Maandamano ya kila mara baada ya uchaguzi Kenya: Faida au hasara?

mm

Chanzo cha picha, Reuters

    • Author, Alutalala Mukwana
    • Nafasi, Wakili na mchambuzi wa maswala ya kisiasa

Raila Amollo Odinga, ndiye mwanasiasa pekeee wa Kenya aliye hai, ambaye amewahi kushikilia cheo cha Waziri Mkuu nchini Kenya. Wa kwanza alikuwa hayati Rais wa kwanza wa Kenya Mzee Jomo Kenyatta, mnamo mwaka wa 1963 hadi 1964 baada ya Kenya kupata uhuru.

Vilevile, ndiye mwanasiasa pekee aliye hai ambaye katwikwa shani ya kuitwa baba wa demokrasia ya vyama vingi, sawia na marehemu Keneth Matiba.

Lakini ni vipi, kwa mara ya tano, Bwana Raila ameshindwa kura za Urais?

Mbona kila mara ashindwapo, hulalamika kwamba kaibiwa kura?

Na je, mbona huita wafuasi wake kuandamana kila mara apotezapo kinyang’anyiro cha Urais?

Je, maandamano hayo yamekuwa na faida zo zote kwa wafuasi wake, kwa taifa la Kenya au hata kwake yeye binafsi?

Na huyu Bwana Raila, ameanzia wapi siasa hizo za maandamano?

mm
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Historia fupi yake Raila Odinga itatupa taswira ya mwanaharakati sugu tangia miaka ya themanini.

Aliingia katika umaarufu wa kitaifa mwaka wa 1982 pale alipokamatwa na kuzuiliwa kizuizini bila kusikizwa mashtaka yake mwaka wa 1982.

Mwaka huo, kuliripotiwa majaribio ya kuipindua serikali yake mwendazake Rais Daniel Moi na hapo kashukiwa yeye Raila kuyachochea majaribio hayo. Alizuiliwa kizuizini hadi Februari 1988, ambapo aliachiliwa kwa kipindi kidogo kabla ya kukamatwa tena Septemba 1988.Wakati huo alikaa korokoroni hadi Juni 1989, alipoachiliwa.

Lakini punde, alikamatwa tena, wakati huu wakikamatwa pia wanaharakati Keneth Matiba na Charles Rubia.

Aliachiliwa Juni 1991na papo hapo akatorokea usalama wake nchini Norway.

Raila Odinga alirejea muda mfupi baadaye, kujiunga na harakati za kupigania haki na maslahi ya raia mwezi Februari 1992.Alijiunga na chama kipya cha FORD (“Forum for the Restoration of Democracy”) kikiongozwa na baba yake, yaani Jaramogi Oginga Odinga. Papo hapo alipewa nafasi ya Naibu mwenyekiti wa kamati ndogo chamani humo.

od

Wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka wa 1992 chini ya katiba kongwe ya Kenya ulipokaribia, FORD kilipasuka katikati-upande mmoja kazaliwa FORD KENYA yake Jaramogi, na kwa nusu ya upande mwingine kazaliwa FORD ASILI yake Keneth Matiba, huku Mbunge maarufu wa zamani wa Butere, mwendazake Martin Shikuku, almaarufu (“Peoples’ Watchman”) akiwa Katibu Mkuu wake.

Katika uchaguzi huo wa mwaka1992, Raila Odinga aliwania kiti cha ubunge cha Lang’ata katika jiji kuu la Nairobi. Hakuwania Urais hivyo hakukutokea maandamano ya wafuasi wake kufuatia uchaguzi huo.

Mwaka 1994 ulikuwa ni wa tanzia katika familia yake Raila Odinga, pale ambapo baba yake, Jaramogi Odinga, aliaga dunia huku akimwacha mwanaye huyu akishikilia wadhifa wa Mkurugenzi wa maswala ya Kura katika chama.

Katika uchaguzi mkuu wa 1997,Raila Odinga aliwania Urais lakini alibwagwa na Mzee Moi kwa wingi wa kura, huku aliyefuatia kwa karibu katika nafasi ya pili akiwa Rais mwendazake Mwai Kibaki. Wakati huo, hakukufanyika maandamano ila Raila alitafuta mbinu ya kujiingiza serikalini matumaini na mikakati yake ikilenga huwania Urais baadaye kupitia chama chake Rais Moi.

Si ajabu pia, alitarajia kuungwa mkono na Rais huyo kwa vile alikwisha kivunja chama chake cha NDP kwa kujiunga uko, nacho chama cha KANU kageuza jina lake na kuitwa New KANU ( maana yake KANU chama Kipya.

Yote tisa, la kumi ni kwamba, katika uchaguzi uliofuatia, wa mwaka 2002, Raila Odinga hakuwania. Badala yake alimuunga mkono Mwai Kibaki ambaye baadaye alishinda kiti cha Urais mwaka huo.

Hivyo, uhakiki mwafaka wa maandamano ya wafuasi wake Raila Odinga wakipinga kushindwa kwake kinyang’anyiro cha Urais sharti uanzie chaguzi zilizofuatia baadaye hususan miaka ya 2007,2013,2017 na 2022.

Je, katika uchaguzi wa 2007,kipi kilijiri kiasi cha kumfanya Raila Odinga apinge matokeo hayo?

Je, malamishi yake yalikuwa na msingi wo wote?

Je, maandamano yaliyojiri, yalimfaidi nani na yalimdhuru nani?

NN

Ikumbukwe kwamba kisirani cha matokeo ya mwaka huo kilijikita mizizi yake katika namna Rais Kibaki alivyoendesha serikali yake ya kipindi cha awali, yaani miaka ya 2002 hadi 2007.

Ilivyojiri ni kwamba kukielekea mwaka wa 2002,Raila Odinga alihitilafiana pakubwa na Rais Moi kutokana na sababu kwamba Rais Moi alimteua Uhuru Kenyatta awe mrithi wake baada ya yeye Mzee Moi kustaafu.

Raila, kama vile walivyoparamia viongozi wenzake pia katika New KANU wakati huo, wakiwemo Makamu Rais wakati huo Prof. George Saitoti, katibu mkuu wa KANU hapo awali JJ Kamotho, aliyekuwa Waziri wa Maswala ya Utalii Kalonzo Musyoka na wengine, alitarajia apewe yeye mwenge wa kuongoza New KANU na kuwania Urais kupitia tiketi ya New KANU.

Huku Moi akishikilia msimamo wake bila kuugeuza, maasi makubwa yalizuka chamani humo. Raila Odinga aliwaongoza viongozi hao na wengine tajika kukigura chama cha New KANU chenye nembo ya Jogoo. Pamoja na kiongozi wa chama cha FORD-People wakati huo, Simeon Nyachae, kiongozi wa National Alliance Party (NAK) Mwai Kibaki na Charity Ngilu, walianzisha vuguvugu la National Rainbow Alliance(NARC) na baadaye ukawa muungano mkubwa wa vyama vingi.

Punde, kwa tamaa za uongozi baina yao, sintofahamu zikazuka katika muungano huo huku Simeon Nyachae, George Saitoti, Kalonzo Musyoka na wengineo wakishindania kuipeperusha bendera ya muungano huo.

Raila Odinga, pekee yake, akiuhutubia mkutano wa halaiki kubwa kuwai kuonekana enzi hizo katika uwanja wa Uhuru Park, Nairobi, alitangaza kwamba “Kibaki Tosha”. Kwa kauli hiyo, umati wa wafuasi wao ukamkubali Mwai Kibaki kuwa ndiye angepeperusha bendera ya muungano wao, ambao sasa uliitwa NARC (National Rainbow Coalition”.)

Isitoshe, Raila Odinga aliingia mkataba na Mwai Kibaki kwamba angelipewa nusu ya idadi ya mawaziri serikalini wakishinda uchaguzi huo. Kadhalika, Raila Odinga angeteuliwa Waziri Mkuu wa taifa la Kenya.

Je, Kibaki alitii mkataba huo?

La hasha!

Alipuzilia mbali mkataba huo asimpe Raila Odinga wadhifa wa Waziri Mkuu wala nusu ya idadi ya mawaziri katika serikali yake. Hapo ndipo mbegu za chuki zilipopandwa baina yao. Kitumbua cha kura za 2007 kiliingiwa mchanga, kisilike tena!

mm

Ikumbukwe kwamba punde baada ya kampeni ya uchaguzi huo wa 2002 kuanza, Mwai Kibaki alihusika katika ajali mbaya ya barabarani na kumfanya asiwe ni mwenye nguvu za kupiga kampeni tena.

Jukumu zima la kampeni hizo likatwikwa mebegani mwa Raila Odinga, huku akichukua usukani wa kampeni hizo. Kuwatia moyo wafuasi wao, alisema kwamba “Kapteni” wa kikosi chao kajeruhiwa tu, lakini timu bado ingaliko na kinyang’anyiro kingeendelea chini yake Raila Odinga. Sasa, iweje tena Kibaki asiwe ni mwenye kurejesha fadhila kuu aina hiyo!

Mbegu chungu ikapandwa na ikamea baina ya viongozi hao na wafuasi wao.

Miaka mitano ya utawala wake Kibaki ikawa ni yenye ugomvi baina yake na Raila Odinga kila mmoja wao akienziwa na wafuasi wake. Nchi ikawa haikaliki vema.

Isitoshe, mwaka wa 2005, Mwai Kibaki alipanga marekebisho ya katiba ya Kenya. Kama ilivyotarajiwa, Raila Odinga akaamua kupinga mabadiliko hayo-nembo yao katika kura ya maoni ikiwa chungwa.Rais Kibaki naye kaunga mkono mageuzi hayo nembo yao ikiwa ndizi.

Mwezi Novemba 2005, kura hiyo ya maoni ilipigwa ambapo upande wa Raila Odinga uliushinda upande wake Rais Kibaki. Mikoa 8 ilipinga, huku mkoa mmoja tu( mkoa wa kati ulio nyumbani kwa Kibaki na kabila lake la Wakikuyu) ukiunga mkono mageuzi hayo.

Kushindwa huku kulimtia doa kubwa Rais Kibaki, lilimshtua na kumtia hamaki. Naye akawafuta mawaziri wake wote waliokuwa wameipigia kura ya “La” akiwemo Raila Odinga.

Papo hapo Raila Odinga na wenzake wakaunda chama cha Orange Democratic Movement (ODM) amabacho kwacho aliwania Urais mwaka wa 2007.

Katika uchaguzi wa 2007, Mwai Kibaki wa Party of National Unity (PNU) alitangazwa kuwa mshindi kwa kupata kura 232,000 zaidi ya Raila Odinga wa ODM. Uchaguzi huo ulikumbwa na matatizo mengi ya kuhesabu kura na matatizo mengine kama vile usalama wa kura.

Raila Odinga alipinga matokeo hayo na akaitisha yeye atangazwe mshindi. Mwenyekiti wa tume ya Uchaguzi wakati huo, mwendazake Samuel Kivuitu, alipoulizwa na waandishi wa habari, alisema kwamba hakujua kwa hakika mshindi wa uchaguzi huo! Mwai Kibaki naye akaharakishiwa kula kiapo cha Urais akiwa katika salama ya Ikulu yake Nairobi masaa ya machweo. Kuapishwa huko kukawa kiberiti moto, na moto ukalipuka nchini.

Raila Odinga na viongozi wenzake wakampiga kamsa! Maandamano yakanoga takriban katika maeneo yote nchini. Zaidi ya wakenya elfu moja waliuwawa na mali ya thamani ya mabilioni ya pesa ikaharibiwa. Watu zaidi ya elfu mia mbili hamsini walikimbizwa makwao na kuifanya halaiki hiyo kuwa wakimbizi wa ndani kwa ndani.

Kwa kweli, laiti jamii ya kimataifa isingaliingilia ikiongozwa na marehemu Koffi Annan, taifa la Kenya lingalizama.

Sasa je, nia ya maandamano hayo ilikuwa nini?

Kwake Raila Odinga na viongozi wa mrengo wake, matokeo yaliyotangazwa yalikuwa ghushi na haramu.

Matokeo yake je? hasara kubwa kiuchumi, kijamii na hata kisiasa. Hadi leo, baadhi ya wakimbizi wa ndani kwa ndani mkoani Rift Valley hawajarejea manyumbani mwao na hawajarejeshewa mali zao zilizonyakuliwa wakati wa machafuko hayo.

Swala hili limekuwa donda dungu hadi wa leo.

Hata hivyo, mghalla muuwe, lakini haki yake mpe! Raila Odinga alifaulu hakufaulu?

Alifaulu! Tena pakubwa.

od

Kupitia miingilio kati ya jamii ya kimataifa, Mwai Kibaki alishurutishwa kugawana mamlaka ya serikali na Raila Odinga nusu bin nusu!...katikati.

Aidha, aliridhia kumpa wadhifa wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kenya. Ikumbukwe kwamba Mwai Kibaki kavunja mkataba wake na Raila mwaka wa 2002 ambao ungempa Raila wadhifa huo huo na mgao huo huo wa serikali. Kwa hivyo, walichonyimwa mwaka wa 2022 na Mwai Kibaki, kakipata mwaka wa 2007 kupitia maandamano! Kweli chembilecho wahenga, amani haiji ila kwa ncha ya upanga!

Faida ya pili: yaliwatia shime Mwai Kibaki na Raila Odinga kuketi pamoja na kuwelewana kuhusu vipengele tata vya katiba ya zamani na kuwezesha marekebisho mwafaka kufanyika mwaka wa 2010.Hofu ya jinamizi la mwaka wa 2007 liliwasukuma kuweka subira na salama katika mazungumzo yao, ndipo suluhu ya katiba ya mwaka wa 2010 ikapataikana. Wembe walioulilia mwaka wa 2007 ulikwisha wakata, wasije katwa tena!

Tatu: katiba ya mwaka wa 2010 imeleta mapinduzi makubwa kiuchumi, kijamii na kisiasa. Ugatuzi ni zawadi kubwa ilotujia kupitia katiba hii. Maendeleo makubwa kama vile ya miundo msingi, afya, elimu, kilimo, n.k yamepatikana kwayo.

Kwa ujumla, maandamano ya mwaka mwaka 2007 yasingalifanyika, Kenya tuitakayo hii, japo haijatimia asili mia, haingalipatikana.

Ingawa, matunda haya yamewezeshwa kwa ujasiri na uthabiti wa msimamo wake Raila Odinga pamoja na wanaharakati wenzake, wakiungwa mkono na wafuasi wao sugu.

Hivyo, si haki kupuzilia mbali maandamano kama njia moja, ya amani na kikatiba, kulazimishia utawala wa nchi kubadili mwendo na kuleta mageuzi ambayo yatanufaisha raia na kundeleza ukuaji wa nchi. Isitoshe, Katiba ya nchi ya Kenya inaruhusu maandamano ya raia kama njia mojawapo ya kupigania haki zao, ila, kwa kufanya hivyo, waandamanaji hao wasidhuru wala kuharamisha haki na uhuru wa wenzao.

Lakini mbona kila mara fujo na uharibifu wa mali hutokea?

Shida ya kwanza ni hulka nzima ya siasa za Kenya na mataifa ya Afrika kwa jumla. Japo katiba imeruhusu maandamano, viongozi

pande zote mbili hawajakolea katika maadili ya ustaarabu kisiasa kama vile Ulaya au hata Marekani, kwa mfano. Mathalan, serikali hutumia vikosi vya walinda usalama kuwazuia waandamanaji kwa misingi kwamba wataharibu na kupora mali za raia na hata kuwaumiza raia wenzao. Madai haya ya serikali yana na ukweli kwa kiasi fulani kwa sababau ndani ya wafuasi hao waandamanaji, majangili hujitosa humo na kutekeleza maovu yao kwa malengo yao ya jinai. Wala viongozi wenye kuandaa maandamano hayo hawana uwezo wa kuwatibua.

Matendo hayo mara nyingi, yanahujumu shughuli nzima ya maandamano ya amani.

Aidha, baadhi ya wanasiasa wa upinzani nao huwaliisha majangili hao hao au vijana fulani milungula kuzusha fujo ili serikali ihofie zaidi matokeo yake na ikubali makataa yao kwa haraka.

Kwa upande wa serikali, aghalabu hutumia nguvu kupita kiasi hata pasipo sababau mwafaka ya kutumia silaha hatari dhidi ya raia wake. Matokeo huwa ni vifo vya kuhuzunisha na uharibifu mkubwa wa mali na raslimali.

Kidole kimoja hakivunji chawa na vivyo hivyo, mara nyingi, wa kulaumiwa maandamano yanapozuka na madhara yanapotokea si Raila Odinga pekee, bali pia serikali.

Kwa hivyo, japo Raila Odinga amelaumiwa kwa machafuko ya baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2007, matunda ya katiba mpya ya 2010 na maraekebisho mazima ya miundo msingi ya uongozi Kenya yalifuatia. Baniani mbaya lakini kiatu chake dawa! Ikumbukwe pia kwamba Rais William Ruto wa leo alikuwa mhusika mkuu katika maandamano hayo!

Johan Kreigler kutoka Afrika alipoulizwa kuhakiki yaliyojiri katika uchaguzi huo, kauli yake ya mwisho ilikuwa kwamba ilikuwa vigumu kujua mshindi na mshindwa. Hivyo alaumiwe Raila au wenye kusimamia uchaguzi huo? Je, alaumiwe Rais Kibaki kwa namna alivyomsaliti Raila Odinga na kwa namna alivyoiendesha serikali yake ya mwaka wa 2002- namna ambayo ilipanda mbegu za chuki baina ya wanasiasa wenyewe nao wakawasha moto uliolipuka mwaka wa 2007?

Ibainike kwamba si wakati wote amezusha rabsha , huyu Bwana Odinga. Kwa mfano, mwaka wa 1997 alikubali kushindwa na Mzee Moi. Baadaye, alijiunga na huyo mpinzani wake (Rais Moi) ndani ya chama cha Jogoo akiwa na nembo yake ya “Tinga” ya chama chake cha NDP(National Democratic Party), tinga ikamezwa na Jogoo!

Katika uchaguzi wa mwaka wa 2013, aliposhindwa na Uhuru Kenyatta, alifuata na kutii katiba ya nchi kwa kupeleka kesi yake mahakamani. Mahakama ilipotupilia mbali kesi yake na kumtangza Uhuru Kenyatta mshindi, na japo aliteta kwamba Jaji Mkuu wakati huo, Daktari Willie Mutunga na wenzake walikataa ushahidi wake muhimu, hakuzusha rabsha. Mghalla muue lakini haki yake mpe!

Mwaka wa 2017 na mwana wa Jaramogi kashiriki uchaguzi wa Rais tena, kwa mara ya nne, akipeperusha bendera ya muungano wa CORD huku Kalonzo Musyoka akiwa mgombea wake mwenza. Katika uchaguzi huo, Uhuru Kenyatta alitangazwa mshindi.

Kwa mara ya tatu katika safari yake ya kuwania Urais, Raila Odinga alipiga kamsa akidai kura zake kuibiwa. Na punde akawasilisha kesi yake mahakamani. Mahakama hiyo ilikubaliana naye Raila

Odinga huku ikishikilia kwamba tume huru ya Uchaguzi Kenya (IEBC) ilikiuka katiba na sheria za uchaguzi katika kuandaa na kusimamia uchaguzi huo kukiwemo kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi huo. Mahakama hiyo ikaamrisha uchaguzi huo wa mwaka wa 2017 urejelewe upya katika mazingira muafaka.

Japo Raila Odinga na wenziwe walifurahia uamuzi huo, Raila alidinda kushiriki katika marudio ya uchaguzi huo kama ilvyoamrishwa na mahakama huku akidai kuwa miundo msingi ya IEBC iliyokashifiwa na mahakama ilikuwa ingalipo, na lazima marekebisho yafanywe kabla ya kurudi uchaguzini. Papo hapo uhuru Kenyatta na mgombea wake mwenza, William Ruto wakati huo, wakajitosa katika kampeni rejeshi. Uchaguzi uliandaliwa upya, japo idadi kubwa ya wapiga kura ilikataa kushiriki. Uhuru Kenyatta alitangazwa mshindi.

mm

Baadaye, huku akishikilia kuwa uchaguzi huo rejeshi bado ulikuwa haramu, Raila Odinga aliitisha maandamano makubwa. Isitoshe, aliitisha mkutano wa kutawazwa kwake kama “Rais wa Watu Wa Kenya” almaarufu “The Peoples’ President”. Kutawazwa huko kulizusha sintofahamu kubwa nchini. Fujo na maandamano yakatanda katika maeneo ya wafuasi wake Raila. Vifo na uharibifu vikaripotiwa. Raila akaagiza picha zote zake Rais Kenyatta ambazo kwa desturi, ziliangikwa kwenye kuta za maofisi za serikali na za kibinafsi zitolewe kutoka majumba na maofisi nchini kote. Alitenga na kutangazwa siku ya sherehe ya kuzitia moto picha hizo hadharani ili kuashiria kwamba yeye na wafuasi wake hawakuitambua serikali yake Kenyatta asilani.

Mambo yalianza kwenda sengemnege. Huku taswira za machafuko ya mwaka wa 2007 zikirejelewa mara kwa mara, Rais Kenyatta alimnyoshea mkono wa heri Raila Odinga, Machi 9 2018 wakafanya suluhu. Suluhu hiyo ikazalisha mchakato wa Building Bridges Initiative (BBI) kwa lengo la kurekebisha vipengele fulani vya katiba ya Kenya.

Baadaye, kupitia ukuruba huo mpya baina, Uhuru kaamua kumuunga Raila Odinga kumrithi yeye kama Rais. Yote tisa, la kumi ni kwamba Raila Odinga kabwagwa na William Ruto katika uchaguzi wa mwaka jana. Kama ilivyo ada yake Raila, kafikisha malalamiko yake mahakamani. Kesi yake haikufaulu wakati huu, huku mahakama ikimtangaza William Ruto mshindi wa uchaguzi wa mwaka wa 2022 .Japo alitangaza hakukubaliana na uamuzi huo, Raila alihakikishia taifa kwamba angeiheshimu amri hiyo ya mahakama.

Ghafla bimfuu, mwana huyo wa Jaramogi kazua utata. Amedai kwamba kidutu mtu fulani aliye katika IEBC kamfichulia siri kubwa ya namna ambavyo wizi wa kura ulivyofanyika.Kwa hivyo, sasa anataka uchunguzi wa kimataifa ufunguliwe kuhakiki kura hizo. Pili, makamishana wane waliojiuzulu kazi kutoka IEBC, almaarufu “the Cherera four” warejeshwe kazini. Tatu, serikali yake William Ruto isiwaajiri makamishna wapya bila kumshirikisha yeye na wadau wenzake. Nne, bei za bidhaa muhimu zishukishwe mara moja. Amekwishatoa makataa ya siku kumi na nne yatekelezwe matakwa hayo la sivyo aitishe maandamano ya kumng’oa Rais William Ruto mamlakani. Isitoshe, amekwisha tangazia taifa zima kuwa yeye na wafuasi wake hawatambui serikali yake William Ruto!

Je, wakati huu, ni faida gani atakoyoizua?

Je, ana haki kuitisha maandamano haya, hususan yale aliyoyapangia siku ya Jumatatu tarehe 20 Machi 2023 kwenda hadi Ikulu kung’atua Rais Ruto kutoka uongozini?

mm

Kwanza, hatua yake Raila Odinga ni kero na haramu kubwa dhidi ya katiba. Uchaguzi ulifanywa chini ya sheria na katiba ya Kenya. Yeye aliungwa mkono na Rais aliyekuwa mamlakani wakati huo. Pamoja naye, wakatumia asasi zo zote ziwazo zile, za kitaifa, kufanya kampeni. Kisheria, tume huru ya uchaguzi nchini (IEBC) ndiyo, pekee, iliyo na uwezo na ruhusa ya kumtangaza mshindi. IEBC ilimtangaza Dr. William Ruto kuwa mshindi.

Kwa kuiheshimu katiba, Raila Odinga alifikisha malalamishi yake mahakamani. Kikatiba, amri ya mahakama yenye upeo zaidi nchini ni sawia na amri ya mwenyezi Mungu-haina rufaa! Kwa hivyo, kwa kutangaza kwamba hamtambui William Ruto kama Rais, Raila Odinga ameharamisha amri ya mahakama na kuikaidi sheria za taifa. Kisheria hilo ni kosa la uhaini.

Isitoshe, Rais Kenyatta, kufuatia uchaguzi huo, kampishia Rais Ruto mamlaka ya kuongoza taifa, na alifanya hivyo kwa mujibu wa katiba ya taifa na kwa amani.

Chini ya katiba ya Kenya, njia ya kutawazwa au kuondolewa mamlakani rais awaye ye yote ni kupitia uchaguzi. Uchaguzi ulio mbele yetu sasa ni wa mwaka wa 2027.Kwa kutishia kumng’atua William Ruto kupitia njia ya maandamano ya wafuasi wake, Raila Odinga amekiuka katiba pakubwa.

Isitoshe, baada yake William Ruto kutawazwa, magavana, wakiwemo wa chama chake cha ODM, wabunge wa mabunge yote mawili ya kitaifa na waakilishi wa wodi (MCAs) walitawazwa kufuatia kukamilishwa na kutambuliwa kwa uchaguzi huu huu. Baadaye, vyama vya kisiasa, kikiwemo chake (ODM) viliteua waakilishi mbali mbali kujaza nafasi katika bunge la Afrika Mashariki. Baadhi ya wale walioteuliwa, na kuidhinishwa na huyu huyu Rais Ruto ni mwanawe Raila Odinga(Winnie Odinga) na wake Kalonzo Musyoka(Ken Musyoka).Iweje sasa kuchaguliwa kwake Rais Ruto kusiwe halali, lakini, wakati huo awe, ana halali ya kuwatawaza wana wao( na wengineo) kuwa wajumbe katika bunge la Afrika mashariki? Hii, kwa heshima kubwa, ni siasa fisadi na haramu.

Sababu mojawapo ya maandamano yake Raila Odinga mwaka huu ni bei za juu za bidhaa muhimu. La ajabu ni kwamba bei hizo hazikupanda wakati William Ruto alitawazwa. Uhuru Kenyatta alikuwa usukani zikipanda. Raila Odinga alikuwa na ukuruba mkubwa naye Uhuru zikipanda. Lakini inavyobainika sasa, kwa ajili ya ukuruba wake huo wa dhati na Uhuru Kenyatta, ilikuwa sawa hivyo. Maandamano dhidi yake hayakuitishwa wakati huo. Mbona hivyo?!

Mwaka wa 2018,kupitia ukuruba wake Raila na mwana wa Jomo, alitumia wingi wa wabunge wake wa ODM bungeni kumsaidia Uhuru Kenyatta kupitisha mswada( Finance Bill 2018) ambao ulipandisha bei ya mafuta kwa asili mia kumi na nane. Je, bei hizi zimepandishwa William Ruto alipotawazwa?

Hivi majuzi, msimamizi wa bajeti Daktari Nyakango’ amefichua kwamba utawala wake Uhuru Kenyatta ulimshurutisha kuidhinisha takriban shilingi billion kumi na tano ambazo zilinuiwa kulipa wasagaji unga nchini ili kushukisha bei ya unga. Wasagaji unga hao wameshasema hadharani kwamba senti hizo hazikuwafikia. Je, hilo si haramu?

Isitoshe, imefichuliwa kwamba shilingi bilioni sita zilitolewa kutoka mkoba wa serikali kununua hisa katika kampuni ya Telkom Kenya kwa niaba ya serikali ya Kenya. Wasimamizi wa Telkom Kenya wameshakana hadharani na kusema kwamba hizo senti hazikuwafikia.

Je, vitendo hivi havina dosari yo yote machoni mwa wapangaji wa maandamano haya?

Vitendo hivyo haviwadhuru raia kwa njia yo yote?

Kwa vyo vyote vile, kwa undani, haya maandamano si kwa manufaa ya raia moja kwa moja japo kwa nje yamevishwa joho la maslahi ya raia. Hivi ni vita vya kunyakua hadhi, nafasi zenye ushawishi na kukwepa kuajibika kufuatia baadhi ya matendo yaliyojiri katika siku za mwisho mwisho za utawala wake Uhuru Kenyatta. Vile vile, hivi ni vita vya kumdhibiti William Ruto, asidhubutu kuendeleza sera zake mpya za kuwatoza ushuru baadhi ya hawa mabwana ambao japo baadhi yao ni wakwasi kupindukia, wametumia nyadhifa zao kukwepa kulipa mgao wao wa ushuru. Ni vita vya kuhifadhi mifereji ya biashara zao mbali mbali nchini na ng’ambo ya nchi hii-biashara zisizo ndogo katu!

Kwa maono yangu, Azimio One Kenya Alliance, kwa kuungwa mkono na Rais Kenyatta, walikuwa na hakika kwamba wangembwaga William Ruto katika uchaguzi wa 2022.

Ushindi wake Ruto umewfyatukia machoni mwao mithili ya radi, hawakuuona hawakuutarajia, na sasa wamo katika heka heka za kutafuta uokozi wa nyota zao kisiasa.

La kukata ini ni kwamba Raila Odinga yungali na ufuasi sugu nchini. Yeye hunawiri sana wakati anapokinzana na serikali.

Kwake yeye, rabsha hizo ni kama kumtosa nyangumi baharini - ataibua mawimbi yasiyostahamilika! Naye Rais William Ruto ni kisigi cha hisia na mweledi wa maneno.

Hamna atakayemuachia mwingine suluhu! Fahali wawili watamenyana, nasi nyasi tutakanyagwa, tutaumia, tutalia na kusaga meno. Lakini mwishowe, watapata suluhu yao, wafalme hao, watasalia katika hadhi zao huku maisha yetu raia yakisalia pale pale, hata kudorora zaidi.

Kweli dunia mti mkavu!.