Jinsi Wasomali watakavyoathirika kutokana na shutuma za Rais Trump

Muda wa kusoma: Dakika 5

Rais Donald Trump amekuwa akishambulia mara kwa mara Wasomali na nchi yao (Somalia) kwa maneno makali, jambo ambalo limezua taarifa nyingi zisizo sahihi dhidi ya Wasomali.

Alipokuwa katika kampeni za uchaguzi wa urais za muhula wa Kwanza Septemba 2016, Trump alishambulia jamii ya Wasomali wanaoishi katika jimbo la Minnesota nchini Marekani ,akiwalaumu kwa kueneza maoni yenye itikadi kali nchini humo.

"Viongozi wetu wana ujinga kiasi gani? Kuruhusu mambo kama haya kutokea? Hapa Minnesota mmekabiliwa na matatizo chungu nzima kutokana na ukaguzi mbovu wa wakimbizi, huku idadi kubwa ya Wasomali wakiingia katika jimbo hili bila wakaazi kufahamishwa, bila usaidizi wenu ama hata ruhusa''..alisema haya alipokuwa akiwania urais wa Marekani.

Tamko la hivi punde la Rais wa Marekani Donald Trump ni kuwa hataki wahamiaji wa Kisomali nchini Marekani, na kuwaambia waandishi wa habari wanapaswa "kurejea walikotoka."

"Siwataki katika nchi yetu, nitakuwa mkweli," amesema wakati wa mkutano wa baraza la mawaziri siku ya Jumanne. Trump amesema Marekani "itaharibika ikiwa tutaendelea kuchukua takataka katika nchi yetu."

"Nchi yao ya Somalia unajua hawana chochote. Wanakimbia huku na huko kuuana," Trump alisema.

Kisha akageukia kumkosoa Mbunge Ilhan Omar, wa chama cha Democratic, ambaye ni Mmarekani mwenye asili ya Somalia, ambaye amekuwa akigombana naye mara kwa mara.

"Siku zote huwa namtazama," Trump alisema, akiongeza kuwa Omar "anamchukia kila mtu. Na nadhani ni mtu asiye na uwezo."

"Kuniandama kwake kunatisha," Ilhan Omar alisema katika chapisho katika mtandao wa kijamii. "Natumai atapata msaada anaohitaji."

Maoni yake ya kudhalilisha yanakuja wakati maafisa wa uhamiaji wakiripotiwa kupanga operesheni katika jamii kubwa ya Wasomali ya Minnesota.

Maafisa katika jimbo hilo wamekosoa mpango huo, wakisema unaweza kuwaondoa isivyo haki raia wa Marekani ambao wanatoka katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

Minneapolis na St Paul, ambazo kwa pamoja zinajulikana kama Twin Cities, ni nyumbani kwa mojawapo ya jumuiya kubwa zaidi za Wasomali duniani na kubwa zaidi nchini Marekani.

Lakini linaathari gani kwa Jamii ya Wasomali?

Minnesota ndiyo jimbo lenye idadi kubwa ya Wasomali nchini Marekani, ambapo takribani Wasomali 87,000 wanaishi.

Wengi wao hutuma fedha nyumbani, jambo ambalo lina mchango mkubwa katika uchumi wa Somalia.

Hata hivyo, baadhi ya fedha zinazokusanywa Minnesota zinasemekana kutumika dhidi ya Wasomali, zikielekezwa kwa makundi ya kigaidi kama Al-Shabaab.

Hii imesababisha Idara ya Hazina ya Marekani, kupitia mtandao wake wa kufuatilia uhalifu wa kifedha (FinCEN), kutoa onyo juu ya uwezekano wa mfumo wa kifedha wa Marekani kutumika vibaya na wahalifu.

Tangu mwaka 2015, serikali ya Marekani imesema fedha zinazotumwa Somalia zinaweza kujipata mikononi mwa wanamgambo kama Al-Shabaab na sasa inachukua hatua kuziba pengo ambalo linatumika na wahalifu.

Dkt. Shafi Sharif Mohamed, mtafiti wa Mogadishu, ameiambia BBC Somalia, kauli za mara kwa mara za Rais Trump zinaathiri Wasomali kwa namna moja au nyingine.

"Marekani wanaleta athari kubwa kiuchumi kwa nchi ya Somalia kwa sababu wanaipa serikali ruzuku... wamekuwa na athari kubwa kwetu kiuchumi, kijamii na kisiasa."

Alibainisha kwamba ikiwa hali hii itaendelea, itapunguza fedha zinazotumwa Somalia, na kuongeza shinikizo kwa Wasomali wanaoishi Marekani wanaotuma fedha kwa familia zao.

Uchunguzi wa fedha za Marekani kufadhili Al- shabaab

Wakati huo huo, Idara ya Hazina ya Marekani inachunguza madai kwamba fedha za kodi zilizokusanywa Minnesota zilitumika kuunga mkono Al-Shabaab.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X, Katibu wa Hazina, Scott Bessent, ameeleza kuwa uchunguzi huu unafanyika kufuatia kauli za Rais Trump kumtaja Gavana wa Minnesota, Tim Walz, na jimbo lake kama "kitovu cha fedha zilizoporwa na udanganyifu."

Ripoti za wabunge wa Republican zilizoshiriki madai haya hazijathibitishwa, lakini zimeibua mjadala kuhusu jinsi baadhi ya fedha zinazokusanywa Marekani zinavyoweza kuathiri usalama wa Somalia.

Bessent amesisitiza kwamba uchunguzi unalenga utawala mbaya na uwezekano wa upotevu wa kodi za raia wa Minnesota kwenda kwa makundi ya kigaidi nchini Somalia.

"Kama nilivyoelekeza, Idara ya Hazina inachunguza madai ya usimamizi mbovu usioisha wa utawala wa Biden na Gavana Tim Walz ambao umesababisha kukengeushwa kwa ushuru wa watu wa Minnesota wanaofanya kazi kwa bidii kwa shirika la kigaidi la Al-Shabaab," Bessent alisema.

Ofisi ya Walz haikujibu mara moja ombi la maoni kutoka kwa shirika la Reuters. Hapo awali gavana huyo alisema utawala wa Trump unakashifu na kutishia jamii nzima ya Wasomali.

Katika mahojiano yaliyorushwa na NBC News siku ya Jumapili ya Novemba 31, Walz aliulizwa kuhusu madai ya Trump na raia kutoka Afrika Mashariki waliopatikana na hatia ya wizi wa fedha ambao wanashtakiwa katika kesi zinazohusiana na wizi wa programu ya Covid. Walz alisema kuna watu ambao wamehukumiwa.

"Inafaa kufahamu kwamba sio Wasomali pekee. Minnesota ni jimbo lenye ustawi... lakini kuna wahalifu wengi wanaokuja. Na watafungwa," Walz alisema, na kuongeza, "Kuaibisha jumuiya nzima kwa jambo ambalo walifanya kwa njia ndogo ni dhaifu."

Somalia ni mojawapo ya mataifa maskini zaidi duniani, na wengi wa wahamiaji waliohamia Marekani waliondoka katika miaka ya 1990 wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miongo kadhaa nchini humo.

Je, hali ikoje kwa Wasomali wanaoishi Marekani baada ya hotuba ya Trump?

Wasomali wanaoishi Minnesota sasa wanakabiliwa na hofu baada ya Rais Trump kuwataja kama watu ambao hawakaribishwi nchini Marekani.

Idara ya Uhamiaji ya Marekani (ICE) imeagizwa na utawala wa Trump kuwalenga wahamiaji wa Kisomali wasio na vibali katika Twin Cities, mtu anayefahamu mipango hiyo ameliambia shirika la habari la CBS News siku ya Jumanne.

Wasomali sasa inaripotiwa kuwa wanalengwa mitaani, sehemu za kazi, na katika vituo vya afya, na wanaulizwa maswali kuhusiana na kukaa kwao nchini humo.

Hii imezua hofu kubwa, kwani shughuli za biashara zimeanza kuathirika katika jimbo hilohuku wengine wakiamua kubaki nyumbani.

Viongozi wa eneo la Minnesota wamelaani mpango ulioripotiwa wa utawala wa Trump.

Seneta wa jimbo la Minnesota Zaynab Mohamed alisema kwenye X kwamba "wakati mawakala wa ICE wanapowasiliana na Wasomali hapa, watapata kile ambacho tumekuwa tukisema kwa miaka mingi: Karibu sisi sote ni raia wa Marekani".

Hatma ya Wasomali wanaoishi Marekani

Mwezi uliopita, Trump alisema atakomesha mfumo unaowalinda Wasomali wanaoishi Minnesota dhidi ya kufukuzwa, akisema "magenge ya Kisomali yanayowasumbua na kutia hofu" watu katika jimbo hilo.

Hatua hii ilisababisha kusitishwa kwa programu inayofahamika kama (TPS) iliyoanza mwaka 1991, wakati nchi hiyo ilipotawaliwa na Chama hicho cha Republican.

Utawala wa Trump, ambao ulimtangulia Rais Joe Biden, uliongeza muda wa kutowafurusha wasomali nchini humo hadi Machi 17, 2026.

Kwa sasa, Wasomali 705 wanaopata ulinzi kupitia mpango wa TPS wanakabiliwa na hatma hiyo mpya. Hii inawaathiri moja kwa moja raia wa Marekani wa asili ya Somalia, ambao wengi wao hutuma fedha nyumbani na kuungia uchumi wa taifa lao.

Utawala wa Trump umezidisha msako kwa wahamiaji kufuatia kupigwa risasi kwa wanajeshi wawili wa Jeshi la Kitaifa huko Washington DC wiki iliyopita, Sarah Beckstrom, 20, aliyefariki na kumjeruhi vibaya Andrew Wolfe, 24.

Mshukiwa, ambaye amekamatwa na kushtakiwa kwa mauaji, anatoka Afghanistan.