Fahamu mataifa ya kigeni yanayohusishwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan

    • Author, Mahammad Maalim na Yussuf Abdullahi
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan bado vinaendelea zaidi ya miaka miwili na nusu tangu vilipoanza, na miongoni mwa sababu zinazochochea kudumu kwake ni uingiliaji wa mataifa ya kigeni yanayotoa msaada wa kisiasa na kijeshi kwa pande hasimu.

Kwa mujibu wa mashirika ya haki za binadamu, zaidi ya watu 150,000 wamepoteza maisha, huku zaidi ya milioni 12 wakilazimika kuyahama makazi yao.

Licha ya kuwepo kwa vikwazo vya kimataifa vya usafirishaji wa silaha, jeshi la Sudan na wanamgambo RSF wanaendelea kupata silaha kwa wingi kutoka nje ya nchi.

Maslahi yanayokinzana ya mataifa ya eneo hili yamegeuza mzozo huu kuwa vita tata vinavyotishia kuleta machafuko makubwa zaidi katika Pembe ya Afrika na kanda nzima.

Ukali wa mapigano ulidhihirika hivi karibuni baada ya RSF kuuteka mji wa El-Fasher, makao makuu ya jimbo la Darfur Magharibi, ambapo kundi hilo lilishtakiwa kwa kufanya mauaji ya kikatili.

Makala haya yanachunguza kwa kina wahusika wa kigeni wanaohusishwa na mzozo huu ambao umezaa moja ya mizozo mikubwa zaidi ya kibinadamu duniani.

Ni akina nani wanaoiunga mkono serikali ya kijeshi ya Sudan

Jeshi la Sudan linadaiwa kunufaika na uungwaji mkono kutoka kwa mataifa kadhaa, yakiwemo Misri, Uturuki, Iran, Urusi, na Eritrea, ambayo yanatuhumiwa kutoa msaada wa moja kwa moja wa kijeshi.

Baada ya vita kuanza mnamo Aprili 2023, Mkuu wa Majeshi ya Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, alifanya ziara yake ya kwanza nchini Misri, hatua iliyothibitisha uhusiano wa karibu kati ya nchi hizo mbili. Taarifa nyingi zimebainisha kuwa Cairo imekuwa ikiunga mkono jeshi la Sudan.

Kiongozi wa RSF, Luteni Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo (Hemedti), amekuwa akishutumu mara kwa mara Misri kwa kulisaidia jeshi la Sudan kwa silaha, zikiwemo ndege za kivita.

Tarehe 5 Novemba 2025, RSF ilidai kuwa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani yaliyotekelezwa Darfur Magharibi yalitoka "vituo vya kigeni" ikihusisha Misri, ingawa Cairo imekanusha kuhusika.

Uturuki, licha ya kujitangaza kuwa na msimamo wa upande wa kati, inaripotiwa pia kuwa imetoa ndege za kivita zisizo na rubani zilizochangia sana katika jeshi kurejesha udhibiti wa maeneo ya kati, yakiwemo Khartoum.

Mnamo mwezi Machi 2025, vyombo vya habari vya Uturuki viliripoti kuwa kampuni kubwa ya silaha ya nchi hiyo, Baykar, ilipeleka ndege za kivita na mamia ya viunganishi vya mabomu kwa jeshi la Sudan.

Kwa mujibu wa taarifa za Middle East Eye, mnamo Novemba 6, 2025, Uturuki na Misri ziliongeza usaidizi wao kwa jeshi baada ya RSF kuuteka mji wa El-Fasher.

Aidha, kuna madai kuwa Urusi na Iran pia zinatoa ndege za kivita na droni kwa jeshi hilo la Sudan.

Mnamo Oktoba 2024, Hemedti alimshtumu Tehran kwa kutoa msaada wa kijeshi kwa jeshi hilo, lakini Iran haikutoa majibu rasmi.

Ripoti ya Bloomberg (Oktoba 2024) ilieleza kuwa Iran na Urusi zimejadiliana na jeshi kuhusu ujenzi wa vituo vya kijeshi katika pwani ya Bahari ya Shamu.

Ingawa Iran ilikanusha, Urusi ilisaini makubaliano na serikali ya kijeshi ya Sudan mnamo Februari 2025 kuanzisha kituo cha kijeshi cha majini nchini humo, azma ambayo Moscow imekuwa nayo tangu 2017.

Eritrea, kwa upande wake, haijaficha uungaji mkono wake kwa jeshi la Sudan. Mnamo Januari 2025, wanamgambo wanaoegemea upande wa jeshi walidai kupokea mafunzo na silaha kutoka nchini humo.

Nchi ya Saudi Arabia pia inadaiwa kuliunga mkono jeshi, ingawa rasmi imesisitiza msimamo wa kutokupendelea upande wowote.

Ni akina nani wanaoiunga mkono RSF

Kundi la RSF linadaiwa kupata msaada mkubwa kutoka Falme za Kiarabu (UAE), ikiwemo silaha, vifaa vya tiba, na msaada wa vifaa vingine vya kijeshi.

Ripoti mbalimbali, zikiungwa mkono na wataalamu wa Umoja wa Mataifa, zinaonyesha kuwa UAE imetuma magari ya kivita, droni, na silaha nzito kupitia Chad, Sudan Kusini, Libya, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), na Somalia.

Kenya imetajwa mara kadhaa kama mwenyeji wa viongozi wa RSF na shughuli zao za kisiasa.

Mnamo Februari 2025, Nairobi iliandaa mkutano wa kisiasa wa ngazi ya juu ambapo RSF ilitangaza kuunda serikali mbadala, hatua iliyosababisha Sudan kumrejesha balozi wake kutoka Kenya.

Serikali ya kijeshi ya Sudan baadaye ilikata uhusiano wa kidiplomasia na UAE, Kenya, na Chad, ikizituhumu kwa kuisaidia RSF. Pia ilishtumu Jeshi la Kitaifa la Libya (LNA) na Sudan Kusini kwa kutoa msaada wa wapiganaji na kuwahudumia majeruhi wa RSF.

Hata hivyo, mataifa yote hayo yamekanusha kuhusika kwa namna yoyote.

Wa hivi punde ni Rais wa Kenya William Ruto akizungumza na shirika la habari la Al Jazeera alishikilia kuwa Kenya inasalia kuwa nchi ya kidemokrasia inayokaribisha makundi yote yanayopenda amani.

"Kenya ni demokrasia kubwa katika eneo hili. Sisi ndio mahali pekee ambapo watu wanaweza kuja na kukutana kwa uhuru," Ruto alieleza wakati akijibu maswali kuhusu hali ya kibinadamu katika eneo hilo.

Pia alizingatia hali ya mzozo huo, akisisitiza kwamba Vikosi vya Wanajeshi vya Sudan (SAF) na RSF vinawajibika kwa usawa kwa machafuko yanayoikumba nchi hiyo.

"Msimamo wangu ni kwamba majenerali hawa wawili SAF na RSF hawana suluhu kwa mgogoro wa Sudan kwa sababu wote wanaamini kwamba wanapaswa kutumia njia za kijeshi kusuluhisha hali hiyo. Hili ni tatizo la utawala," Ruto alibainisha.

Soma pia:

Soko la silaha na wapiganaji wa kulipwa

Baadhi ya nchi ambazo hazihusiki moja kwa moja na vita zimegeuka kuwa masoko ya silaha na vyanzo vya wapiganaji wa kulipwa.

Mnamo Oktoba 2025, Pakistan na jeshi la Sudan walisaini mkataba wa ulinzi wa dola milioni 230 unaojumuisha ndege za mafunzo, droni, magari ya kivita, na utengenezaji wa pamoja wa vifaa vya kijeshi.

Vyombo vya habari vya Sudan vimeripoti kuwa jeshi linatafuta kununua ndege za kivita za kisasa za Urusi aina ya Sukhoi kutoka Kazakhstan na Uzbekistan.

Kwa upande mwingine, RSF inadaiwa kutumia silaha na droni za Kichina ambazo zilinunuliwa awali na Falme za Kiarabu kabla ya kufikishwa kwake.

Wakati huo huo, madai dhidi ya Kenya kuwauzia silaha RSF yalitokana na uchunguzi wa pamoja wa shirika la habari nchini humo NTV na jukwaa la kijasusi la Bellingcat, ambalo lilifichua picha za makreti ya risasi yenye lebo ya Kenya yanayodaiwa kupatikana katika ghala la RSF lililotekwa karibu na mji mkuu wa Sudan, Khartoum.

Ingawa yaliyomo katika kila kreti hayakuweza kuthibitishwa kwa uhuru, risasi za karibu zinazolingana na lebo zinazoonyesha silaha zilizonunuliwa au kutumwa Kenya kwa Wizara ya Ulinzi zilionyeshwa na Wanajeshi wa Sudan kwenye video zinazosambazwa hivi sasa. Hata hivyo, serikali ya Kenya ilikanusha mashtaka yote.

Kundi hilo pia linadaiwa kuajiri wapiganaji wa kulipwa, wakiwemo wataalamu wa kijeshi na marubani kutoka nchi kadhaa za Afrika, Ukraine, na Kolombia.

Mnamo 5 Novemba 2025, Waziri wa Ulinzi wa Somalia aliripoti kuwa ndege zisizotambulika ziliruka kutoka Uwanja wa Ndege wa Bosaso, zikienda "kubeba kitu" kuelekea Darfur.

Taarifa zaidi zilidokeza kuwa UAE inautumia uwanja huo kusafirisha silaha na wapiganaji wa kulipwa kwa RSF.

Awali aliyekuwa naibu mkuu wa Kenya Rigathi Gachagua alihusisha utawala wa Kenya katika kuuzia silaha wanamgambo wa RSF.

Hata hivyo, Rais wa Kenya amepuuzilia mbali madai yanayomhusisha na wanamgambo wa (RSF), akikanusha madai kwamba utawala wake ulihusika na ulanguzi wa silaha .

Na vipi kuhusu mazungumzo ya amani?

Katika miezi ya karibuni, Marekani imeongeza jitihada za kidiplomasia kupitia mchakato wa Quad, unaojumuisha Saudi Arabia, Misri, na Falme za Kiarabu, kwa lengo la kuweka usitishaji wa mapigano wa kibinadamu wa miezi mitatu, kisha makubaliano ya kudumu ya amani.

Hata hivyo, tofauti za ndani kati ya mataifa ya Kiarabu zinazoshiriki katika mazungumzo hayo zimekuwa zikikwamisha juhudi hizo.

Mnamo Novemba 6, RSF ilikubali pendekezo la kusitisha mapigano, lakini jeshi bado lilipinga hatua hiyo.

Jeshi limekataa ushiriki wa Falme za Kiarabu katika mazungumzo hayo, likitaka washirikishwe Uturuki na Qatar.

Kwa sasa, kutokana na misimamo mikali ya pande zote mbili na kuimarika kwa ushirika wa moja kwa moja na wa siri kati ya wahusika wa kigeni, matumaini ya kupatikana kwa amani ya haraka Sudan yanaendelea kudidimia.

Taarifa hii pia imeandikwa kwa ushirikiano na Mariam Mjahid.