutaka kutumia vyanzo vipya vya nishati safi. Morocco inatarajia kuwa sehemu ya suluhisho.
Iko jirani ama mlangoni mwa Ulaya, na ina mipango kabambe ya kuzalisha 52% ya umeme wake kutoka kwa vyanzo mbadala ifikapo 2030. Matumaini ni kwamba umeme huu mwingi utasafirishwa kupitia nyaya za chini ya bahari hadi Ulaya.
Lakini kwa sasa, nchi hiyo bado inapaswa kujenga miundo mbinu mingi zaidi ya jua na upepo. Hivi sasa taifa hilo la kaskazini mwa Afrika lenye watu milioni 39 linategemea uagizaji wa bidhaa kutoka nje kwa asilimia 90 ya mahitaji yake ya nishati, na bidhaa nyingi zaidi ni nishati ya mafuta.
Mwaka 2021, takriban asilimia 80.5% ya uzalishaji wa umeme nchini Morocco ulitokana na makaa ya mawe, gesi na mafuta. Lakini ni asilimia 12.4% tu ilitoka kwa nishati ya upepo, na 4.4% ilitoka kwa jua.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hata hivyo, Morocco tayari inapiga hatua inayoonekana kwenye sekta hii ili kuongeza uzalishaji wake wa nishati mbadala, kutokana na miradi kama vile Noor-Ouarzazate Solar Complex. Huku awamu ya kwanza ikifunguliwa mwaka wa 2016, hiki ndicho kiwanda kikubwa zaidi cha nishati ya jua duniani.
Kuna vioo vya jua vilivyoenea zaidi ya hekta 3,000 (maili za mraba 11.6). Kituo hicho kilitengenezwa na kampuni ya Saudi Arabia ya ACWA Power, kwa ufadhili pia kutoka Benki ya Dunia na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya.
Bw Zniber anasema kuwa makampuni binafsi ya Morocco kama yake sasa yanapanga kusafirisha umeme wa jua na upepo kwenda Ulaya.
Anaongeza kuwa Gaia Energy inatengeneza mifumo ya upepo na jua ambayo inaweza kukidhi hadi 4% ya mahitaji ya umeme ya nchi ya Ujerumani na Italia. "Na kwa upande wa hidrojeni ya kijani tuna miradi sita ambayo kampuni yetu inaendeleza ambayo inaweza kukidhi asilimia 25% ya mahitaji ya EU."
Wakati huo huo, kampuni ya nishati ya Uingereza ya Xlinks ina mipango ya kuunganisha waya za umeme umeme kupitia chini ya bahari kutoka Morocco hadi Uingereza. Matumaini yake ni kwamba nishati ya jua na upepo ya Morocco inaweza kukidhi asilimia 8% ya mahitaji ya umeme ya Uingereza kufikia mwaka 2030.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kuongezeka kwa ukubwa wa uzalishaji wa nishati ya jua na upepo nchini Morocco kunaweza kusaidia kuimarisha ukuaji wa uchumi nchini humo, kwa mujibu wa Benki ya Dunia. Imetoa mamilioni ya dola za ufadhili kwa sekta hizo.
Manufaa hayo ni pamoja na kutoathirika na "kuyumba sana kwa bei za mafuta", kulingana na mwanauchumi mkuu wa Benki ya Dunia katika eneo hilo, Moez Cherif.
Katika nchi iliyo na kiwango cha ukosefu wa ajira cha 11.2%, Bw Cherif anaongeza kuwa inaweza kutengeneza ajira mpya 28,000 zinazohitajika kila mwaka.
Pia anasema itairuhusu Morocco "kujiweka kama kitovu cha viwanda kwa uwekezaji wa mauzo ya nje ya bidhaa za viwandani" kama vile utengenezaji wa magari kwa kutumia nishati mbadala.
Hata hivyo Benki ya Dunia inakadiria kuwa itagharimu $52bn (£41.6bn) kwa Morocco kufikia lengo lake la uzalishaji wa nishati mbadala kufikia mwaka 2030, huku pesa nyingi zikitoka kwenye sekta ya binafsi. Serikali ya Morocco inakubaliana na hilo.
Utawala unafahamu vyema manufaa yanayoweza kutokea, na unajaribu kuharakisha maono yanayoweza ya nishati mbadala yaliyowekwa kwa mara ya kwanza na Mfalme Mohammed VI mnamo mwaka 2009.
Waziri wa Mpito wa Nishati na Maendeleo Endelevu wa Morocco Leila Benali anasema ukuaji wa polepole wa sekta ya nishati mbadala nchini humo katika miaka ya hivi karibuni umesababishwa na sababu mbalimbali.

"Ulimwengu umetoka kwenye janga la kihistoria (Covid-19), kuvurugwa kwa minyororo ya usambazaji na minyororo ya thamani - pia inaathiri nishati mbadala, pamoja na jinsi tunavyofanya biashara ya paneli za jua na turbine za upepo."
Walakini, anakubali pia kuna vizuizi vya ndani vya kukabiliana.
Hizo ni pamoja na "kuharakisha na kuondoa urasimu", ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kampuni zinapata vitu kama vile "vibali vya ardhi kwa haraka ili kuhakikisha kuwa wawekezaji wanapata fursa wanazotaka".
Bibi Benali anaongeza kuwa mkakati wa serikali wa nishati umejikita katika nguzo tatu za kukusanya nishati mbadala, kuongeza ufanisi, na ushirikiano zaidi katika masoko ya kimataifa ya nishati.
Alipoulizwa kama ina mantiki ya kuuza nje umeme kabla ya kukidhi mahitaji yote ya Morocco kufipitia njia mbadala, Bibi Benali anasema kwamba "kipaumbele" ni kwa Wamorocco kupata nishati hiyo "ya gharama ya chini".
Anaongeza kuwa kuna haja pia ya kuchukua "fursa ya kihistoria" kuunganishwa na soko la nishati la Ulaya, na kwamba fursa kama hizo zinaweza kuwa motisha kwa uwekezaji binafsi unaohitajika sana.
Moez Cherif wa Benki ya Dunia anaamini kwamba Morocco inapaswa kuongeza mauzo ya nje ya nishati mbadala, na kuongeza zaidi matumizi ya ndani. "Kwa kweli unapaswa kufanya yote mawili," anasema.












