Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tetesi kubwa 5 za soka jioni hii: 'Man Utd inahitaji kusajili wapya watano'
Mchambuzi na beki nguli wa zamani wa Manchester United, Gary Neville anasema klabu hiyo inahitaji kusajili wachezaji watano ili kuendana na mfumo wa kocha Ruben Amorim.
Manchester United iko katika nafasi ya 13 kwenye ligi kuu England baada ya kutoka sare ya 0-0 nyumbani na Manchester City Jumapili, wakiwa wameshinda michezo miwili pekee kati ya minane iliyopita ya ligi.
Kocha wa Manchester United, Ruben Amorim anajaribu kucheza mfumo wa anaoupendelea zaidi wa 3-4-3; Patrick Dorgu alikuwa usajili wake mkuu wa kwanza kwa mkataba wa £30m kutoka Lecce wakati wa dirisha la uhamisho wa majira ya baridi.
"Waachezaji watatu wa mbele hawatoshi na mabeki wawili wa pembeni, hawatoshi. Wanahitajika wachezaji watano. Wanahitaji wachezaji watano ambao wanatosha kwenye mfumo huu ili kuweza kucheza mfumo wake anavyotaka." (Skysport)
Liverpool wameingia katika mbio za usajili wa Osimhen, Sesko
Liverpool wanatafuta mbadala wa Diogo Jota au Darwin Núñez katika safu ya ushambuliaji, huku Victor Osimhen wa Napoli na Benjamin Sesko wa RB Leipzig wakiwa kwenye rada zao.
Kwa bei ya takriban pauni milioni 70, Osimhen na Sesko wanaonekana ni nafuu zaidi kuwapata kuliko uwezekano wa kumnunua mshambuliaji wa Newcastle United Alexander Isak, ambaye uhamisho wake unaweza kugharimu zaidi ya £130m.
Arsenal, Juventus, PSG na Manchester United zote zinadaiwa kuwa na nia ya kuwanunua Osimhen na Sesko pia, kwa hivyo kunaweza kuwa na timu nyingi zinazopambana kuwania saini za nyota hao katika msimu wa joto (ESPN).
"Kama si Ronaldo na Zidane nisingekuwa Madrid" - Mbappe
Kylian Mbappe amefichua kwamba kama si nyota wawili wa zamani wa Real Madrid Cristiano Ronaldo na Zinedine Zidane, asingekuwa Madrid. Nyota hao walichochea ndoto yake ya kuhamia kwenye klabu hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mbappe alisema: "Ninaishi ndoto kila siku kucheza hapa. Zidane alikuwa mtu niliyempenda, nilianza soka kwa sababu yake. Klabu hii ni bora zaidi duniani. Tangu Cristiano atue hapa wakati huo nilifuatilia kila mechi; alikuwa mtu mwingine niliyemfuatilia. Nilikutana na Zidane hapa nikiwa na umri wa miaka 13. Nilikaa wiki moja huko Valdebebas na niliweza tu kuzungumza 'Kifaransa, lakini nilikuwa na nafasi ya kuzungumza na Zidane, haikuwezekana kwa sababu ya familia yangu sikuweza kuja peke yangu (Goal.com)
Wawakilishi wa Gyökeres kuiangalia Arsenal Emirates dhidi ya Madrid
Wawakilishi wa mshambuliaji wa Sporting CP Viktor Gyökeres watakuwepo kwenye uwanja wa Emirates kushuhudia Arsenal ikicheza robo fainali ya Ligi ya mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid. (Football Transfers)
Arsenal inasaka mshambuliaji na imemuweka kwenye orodha yake nyota huyo ambaye yuko kwneye kiwango kizuri katika misimu miwili iliyopita, akichapicha mabao 30 kutoa pasi za mabao 6 katika mechi 26 za ligi msimu huu.
Huenda Liverpool na Manchester United zikaingia kwenye mbio za kumuwania nyota huyo, Msweden huyo.
'Hakuna haraka' - Saka kuhusu mkataba mpya Arsenal
Nyota wa Arsenal, Bukayo Saka anasema 'hana haraka' ya kusaini mkataba mpya huku kukiwa na uvumi kwamba anaweza kuondoka Arsenal siku za usoni.
Lakini mchezaji huyo wa kimataifa wa Uingereza pia anasisitiza kuwa ana furaha Emirates na amedhamiria sana kushinda mataji akiwa na klabu yake hiyo ya tangu utotoni.
Mkataba wake umesalia miaka miwili, ambapo klabu yake inahaha kupata uhakika wa nyota huyo kusalia London.
Saka bila shaka amekuwa mchezaji bora wa Arsenal kwa miaka michache iliyopita, akiwa amechangia mabao 133 katika mechi 252. (Metro)