Stinger: Kombora la Marekani la ulinzi wa anga linalotungua droni na helikopta

er

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 4

Utawala wa Rais wa Marekani, Donald Trump umeidhinisha upelekaji wa makombora 600 ya ulinzi wa anga aina ya Stinger na vifaa vya kurushia makombora hayo nchini Morocco, kwa mkataba wa thamani ya dola milioni 825.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imeidhinisha mpango huu na inasubiri idhini ya mwisho kutoka Congress ili kuanza kupeleka makombora hayo nchini Morocco.

Shirika la Ushirikiano katika masuala ya Usalama na Ulinzi la Marekani, sehemu ya Idara ya Ulinzi ya Marekani, limesema katika taarifa yake kuhusu mpango huo, silaha hizi zitaisaidia Morocco kuboresha uwezo wake na "kupanua uwezo wake wa ulinzi wa anga katika masafa mafupi."

Taarifa hiyo imeeleza, hilo litaipa Rabat uwezo wa kukabiliana na "vitisho vya sasa na baadaye," hasa kwa vile mfumo huo unajulikana kwa ufanisi wake katika kulenga ndege zisizo na rubani, helikopta na ndege zinazoruka chini.

Mbali na kuimarisha uhusiano kati ya vikosi vya jeshi la Morocco na wenzao wa Marekani na washirika; kwa jeshi la Morocco ambalo linategemea silaha za Marekani, mpango huo unawakilisha muendelezo wa uhusiano bora kati ya Marekani na Morocco, kufuatia Washington kuitambua upya mamlaka ya Morocco juu ya Sahara Magharibi.

Pia unaweza kusoma

Makombora ya Stinger

d

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Toleo lililoboreshwa la kombora la Stinger katika Maonyesho ya Ujerumani 2024.

Jeshi la Morocco limeomba makombora 600 ya FIM-92K Stinger Block I, pamoja na usaidizi wa kiufundi, vifaa na uhandisi kutoka serikali ya Marekani na wakandarasi, pamoja na usaidizi mwingine wa vifaa na programu za kisasa za ulinzi.

Makombora haya ni toleo la karibuni zaidi la mfumo wa Stinger. Makombora ambayo hurushwa kutokea begani. Ni kombora la masafa mafupi, kutokea ardhini hadi angani ili kutoa ulinzi wa angani dhidi ya ndege, helikopta na droni.

Hatua za kwanza za uzalishaji wake ilianza katika miaka ya 1960 na kampuni ya Marekani ya General Dynamics, na mwaka 1972 hatua mbalimbali za uboreshaji zilianza. Kombora hilo lilianza kuzalishwa huko Raytheon mwaka 1978 na liliingia katika Jeshi la Marekani mwaka 1981. Linatumiwa na majeshi ya Marekani na nchi zingine 29.

Kombora la Stinger lina urefu wa mita 1.52. Kombora lenyewe lina uzito wa kilo 10.1. Lakini kombora hilo na mfumo wake wa kulirusha kwa pamoja ya uzito wa takriban kilo 15.2.

Masafa yake ni kilomita tano na linaweza kuinuka hadi mita 4,800, na wanajeshi wanaweza kufyatua kombora hilo kutoka popote, ikiwa ni katika magari ya vita na helikopta ikiwa angani. Linatembea na kufikia kasi ya juu ya mita 750 kwa sekunde.

Stinger nchini Ukraine

f

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mwanajeshi wa Ukraine akifanya mazoezi ya kutumia kombora la Stinger huko Ukraine mwaka 2024.

Makombora haya yanafanya kazi kubwa katika vita kati ya Urusi na Ukraine. Ukraine iliyatumia sana kukabiliana na mashambulizi ya anga ya Urusi, haswa kutoka kwa helikopta na ndege zisizo na rubani.

Hii ilisababisha nchi za Ulaya, pamoja na Ujerumani, Uholanzi, na Italia, kuagiza shehena kubwa ya makombora haya mwaka 2023, katika makubaliano yenye thamani ya dola za kimarekani milioni 780.

Machi 12, 2024, Marekani ilitangaza nyongeza ya msaada wa dola milioni 300 kwa Ukraine, ikiwa ni pamoja na silaha zinazohitajika haraka, yakiwemo makombora ya ulinzi wa anga ya Stinger.

Makombora hayo kwa Ukraine yaliboreshwa, ili kuyawezesha kudumisha mwelekeo na uthabiti hata wakati wa kukata kona. Na hilo huboresha uwezo wa kupiga shabaha zinazotembea kwa kasi.

The Stinger ni kombora la ulinzi wa anga linaloweza kubebwa na binadamu, linalowapa wanajeshi ulinzi dhidi ya vitisho vinavyotokea angani.