Ethiopia yaonya dhidi ya uvamizi huku kukiwa na mvutano wa kikanda

    • Author, Farouk Chothia
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 3

Waziri Mkuu wa Ethiopia ameonya kwamba yeyote anayepanga kuivamia nchi yake anapaswa "kufikiri mara 10" kabla ya kufanya hivyo kwa sababu, shambulio lolote litajibiwa.

Abiy Ahmed hakutaja taifa lolote katika maoni hayo, lakini yanakuja wakati ambao kuna ongezeko la mvutano na nchi jirani za Somalia na Misri.

Somalia imeelezea mapatano juu ya bahari ambayo serikali ya Abiy ilitia saini na jamhuri iliyojitangazia uhuru ya Somaliland mwezi Januari kama kitendo cha "uchokozi", na imejibu kwa kuunda uhusiano wa karibu wa kijeshi na Misri.

Somaliland ilijitenga na Somalia zaidi ya miaka 30 iliyopita, lakini Mogadishu inaiona kuwa ni sehemu ya ardhi yake.

Misri imekuwa katika mzozo wa muda mrefu na Ethiopia kuhusu uamuzi wa Addis Ababa wa kujenga bwawa kubwa kwenye Mto Nile.

Inaripotiwa kuwa Misri inapanga kutuma wanajeshi wake nchini Somalia kufuatia kusainiwa kwa mkataba wa kijeshi kati ya serikali hizo mbili mwezi uliopita.

Katika hotuba ya televisheni kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Ethiopia, Abiy alisema taifa hilo la Afrika mashariki halina nia ya kuanzisha migogoro.

Hata hivyo, alisema "walio mbali na walio karibu" wanapaswa kujua kwamba "kwa kawaida huwa tunawa fedhehesha na kuwafukuza wale wanaojaribu kutuvamia.”

"Yeyote anayenuia kuivamia Ethiopia anapaswa kufikiria sio mara moja tu bali mara 10 kwa sababu jambo moja kuu ambalo sisi Waethiopia tunalijua ni jinsi ya kujilinda," alisema Abiy.

Pia unaweza kusoma

Chanzo cha mvutano

Somalia imekasirishwa na uamuzi wa Ethiopia ambayo haina bahari, kuingia makubaliano na Somaliland ili kuweza kutumia bandari.

Somaliland pia imesema inaweza kukodisha sehemu ya pwani yake kwa jeshi la wanamaji la Ethiopia, ili serikali ya Abiy kuwa ya kwanza kuitambua kama taifa huru.

Mvutano katika eneo hilo uliongezeka mwezi uliopita baada ya ndege mbili za jeshi za Misri aina ya C-130, kuwasili katika mji mkuu wa Somalia kuashiria kuimarika kwa uhusiano.

Misri inaripotiwa itatuma hadi wanajeshi 5,000 kujiunga na kikosi chenye sura mpya cha Umoja wa Afrika (AU) nchini Somalia mwishoni mwa mwaka huu, na wengine 5,000 wakitumwa na nchi zingine.

Kikosi cha AU kimekuwa nchini Somalia tangu 2007 kusaidia serikali kupambana na al-Shabab, kundi la wanajihadi linaloendesha uasi wa kikatili nchini humo.

Wanajeshi wa Ethiopia ni sehemu ya kikosi hicho, lakini Somalia imetangaza kuwa wanapaswa kuondoka mwaka ujao.

Kwa upande wake, Misri imeishutumu Ethiopia kwa kutatiza utiririkaji wa maji ya Mto Nile kufuatia kuanzisha ujenzi wa Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance (Gerd) katika nyanda za juu za Ethiopia, ambako asilimia 85 ya maji ya Mto Nile hutoka.

Gerd ni mradi mkubwa zaidi wa bwawa la kuzalisha umeme barani Afrika, na Ethiopia inauona kuwa muhimu kukidhi mahitaji yake ya nishati.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah