Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ni zipi athari za wazazi wenye hasira kwa watoto?
“Wazazi wangu walinifanya nihuzunike sana. Nililia karibu kila siku, lakini mwishowe nikaona ni bora kuwapuuza."
Sio kawaida kusikia maneno kama haya kutoka wa binti, ingawa naye sasa amekuwa mama. Hata hivyo, Sarika anasema tabia ya wazazi wake ya unyanyasaji na hasira kwa miaka mingi imeharibu afya yake ya akili.
Mwanamke huyu mwenye umri wa miaka thelathini ni mkazi wa Malaysia. Aliambia BBC: "Iliniathiri sana, hasa nilipokuwa mjamzito. Nina hakika mtoto ambaye alikuwa tumboni alinisikia nikilia."
Sarika amepunguza mawasiliano na wazazi wake, lakini uamuzi wa kuwa mbali na wazazi wake haukuwa rahisi kwake.
Watu wengine wengi pia wamechapisha video kwenye TikTok na mitandao mingine ya kijamii na kusema jinsi walivyotengana na wazazi wao kwa sababu ya tabia yao ya hasira.
Wanasema tabia ya hasira za wazazi wao imewafanya wawe na hofu maisha yao yote tangu utoto.
Athari za utotoni na ukubwani
Mwanasaikolojia Eve Adisiwi, ambaye amesajiliwa na Shirika la Tiba ya Saikolojia la Uingereza, anasema: "Idadi ya watu wanaotafuta matibabu kutokana na athari ya hasira ya wazazi ni kubwa sana."
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF linasema: "Malezi bora yanahusisha matendo ya heshima kwa watoto na sio ukali.”
Ingawa hakuna ufafanuzi maalumu kuhusu mzazi mwenye hasira, lakini neno hilo hutumika kwa wazazi wenye sifa na tabia mbaya kwa watoto wao.
Ayo Adisiwi anatoa mfano, “ikiwa mzazi anamuuliza mtoto wake kuhusu marafiki zake. Je, ana rafiki au hana? Hii linakuwa ni swali la kawaida, lakini ikiwa swali hili ni kwa ajili ya udhibiti, litakuwa na athari mbaya kwa mtoto.”
"Wakati mwingine wazazi hawaelewi na hufanya hivi kwa kutojua."
Matokeo ya utafiti wa mwaka 2013 wa Chuo Kikuu cha California, Los Angeles na UCLA, yanaonyesha watoto wanaokabiliwa na msongo wa mawazo wakiwa wadogo wanakuwa na shinikizo la damu na kisukari kadri wanavyozeeka.
Malezi mabaya kwa watoto
Katika chumba chake cha ushauri, Hawa Alessivi amegundua aina mbili za wazazi wenye hasira; wazazi wanaoingilia kazi ya watoto wao, maisha ya kijamii, elimu, au mahusiano na wazazi ambao watoto wao sio kipaumbele. Anasema makundi haya mawili ya wazazi mara nyingi yana sifa zinazofanana.
Mshauri wa saikolojia Alison Koerner anasema kuna aina nyingine ya wazazi:
- Wazazi wanaofanya maamuzi kuhusu watoto wao bila kushauriana nao.
- Mzazi ambaye huona makosa katika kila jambo analofanya matoto wake.
- Mzazi ambaye anakosa kitu fulani katika maisha yake na anataka kukitimiza kupitia maisha ya watoto wake.
- Wazazi ambao ikiwa watoto wao wanafanya jambo bora kuliko wao, huwakemea, wakati huo huo huwakosoa.
- Wazazi ambao huwakemea watoto wao kwa mambo madogo madogo.
- Akina baba wanaomuachia mwanamke maamuzi yote.
Ayo Alisivi anasema licha ya kukumbana na visa vingi vya kuhuzunisha katika fani hii, pia amewahi kuwatibu na kuwasaidia watu waliokuwa wakifikiria kujiuwa kutokana na tabia ya wazazi wao.
Miiko ya kitamaduni
Sarika anasema alijaribu kuzungumza na mtu wa tatu nje ya familia yake lakini anasema alishindwa: "Utamaduni wetu uko hivi, kila mtu anadhani watoto ndio wenye makosa na mama na baba wako sahihi."
Mwanasosholojia wa Chuo Kikuu cha Hong Kong Profesa Charis Shun Chin-chan anasema, mambo mbalimbali ya kijamii na kiuchumi yanaweza kuchangia hasira za mzazi.
Kwa mfano, sheria ya China ya mtoto mmoja, imeweka shinikizo kubwa kwa mtoto huyo mmoja. Anasema "Mtoto huyo yuko chini ya shinikizo kubwa kutimiza matarajio na mahitaji yote ya wazazi wake, kwa sababu wazazi wake watakuwa wamejitolea sana kumpa kila kitu."
Anasema: "Aina ya malezi ya hasira kwa watoto ni magumu kwa watoto."
Eve Alessivi anasema watoto waliokulia chini ya unyanyasaji, pamoja na kusumbuliwa na shida nyingine, huwa hawajiamini, hawajionei huruma, hawana huruma na wengine, na ni vigumu sana kuomba msaada kutoka kwa wengine.
Kukabiliana na wazazi wenye hasira
Sarika anasema baada ya ndoa yake, uhusiano na wazazi wake umekuwa mbaya zaidi.
"Baba yangu na mama yangu husema wamenifanyia kila kitu na mimi sijawafanyia chochote, na pia husema nimewatukana."
Dk Asha Patel, kutoka kampuni inayotoa msaada wa kisaikolojia kwa watoto na vijana nchini Uingereza, anasema ni jambo la kawaida kufikiria kuwa una wazazi wenye hasira, lakini cha muhimu ni kujishughulikia mwenyewe na kujipa kipaumbele.
Anaongeza: "Hakuna mtu mwingine aliye katika hadithi yako ya afya ya akili. Kwa hiyo mtu pekee anayeweza kufanya hivyo ni wewe."
“Epuka kuingia kwenye mabishano yasiyo ya lazima na wazazi wako. Jiwekee mipaka na kubali kuwa wewe si mtoto tena na umekua,” anasema Ayo Adisiwi.
Sarika anasema: "Sitaki kuwa kama wazazi wangu. Nataka kumsaidia binti yangu. Kumtunza vizuri na kumwacha afanye maamuzi yake ya maisha na ikiwa anataka ushauri, nitakuwa pale kila wakati kwaajili yake. "