Maandamano Kenya:Mateso yatakuwa jambo la kawaida iwapo Ruto ataruhusiwa kutekeleza Sheria ya Fedha-Raila

th

Chanzo cha picha, AFP

    • Author, Yusuf Jumah
    • Nafasi, BBC Swahili

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya amesema Wakenya wataendelea kuteseka iwapo serikali yar ais William Ruto itaruhusiwa kutekeleza sheria ya fedha inayopendekeza kuongezwa kwa ushuru .

Katika mkutano na waandishi wa habari ,Odinga ametangaza kuahirisha mkutano wa hadhara katika eneo la Kamukunji jijini Nairobi kutokana na kile alichosema ni ‘njama ya kuwashambulia viongozi wa Azimio’.

Amesema hali ya kawaida itarejelewa tu wakati rais Ruto atakapojitokeza na kubadilisha sheria hiyo na kutangaza mikakati ya kupunguza gharama ya maisha Pamoja na kukubali mazungumzo ya kuunda upya tume ya uchaguzi na mipaka .

Maelezo ya video, Jinsi polisi walivyokabiliana na waandamanaji nchini Kenya

Odinga amesema maandamano yanayoongozwa na upinzani ni ya amani na ghasia hutokea wakati polisi wanapoingilia kuyavunja na kuwatupia vitoa machozi waandamanaji .

Amesema Ruto lazima akome kuingilia masuala ya chama cha Jubilee na wabunge wa Jubilee wanaotaka kuhama wako huru kufanya hivyo lakini wanafaa kukiacha chama hicho katika muungano wa Azimio.

Kiongozi huyo upinzani amesema maandamano yaliyoshuhudiwa katika sehemu mbali mbali za nchi ni ujumbe tosha kwa utawala wa rais Ruto kwamba wananchi ‘wamechoka’ hasa kutokana na gharama ya juu ya maisha .

th

Chanzo cha picha, AFP

Kumekuwa na ripoti za watu watano kuuawa -mmoja katika eneo la Emali ,kaunti ya Makueni ,mashariki mwa Kenya baada ya polisi kuwafyatulia risasi waandamanaji walioliteketeza gari la serikali na kurusha mawe katika benki moja na wengine kujeruhiwa katika sehemu mbali mbali za nchi .

Kumekuwa pia na matatizo ya usafiri na biashara nyingi kufungwa katika miji kadhaa kama vile Nairobi,Mombasa,Kisumu Machakos na Nakuru .

Waandamanaji wameamua kuwasha moto barabarani, huku wafanyikazi wa usafiri wa umma wanaogoma wakishiriki katika shughuli kama vile michezo ya kandanda kwenye vituo vya mabasi, kama inavyonaswa kwenye video zinazosambazwa mtandaoni.