Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Operesheni Mogadishu: Jinsi Marekani ilivyolazimika kuikimbia Somalia na askari waliovuja damu kwenye malori
Jeshi la Marekani linajulikana kwa nguvu zake kubwa. Hata hivyo, katika nchi maskini sana na iliyo nyuma kama Somalia, jeshi lile lile la Marekani lilikuwa katika hali mbaya.
Marekani ilikuwa na aibu ya kuwaondoa wanajeshi wake katika operesheni ya kijeshi iliyoshindwa ya 'Operesheni Mogadishu'. Nakala hii inaelezea kile kilichotokea katika operesheni hii.
Ukitazama historia ya hivi karibuni ya Somalia, utaona njaa, madikteta katili, makundi yanayopigana, na machafuko.
Katika miaka ya 80, kulikuwa na njaa mbaya nchini Somalia. Athari yake ilikuwa kubwa kiasi kwamba iliharibu kabisa miundombinu nchini Somalia.
Mnamo 1992, baadhi ya wanajeshi kutoka Idara ya Kwanza ya kikosi cha majini cha Marekani na Kikosi Maalumu walitumwa Somalia kufanya kazi ya kutoa msaada.
Hakukuwa na serikali nchini Somalia wakati huo. Kulikuwa na mapambano ya kugombea madaraka kati ya viongozi wa magenge mawili huko.
Mnamo Juni 5, 1993, wakati wa ukaguzi wa kawaida wa silaha, waasi watiifu kwa Mohammad Farah Aidid waliwavizia na kuwaua askari 24 wa Pakistani.
Kampeni ya kuwakamata wafuasi wa Aidid
Kwa kuzingatia tukio hili, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio. Kwa hiyo, amri ilitolewa kumkamata Aidid na wanachama wake wa Muungano wa Kitaifa wa Somalia.
Matt Eversman na Dan Schilling wameandika kitabu 'Battle of Mogadishu'. Ndani yake, anaandika, "Kwa maelekezo ya Wakuu wa Marekani, Kamandi Maalum ya Operesheni ya Marekani iliunda kikosi maalum cha kumkamata Aidid."
Mnamo Agosti 26, 1993, kikosi cha wanajeshi wa Marekani- wanajeshi wa majini, na wanajeshi wa anga walifika kwenye katika uwanja wa ndege wa Mogadishu. Mogadishu ni mji mkuu wa Somalia.
Wiki tano baadaye, siku ya Jumapili alasiri, askari hawa walianza Operesheni 'Gothic Serpent'. Hii ilikuwa operesheni yake ya saba na ya mwisho.
Kufikia wakati huo, waasi wa Somalia walikuwa wamepata uzoefu mkubwa wa vita kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka kumi. Wakazi wa mji wa Mogadishu walikuwa zaidi ya milioni moja.
Wengi wa watu hawa walikuwa na silaha.
Mnamo Oktoba 3, 1993, askari wa Marekani walipata taarifa kwamba waasi wawili wa Kisomali karibu na Aidid walikuwa wakikutana katika jengo karibu na Hoteli ya Olympic.
Kikosi cha Kimarekani ndipo kiliamua kushambulia jengo hilo na kuwakamata watu hawa. Mahali hapa palikuwa katika soko la Bakara, katikati mwa jiji la Mogadishu.
Eversman alikuwa katika kikosi cha wanajeshi wa Marekani. Anaandika, "Tulipaswa kushambulia jengo huko Mogadishu. Helikopta yetu ilipaa hadi kufikia lengo saa tisa na dakika 32 alfajiri. Ingechukua dakika 3 tu kufikia lengo letu."
"Hili lilikuwa eneo lenye watu wengi. Kulikuwa na wafuasi wa Aidid kila upande. Tulipanga kukamilisha operesheni hii katika muda wa nusu saa. Hata hivyo, operesheni hii ya kuwashambulia wafuasi wa Aidid iligeuka na kuwa operesheni ya uokoaji baada ya helikopta kuanguka."
"Mara tu tulipoondoka, rubani wetu alituambia kuwa Wasomali walikuwa wakichoma matairi barabarani. Wengine waliamini kwamba kwa kuchoma matairi, waasi wa Somalia walikuwa wakiwatahadharisha watu wao kuhusu mashambulizi yetu. Ilikuwa ni lugha yao ya siri."
"Baadhi ya watu walidhani kwamba kwa kuchoma matairi walikuwa wakizuia njia ya askari wa Marekani."
Wingu kubwa la vumbi lilipandishwa angani na helikopta hiyo.
Operesheni hiyo ilihusisha helikopta 12 za Black Hawk na karibu wanajeshi 100 wa Marekani.
Kila helikopta ilikuwa na askari wanne. Askari hao walikuwa wamevalia makoti meusi ya kuzuia risasi. Walikuwa na kipaza sauti cha kuzunguka, walikuwa wakiwasiliana kila mara.
Mara baada ya helikopta kufika kwenye makazi ya watu wengi, watu na magari ya chini yalianza kutawanyika.
Baadhi ya watu waliokuwa wamesimama chini walikuwa wakielekea juu. Ni kana kwamba walikuwa wakimpa changamoto ya kushusha helikopta na kupigana.
Mark Bowden ameandika kitabu 'Black Hawk Down: A Story of Modern War'.
Ndani yake, anaandika, "Helikopta mbili za kwanza zilitua kusini mwa jengo lililolengwa. Helikopta hizi zilipotua, vumbi jingi lilianza kutimka hivi kwamba marubani na askari waliokuwa kwenye helikopta nyingine hawakuweza kuona kitu chochote cha chini."
"Helikopta ya kwanza ilitua pale ambapo helikopta ya pili ilitakiwa kutua. Helikopta ya pili ilipaa tena na kutua mbele ya jengo lililolengwa. Hili halikuwa eneo ambalo awali lilitengwa kwa ajili ya kutua."
Askari mmoja alianguka kutoka kwa helikopta.
Ajali ilitokea mara tu wanajeshi wa Marekani waliposhuka kwenye helikopta. Mwanajeshi alianguka chini kutoka urefu wa futi 70 kutoka kwa helikopta ya Todd Blackburn angani.
Matt Eversman anaandika kuhusu tukio hilo, "Nilipoanza kushuka, nilianza kutazama tumbo la helikopta. Hata nikiwa nimevaa glovu, kamba ya nailoni ilikuwa ikichoma mikono yangu."
"Nilitazama pande zote ili nione jinsi nilivyopaswa kwenda chini. Nilitazama chini na moyo wangu ukaruka mapigo. Kulikuwa na mwili uliovunjika ukiwa umelala chini."
"Wazo la kwanza lililonijia wakati huo ni kwamba kuna mtu amepigwa risasi. Je, amekufa? Nilipotua chini, mguu wangu ulikaribia kugusa mwili wake."
"Madaktari walianza kumhudumia. Damu zilikuwa zikimtoka puani, masikioni na mdomoni. Alikuwa amepoteza fahamu."
"Wakati nikishuka kutoka kwenye helikopta, kamba ilikuwa imetoka mkononi mwake na alikuwa ameanguka futi 70. Nilitazama huku na huku ili kuangalia wenzangu wengine. Hapo ndipo nilipogundua kuwa tunapigwa risasi."
Kufariki kwa mwanajeshi wa Marekani aliyepigwa risasi
Wakati ufyatuaji risasi ulipoanza, risasi za waasi wa Somalia hazikuwalenga walengwa. Lakini baadaye waliwalenga wahusika.
Gari lililotelekezwa lilikuwa limeegeshwa katikati ya barabara. Waasi wa Somalia walikuwa wakichukua fursa hiyo na kuwafyatulia risasi wanajeshi wa Marekani.
Walikimbia kutoka upande mmoja wa jengo kuelekea kwenye gari. Wangeweza liweza kujificha upande mwingine wa barabara.
Wakati huo huo, helikopta za Black Hawk pia zilianza kuwafyatulia waasi wa Somalia risasi kutoka juu. Hata hivyo, pamoja na hayo, wanajeshi wa Marekani walifanikiwa kuwakamata washukiwa wa uasi huo 19 -waasi wa Kisomali.
Matt Eversman anaandika, "Mlio wa risasi za bunduki ulikuwa mkubwa sana kiasi kwamba ulifanya meno yangu kugongana. Wakati huohuo, sajenti wetu mmoja, Cassie Joyce, alipigwa risasi."
"Ni kweli alikuwa amevaa fulana ya Kevlar ya kuzuia kupenya kwa risasi mwilini. Lakini risasi ilikuwa imeingia mwilini mwake kutoka eneo la karibu na kwapa ambalo halikufunikwa na fulana. Jeraha lake lilikuwa dogo sana kiasi kwamba nilikaribia kulipuuza."
"Ilionekana kana kwamba hakuwa na maumivu hata kidogo. Hakujiweza hata kidogo. Alikuwa akinitazama tu. Lakini baada ya daktari wetu kumchunguza, mara moja alisema kwamba mwili wa sajenti unapaswa kuwekwa kwenye lori."
"Hapo ndipo nilipogundua kuwa mmoja wa washiriki wa timu yangu alikuwa amekufa."
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi