Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kila kitu unachohitaji kujua kuhusu mzozo kati ya Ethiopia na Somalia
Serikali ya Somalia imerejesha nyumbani balozi wa Ethiopia nchini humo na kuamuru kufungwa kwa ofisi mbili za balozi ndogo kwenye majimbo ya Somaliland na Puntland. Hatua hii imesemekana kuchochewa na mvutano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili jirani katika eneo la Pembe ya Afrika.
Mogadishu pia imemrejesha nyumbani balozi wake kutoka mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, kwa "mashauriano ya kina" baada ya kuishutumu Ethiopia kwa kuingilia "mambo ya ndani ya Somalia."
Ethiopia hapo awali ilikanusha madai ya kuvuka mipaka na vile vile shutuma za kukiuka mamlaka ya Somalia , lakini hadi sasa bado haijatoa tamko lolote kuhusianana hatua za hivi punde.
Ni nini chanzo cha mzozo huo?
Mvutano kati ya nchi hizo mbili ulipamba moto wakati Ethiopia – taifa ambalo halipakani na bahari - ilipotia saini mkataba wa matumizi ya bandari ya Berbera iliyopo mjini Hargeisa, Somaliland. Jimbo hilo la Somalia, lilitangaza kujitenga na taifa hilo mnamo 1991, japo hadi sasa halijatambuliwa kuwa taifa huru na Umoja wa mataifa.
Kulingana na mpango huo kati ya Somaliland na Ethiopia - ambao Somalia inasema haina misingi kisheria - unaonekana kama taarifa ya dhamira ya kutengeneza njia ya mkataba wa siku zijazo, Ethiopia inaweza kukodisha ukanda wa pwani wa kilomita 20 (maili 12) kujenga kituo cha jeshi la majini.
Hili liliighadhabisha serikali ya Mogadishu ambayo inachukulia Somaliland kuwa sehemu ya eneo lake. Ilielezea mpango huo kama kitendo cha uchokozi.
Wakati huo, maafisa wa Somaliland walisema Ethiopia, kwa upande wake, itakuwa nchi ya kwanza duniani kuwatambuwa kama taifa huru.
Somaliland ilijitenga na Somalia zaidi ya miaka 30 iliyopita, lakini uhuru wake hautambuliwi na Umoja wa Afrika (AU) wala Umoja wa Mataifa (UN).
Mamlaka nchini Ethiopia hazijakiri hadharani kwamba zitaitambua Somaliland kama taifa huru. Badala yake, walisema wangetoa hisa katika makampuni yenye faida kubwa kama vile shirika la ndege la Ethiopia.
Je, kumekuwa na jitihada za kupunguza mvutano?
Kutokana na makubaliano hayo, Ethiopia ilishutumiwa vikali kimataifa kimataifa huku AU na nchi kadhaa za magharibi ikiwa ni pamoja na Marekani zikitaka uadilifu wa eneo la Somalia uheshimiwe.
Katika jitihada za kupata uungwaji mkono wa kikanda Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud alizindua kampeni ya kidiplomasia na kusafiri hadi Eritrea na Misri - nchi mbili ambazo pia hazina uhusiano mzuri na Ethiopia.
Alipoingia madarakani, Waziri Mkuu Abiy Ahmed aliweka juhudi za kufungua upya uhusiano kati ya Ethiopia na Eritrea, na hata kufanikisha kufunguliwa mpaka kati ya mataifa hayo mawili.
Kuhusu Somalia, kumekuwa na juhudi za kidiplomasia nyuma ya pazia ili kupunguza mvutano lakini matakwa ya Somalia ya kubatilisha mpango huo hadharani bado hayajatimizwa.
Kwa nini Ethiopia inahitaji ufikiaji wa bahari?
Ikiwa na idadi ya watu wapatao milioni 120, Ethiopia ndiyo nchi yenye watu wengi zaidi isiyo na bahari.
Zaidi ya 90% ya biashara yake ya kimataifa inafanywa kupitia taifa jirani la Djibouti. Maafisa mjini Addis Ababa wanaona hili kama haliwezekani.
Kabla ya mkataba wa Somaliland kutiwa saini, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alisema upatikanaji wa bahari ni suala "lililopo" kwa nchi yake. Matamshi yake kwamba Ethiopia ingetafuta njia za amani kupata ufikiaji wa bandari lakini "kama hilo litashindikana, tutatumia nguvu" yalizua mvutano katika eneo hilo.
Ethiopia pia ina azma ya kujenga kikosi cha wanamaji - licha ya kutokuwa karibu na bahari . Mnamo mwaka wa 2018 Abiy alisema Addis Ababa inapaswa kuunda kikosi cha wanamaji sambamba na vikosi vyake vya anga na ardhini.
Hatua hizi za hivi punde ni muhimu kiasi gani?
Kurejeshwa nyumbani kwa wanadiplomasia wa Ethiopia na Somalia kunaashiria kudorora kwa mambo katika uhusiano wa kidiplomasia ya mataifa husika.
Hatua hiyo ilitangazwa siku moja baada ya Addis Ababa kuwakaribisha maafisa kutoka Puntland – Jimbo la Somalia linaojitawala.
Somalia ina mfumo wa uongozi wa majimbo huru yaani FEDERAL GOVERNMENT, huku ikiwa na majimbo sita yenye uhuru wa kiwango Fulani ambayo yote yana viongozi wake ila yote sita yanapaswa kuwa chini ya serikali kuu ya Mogadishu.
Jimbo la Puntland hivi karibuni limezozana na serikali kuu ya Somalia kuhusu mageuzi ya katiba.
Mwishoni mwa Mwezi wa Machi bunge la Somalia lilipitisha marekebisho ya katiba ambayo ni pamoja na kuanzishwa kwa uchaguzi wa moja kwa moja wa rais na kuidhinishwa kwa rais kumchagua waziri mkuu.
Hata hivyo, jimbo la kaskazini-mashariki la Puntland lilikataa hatua hiyo. Puntland, ambayo imekuwa na hadhi ya kujitawala kwa kiwango fulani tangu mwishoni mwa miaka ya 1990, ilisema itajiondoa kutoka kwa mfumo wa shirikisho na kujitawala yenyewe hadi kura ya maoni ya kitaifa itakapofanyika. Safari ya wajumbe wa Puntland kwenda Addis Ababa kutokana na mgawanyiko huu haikupokelewa vyema mjini Mogadishu.
Haijabainika ikiwa Ethiopia itachukua harua gani kulipiza kisasi ikiwa itaamua kufanya hivyo. Lakini hakuna matarajio ya mgogoro huo kufikia hatua ya vita.
Hata hivyo, kuzorota kwa mahusiano kunaweza kuathiri kampeni dhidi ya wanamgambo wa Kiislamu katika Pembe ya Afrika.
Tayari kuna wasiwasi kwamba kundi la Al-Shabaab lenye mafungamano na Al-Qaeda linaweza kutumia mivutano inayoendelea kuwaajiri wapiganaji na kuongeza vitisho vya usalama.
Ethiopia pia ni mojawapo ya nchi zinazochangia wanajeshi kwa ajili ya kikosi cha kulinda amani kinaoongozwa na Umoja wa Afrika nchini Somalia {ATMIS }.
Kulingana na mpangilio wa majukumu ya kikosi hicho, kwa sababu kilibuniwa kuhudumu kwa muda wa miaka mwili kinatarajiwa kujiondoa nchini humo mwishoni mwa mwaka huu, na kukabidhi majukumu ya usalama kwa serikali ya Somalia.
Kwa sasa takriban wanajeshi elfu nne na maafisa wa polisi elfu moja waliohudumu kwenye kikosi hicho wameshaondoka Somalia.
Lakini mvutano kati ya Somalia na majirani zake muhimu zaidi unaweza kuathiri kipindi cha mpito.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi na kuhaririwa na Laillah Mohammed