Droni zaongezeka eneo la dhahabu na mafuta la Sudan- ngome mpya muhimu ya mapambano

    • Author, Barbara Plett Usher
    • Nafasi, Africa correspondent
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Idadi ya ndege zisizo na rubani imeongezeka eneo la dhahabu na mafuta la Sudan, Kordofan, na kuifanya kuwa mstari mpya muhimu wa mapambano. Mashambulizi haya yamesababisha vifo vingi vya raia katika wiki chache zilizopita na yanabadilisha mwelekeo wa mgogoro huo.

Kitovu cha mapigano sasa kimehamia eneo la Kordofan ya kusini-kati, baada ya jeshi la Sudan na vikosi vya Rapid Support Forces (RSF) kuimarisha nguvu zao katika maeneo mengine.

Mgogoro huu umegeuka kuwa moja ya migogoro yenye madhara makubwa zaidi kwa raia barani Afrika, na licha ya juhudi za amani, hakuna dalili thabiti za kupungua kwa mapigano.

Mashambulizi ya ndege zisizo na rubani yamelenga masoko, vituo vya afya, misafara ya misaada ya kibinadamu, na maeneo ya makazi katika eneo la Kordofan. Hali hii imezua wasiwasi na kulaaniwa vikali na Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada.

"Mashambulio yanayoendelea kufanywa na pande zote dhidi ya miundombinu ya kiraia lazima yakome," mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk alisema wiki iliyopita.

"Pande zote mbili lazima zichukue hatua za dharura kulinda raia, ikiwa ni pamoja na kujiepusha na matumizi ya kijeshi ya miundombinu ya kiraia.''

Alikuwa akizungumza baada ya ripoti kuwa zaidi ya raia 50 wameuawa kwa muda wa siku mbili katika mashambulizi tofauti ya ndege zisizo na rubani huko Kordofan Kaskazini na Magharibi.

Mashambulizi hayo yalilaumiwa kwa jeshi la Sudan na ripoti za ndani na wachunguzi wa vita, lakini pande zote mbili zinashutumiwa kwa mashambulizi mabaya kwa raia na miundombinu ya kiraia.

Eneo la Kordofan linajumuisha majimbo matatu na ina thamani kubwa ya kimkakati, kwani inaunganisha eneo la magharibi la Darfur na mji mkuu wa Sudan, Khartoum ambalo sasa liko mikononi mwa jeshi.

Vita vilizuka Aprili 2023 baada ya mvutano wa madaraka kati ya viongozi wa Jeshi la Sudan na RSF.

RSF imekuwa ikipambana na jeshi la Sudan kwa muda mrefu, na kuunda muungano na vuguvugu la waasi la Sudan People's Liberation Movement-Army North (SPLM-N). Hii imewapa nguvu na udhibiti wa maeneo na njia za kimkakati.

Mapigano yalianza kushika kasi katika eneo la Kordofan, ukanda wa kimkakati wenye utajiri mkubwa wa dhahabu na mafuta, mara baada ya Jeshi la Sudan (SAF) kurejesha udhibiti wa mji mkuu, Khartoum, mwaka uliopita.

Eneo la kusini-kati likageuka kuwa uwanja mkuu wa mapambano kufuatia RSF kuimarisha mamlaka yake katika Darfur kwa kuuteka mji wa el-Fasher mwezi Oktoba mwaka jana.

Kupata udhibiti kamili wa majimbo ya Kordofan kungeiweka RSF katika nafasi ya kudhibiti ukanda wa kati wa Sudan, mhimili muhimu wa kijiografia na kisiasa wa taifa hilo.

RSF ilianzisha serikali sambamba mwaka jana, hatua iliyozidisha na kuimarisha mgawanyiko wa kivitendo wa taifa hilo.

Hatua hiyo ilichukuliwa kwa ushirikiano na kundi la waasi la Sudan People's Liberation Movement–Army North (SPLM-N), lenye makao yake katika Kordofan Kusini, na hivyo kuipatia RSF fursa ya kupata wapiganaji wenye uzoefu, udhibiti wa maeneo pamoja na njia za mipakani.

Kwa miongo kadhaa, SPLM-N imekuwa ikipigana dhidi ya serikali kuu na majeshi ya taifa, ikidai kukomeshwa kwa kutengwa kisiasa na kiuchumi kwa maeneo ya Nuba na Blue Nile nchini Sudan.

Hata hivyo, jeshi la Sudan limepata mafanikio ya kimkakati kwa kuvunja mzingiro wa RSF na washirika wake SPLM -N katika miji ya Kadugli na Dilling, Kordofan Kusini.

Wachunguzi wa usalama wa chakula wanasema kwamba mizingiro hiyo ilisababisha hali ya njaa kali.

Tangu kuchukuliwa kwa miji hiyo, SAF imeongeza mashambulizi yake ya misimamo ya RSF, ikiwa ni pamoja na silaha zake za anga.

RSF na jeshi la Sudan zote zinatumia ndege zisizo na rubani katika mapigano.

Inaripotiwa kwa upana kuwa wanatumia ndege zisizo na rubani za masafa marefu za Kichina aina ya CH-95, zinazodaiwa kusambazwa na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), madai ambayo UAE imeyakanusha.

Jeshi la Sudan hutumia ndege zisizo na rubani kutoka kampuni ya Baykar, mkandarasi mkubwa zaidi wa sekta ya ulinzi nchini Uturuki. Inaaminika kuwa katika mwaka uliopita, uwezo wake uliimarishwa zaidi kwa kupokea mifumo ya kisasa ya kivita aina ya Akinci.

Serikali ya Uturuki imesema haitoi msaada wa moja kwa moja kwa Jeshi la Sudan (SAF).

Mapema mwezi Februari, jeshi la Sudan lilitangaza kuwa limeharibu ndege zisizo na rubani pamoja na makombora ya kujihami dhidi ya mashambulizi ya anga yaliyokuwa yakimilikiwa na RSF katika maeneo ya Kordofan na Darfur.

Msemaji wake, Brigedia Jenerali Asim Awad, alisema hatua hiyo ilikuwa "sehemu ya mkakati wa kuvunja na kudhoofisha uwezo wa anga usio wa kawaida unaotumiwa na RSF."

BBC haikuweza kuthibitisha kwa uhuru taswira zilizochapishwa na shirika la habari la serikali ya Sudan. Hata hivyo, vyombo vya habari vya Uturuki viliripoti kuwa tarehe 10 Februari, ndege isiyo na rubani aina ya Akinci iliharibu mfumo wa ulinzi wa anga wa Kichina aina ya FK-2000 nchini Sudan.

"Ikiwa miundombinu ya ulinzi wa anga ya RSF itaanguka, ukombozi wa Sudan unaweza kuwa karibu," mtaalam wa ulinzi wa Uturuki Yusuf Akbaba alichapisha kwenye X.

Siku tano baadaye jeshi lilitangaza tena kuwa lilikuwa limeharibu mfumo wa ulinzi wa anga wa RSF, katika jimbo la Kordofan Magharibi.

Inaonekana kusonga mbele kwa jeshi kulisaidiwa na kuvurugika kwa njia za usambazaji za RSF kutoka Libya kuelekea eneo la Kordofan, ambazo zinaripotiwa kulengwa na ndege zisizo na rubani za Uturuki zilizorushwa kutoka uwanja wa ndege wa Misri ulio karibu na mpaka wa Sudan.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti la The New York Times pamoja na shirika la habari la Reuters umebaini kuwa Misri imeongeza ushiriki wake katika vita hivyo katika kipindi cha miezi sita iliyopita, ikihofia kuimarika kwa RSF katika eneo la Darfur.

Mashambulizi ya hivi karibuni yaliyoongozwa na SPLM-N katika Jimbo la Blue Nile, kusini-mashariki mwa Kordofan, pia yanatishia kupanua vita vya Sudan na kuvigeuza kuwa mgogoro wa kikanda.

Jimbo hilo ni ukanda mwembamba wa ardhi unaojitokeza kati ya Ethiopia na Sudan Kusini.

Jeshi la Sudan limezituhumu nchi hizo mbili kwa kuruhusu RSF kutumia maeneo yao kuzindua mashambulizi. Addis Ababa na Juba zimekanusha tuhuma hizo, huku Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) nao ukikanusha ripoti tofauti zilizodai kuwa unafadhili kambi ya mafunzo ya RSF nchini Ethiopia.

Wachambuzi wanaamini kuwa RSF na washirika wake wa SPLM-N wanajaribu kufungua mstari mpya wa mapambano katika eneo la Blue Nile, kwa sehemu ili kupunguza shinikizo wanalokumbana nalo katika eneo la Kordofan.

"Ndugu zetu katika Jimbo la Blue Nile wanafanya kazi nzuri," alisema kiongozi wa RSF, Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, wakati wa ziara yake nchini Uganda wiki iliyopita.

"Umbali kule ni mfupi [akirejelea ukaribu wake na maeneo ya mashariki yanayodhibitiwa na jeshi]. Si kama Darfur."

Mapema mwezi huu, mjumbe maalum wa Marekani, Massad Boulos, alisema ana matumaini ya kufanikisha makubaliano ya kusitisha mapigano ifikapo mwezi wa Ramadhani, ulioanza tarehe 18 Februari.

Hata hivyo, siku ya kwanza ya mwezi huo mtukufu wa Kiislamu, shambulizi la ndege isiyo na rubani lililolaumiwa kwa jeshi la Sudan liliwalenga familia zilizokuwa zimekusanyika katika eneo la kuchota maji huko Kordofan Magharibi. Watoto wadogo walikuwa miongoni mwa waliouawa.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid