Je, maandamano ya Chadema yamefanikiwa?

dfv

Chanzo cha picha, REUTERS/Emmanuel Herman

Maelezo ya picha, Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA, Freeman Mbowe akikamatwa na polisi kabla ya kuanza kwa maandamano Septemba 23, 2024.
    • Author, Rashid Abdallah
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Msururu wa maandamano ya kusimamisha shughuli na kutikisa nchi kwa sehemu kubwa yalimaliza wakati wa utawala wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, wingi wa maandamano ya wakati huo – yalikifanya chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kupachikwa lakabu ya “Chama cha Maandamano” na wapinzani wao wa kisiasa, yaani chama tawala.

Kinachoshuhudiwa sasa ni matangazo makali ya maandamano lakini – maandamano yenyewe hayaji na uzito kama wa wakati ule. Kwa lugha nyingine unaweza kusema haya ya sasa ni ‘maandamano tepetepe.’

Lakini mwitikio mdogo, sio kipimo pekee cha kupima ikiwa maandamano yamefanikiwa au la. Na kabla hatujazama kwenye mjadala huo, kwanza tujiulize katiba ya Tanzania inasemaje kuhusu maandamano.

Mwanasheria Rugemeleza Nshala, ambaye aliwahi kuwa rais wa chama cha wanasheria Tanganyika ameiambia BBC, hatua ya polisi kuzuia maandamano si halali kwani Katiba ya Tanzania, inaruhusu kuandamana, kutoa hisia na kupinga vitu vinavyoonekana kuwa kinyume cha Katiba.

Kauli kama hiyo pia imesemwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, dakika chache kabla hajakamatwa na Jeshi la Polisi siku ya jana, akiwa katika eneo ambalo maandamano yangeanza katika jiji la Dar es Salaam, “maandamano ni haki ya kikatiba. Maandamano yetu ni ya amani.”

Nguvu Kubwa hutumika

K

Chanzo cha picha, IKULU TANZANIA

Maelezo ya picha, Rais Samia Suluhu Hassan

Tanzania ina historia ya muda mrefu ya kutumia nguvu kubwa kupita kiasi katika kuzima maandamano. Moja ya tukio kubwa na baya la kuzuia maandamano, ni lile lililosababisha mauaji ya makumi ya watu, majeruhi na wakimbizi katika visiwa vya Zanzibar.

Katika ripoti ya shirika la haki za binaadamu la Human Rights Watch, inasema mashambulizi ya vikosi vya usalama dhidi ya maandamano yaliyofanyika Zanzibar tarehe 27 Januari, 2001, kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa 2000, yalisababisha vifo vya watu 35, na wengine wapatao 600 kujeruhiwa na Wazanzibari 2,000 walikimbilia nchi jirani ya Kenya.

Ni kumbukumbu inayoashiria kuwa vikosi vya usalama vya Tanzania vina utamaduni wa tangu enzi wa kudhibiti maandamano, na wakati mwingine matokeo ya udhibiti huo yanakuwa mabaya.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Habari njema ni kwamba, katika maandamano ya jana, hakukutokea umwagaji damu, lakini uhudhuriaji haukuwa wa kusimamisha shughuli za nchi. Na hali hiyo haikuwa hivyo kwa bahati mbaya.

Kwa hakika kuna hofu ambayo mizizi yake ni marufuku ya tangu wakati wa hayati Rais John Pombe Magufuli. Kupitia vikosi vya usalama alifanya kazi kubwa kuzuia shughuli za kisiasa za vyama vya upinzani, yakiwemo maandamano.

Kulikuwa na vitisho vikubwa vikitolewa na maafisa wa ngazi ya juu wa Jeshi la Polisi, kwenda kwa wale wanaofikiria kuandamana.

Moja ya kauli maarufu ni ile ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa mji mkuu wa utawala wa Dodoma, wa wakati huo Gilles Muroto, akizungumza na waandishi wa habari Aprili 2018, alisema:

"Wanaopanga kuandamana kesho watakiona cha moto, watapigwa kama mbwa koko."

Oktoba 2020 Kamanda huyo pia alitoa kauli mfano wa hiyo, aliposema wanaotaka kuandamana waache kwani Polisi imejipanga kuwapa kipigo alichokiita cha mbwa koko.

Hayati Magufuli alifanikiwa pakubwa kuhakikisha kunakuwa na hofu kwa wanaowaza kuandamana, fauka ya hilo, alifuzu kuvitumia vikosi vya usalama kuhakikisha hofu hiyo inatamalaki vichwani mwa baadhi ya wafuasi wa upinzani.

Katika maandamano ya jana, ripoti zinasema dazeni ya wanachama wa Chadema wamekamatwa akiwemo Mwenyekiti wake Freeman Mbowe na Makamu Mwenyekiti, Tundu Lissu. Ingawa wao na wengine wengi tayari wameachiwa kwa dhamana.

Kwa mujibu wa taarifa ya polisi viongozi hao na wafuasi wengine wa Chadema, walikamatwa kwa tuhuma za kuhamasisha kufanya maandamano ambayo hayana kibali.

Je, maandamano yamefanikiwa?

x

Chanzo cha picha, CHADEMA TANZANIA

Maelezo ya picha, Jeshi la Polisi likiwa nje ya nyumba ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu kabla ya kumkamata siku ya jana

Turudi sasa kwenye mjadala mkuu: Januari 2023 wakati akizungumza na viongozi wa vyama vya kisiasa, katika kikao kilichofanyika katika Ikulu ya Dar es Salaam, Rais Samia Suluhu Hassan alitoa tamko la kuruhusu shughuli za nje za kisiasa, ikiwemo mikutano ya hadhara.

Wengi waliamini ndio mwanzo mpya wa uhuru wa kisiasa nchini Tanzania, baada ya kipindi kirefu cha shughuli za kisiasa za upinzani kuwa kifungoni.

Swali la ikiwa maandamano ya jana yamefanikiwa au la, bila shaka litakuwa na jawabu tofauti, kulingana na nani unaye muuliza.

Kwa ambaye anataka maandamano yawe chanzo cha serikali kurudi nyuma na kubadili msimamo, na matakwa ya wanaoandamana yatekelezwe, jawabu itakuwa, ‘bado maandamano haya hayajafanikiwa.’

Lakini kwa upande wa utawala, kuzuia maandamano inaweza kuingia katika hesabu ya ushindi, ingawa kwa nchi ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikituhumiwa kwa kukandamiza shughuli za upinzani, kuuhesabu huo kuwa ni ushindi, kwa hakika ni namna mbovu ya kuhesabu ushindi.

Wakati Chadema inashindwa kweli kufanikisha kile wanacho kitaka – yaani kuandamana hadi viwanja vya Mnazi Mmoja, lakini inafanikiwa kuuonesha ulimwengu kile kinachosemwa kuhusu ukandamizaji wa uhuru wa kisiasa nchini Tanzania.

Imehaririwa na Yusuf Jumah