Mkutano wa AGRF:Mkutano unapoanza Tanzania wakulima watanufaika vipi?
Na Alfred Lasteck
BBC Dar es Salaam

Chanzo cha picha, UN
Mkutano Mkuu wa Mifumo ya Chakula ya Afrika (AGRF) 2023 unatarajiwa kuanza leo jijini Dar es Salaam nchini Tanzania ambapo utakutanisha maelfu ya washiriki wakiwemo viongozi wa serikali, wanasayansi, wawekezaji, watunga sera, wakulima na vijana kutoka mataifa zaidi ya 70.
Mkutano huo wa siku nne, utalenga zaidi kujadili mabadiliko ya mifumo ya chakula na kuhakikisha uhakika wa chakula kwa wote.
Rais wa Tanzania, Suluhu Hassan anatarajiwa kuongoza na kujadili na viongozi wa mataifa mbalimbali, wataalamu, wawekezaji, vijana na wengineo juu ya namna Afrika inaweza kuendeleza na kuja na njia mbadala ili kunufaika na kilimo cha chakula.
Lakini inaelezwa kuwa wengi wanajiuliza nani haswa ana lengwa na ni yupi atanufaika na maamuzi yatakayopatikana kwenye mkutano huo?
Mambo yanayotarajia kujadiliwa
Zaidi watoa mada 150 watazungumza ikiwa ni sehemu ya kuonesha changamoto na fursa katika sekta ya kilimo.
Aidha kutafuta suluhu ya changamoto zinazokabili mataifa ya Afrika katika upatikanaji wa chakula ikiwemo athari za mabadiliko ya tabia nchi, Wataalamu watashauri na pia kuangalia njia bora ya kunufaika na miradi endelevu ya kilimo.
Sambamba wadau mbalimbali watazungumzia ushirikishwaji wa vijana na wanawake kwenye maamuzi, utungaji wa sera, pamoja na kuvumbua bunifu mbalimbali zitakazochagiza uzalishaji wa chakula.
Mwenyeji Tanzania atanufaika vipi?

Chanzo cha picha, Wizara ya kilimo Tanzania /Twitter
Ikiwa na lengo la kuwa kitovu cha uhakika wa chakula kimataifa, Tanzania inayosifika kwa uzalishaji wa chakula katika eneo la Afrika Mashariki kuongeza ushirikiano na kukaribisha uwekezaji katika mlolongo wa thamani ya mifumo ya chakula.
Hivi karibuni, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema mkutano huo utakaokutanisha wadau kutoka mataifa mbalimbali utaipa Tanzania fursa ya kuwa kitovu cha uwekezaji cha kipekee barani Afrika.
Bashe alisema, “Katika mkutano wa AGRF, washiriki watakuwa na fursa muhimu ya kuona mafanikio na shughuli za wakulima wa Tanzania, wakipata ufahamu muhimu juu ya mazoea mazuri ndani ya sekta ya kilimo na kuwavuta wawekezaji nchini.”
Mataifa mengine Afrika yatanuika vipi?
Kwa mujibu AGRF, hakuna nchi itakayoachwa nyuma kwenye mapinduzi ya chakula na kwamba ushirikishwaji kwenye kila eneo unayapa mataifa yote wanachama nafasi ya kukuza sekta za kilimo na uboreshaji wa chakula.
Usawa kijinsia na ukombozi kwa wanawake wazalishaji chakula

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ripoti ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) ya mwaka 2023 inaonesha kuwa kuna ukosefu wa usawa wa kijinsia katika mifumo ya chakula cha kilimo na athari zake katika uzalishaji na uboreshaji mifumo ya chakula.
Dorine Odongo, Mwandamizi wa Taasisi ya Watafiti Wanawake katika Kilimo (AWARD) ameeleza umuhimu wa kujadili jinsi ya kuimarisha juhudi za kufikia usawa wa kijinsia katika kilimo na mifumo ya chakula.
Dorine alisema kuwa ni lazima wanawake wanawake wawe sehemu ya maamuzi ya juu katika sekta ya kilimo ikiwa ni kuongoza na kusimamia utungaji sera za kilimo na chakula.
"Ili kuunda sera na programu kwa kuzingatia jinsia, ni muhimu kujumuisha mitazamo na uzoefu wa wanawake katika michakato ya kufanya maamuzi," alisema mtaalamu huyo.
Kwa upande wake Dina Esposito, Ofisa katika Ofisi ya Ustahimilivu na Usalama wa chakula wa Shirika la USAID alisema, "wanawake katika kilimo wanapofaulu, sote tunafaulu."
Dina alitolea mfano, katika nchi za kipato cha chini na cha kati, mashamba yanayosimamiwa na wanawake kwa wastani wa asilimia 24 chini ya uzalishaji kuliko yale ya wenzao wa kiume - idadi ambayo kimsingi imebakia bila kubadilika kwa miaka 10.
"Sera na kanuni zinaweza kusaidia au kuumiza maendeleo kwa wanawake. Zinaweza kufungua fursa kwa wanawake kumiliki ardhi au, kudhoofisha haki zao. Zinaweza kukuza upatikanaji wa fedha kwa wanawake au, kuwaporomosha. Mapengo haya ya ubaguzi wa kijinsia katika sera na katika utekelezaji wa sera yanahitaji kuvunjwa. Hivyo wanawake wana jukumu muhimu la kutekeleza kazi hii na kwa kuanzia mkutano huu," alisema.

Chanzo cha picha, Wizara ya kilimimo Tanzania/Twitter
Je mkulima atanufaika vipi?
Gideon Baraka wa Arusha Tanzania, ameiambia BBC kuwa mkutano huo ukiwa na tija basi hao kama wakulima wadogo wangependa kuona unafuu katika uzalishaji wa chakula kuanzia upatikanaji wa mbegu bora, mbolea iliyo nafuu lakini soko la uhakika la chakula.
Mike Mkombwe wa Zambia, anasema ili mjadala uwe na tija basi kinachajadiliwa kilengo uongezaji thamani wa chakula ili kulinasua bara la afrika katika biashara isiyokuwa na tija ya vyakula.
Wataalamu wa masoko ya kilimo wanasema kuwa Afrika uzalisha chakula kingi lakini uongezaji dhamani ni mdogo hivyo kipato wanachokipata si stahiki.
Mtafiti nchini Tanzania, Dkt Linda Salekwa anasema,”Tunazalisha sana ila ubora unatengenezwa nje ya bara, hivyo tunapoteza fedha nyingi kwenye mnyororo wa thamani. Kama ipo hivyo basi mkutano huu utueleze njia bora za kuboresha biashara ya chakula ili wakuliwa wazalishe kwa wingi na kuongeza kipato.”















